62. Je, ninaweza kudai Mwajiri wakati sina Mkataba wa Maandishi?

Utangulizi

Ndugu msomaji wa makala za Uchambuzi wa Sheria ambapo tumekuwa tukiichambua Sheria ya Kazi. Katika makala iliyopita  tuliangalia endapo mfanyakazi anaweza kuwa na madai kwa mwajiri wake pasipo kuwa na mkataba wa maandishi. Tumeona juu ya hatua ya kwanza ya uwepo wa dhana ya mahusiano ya kiajira. Leo tunaangalia hatua nyingine ambayo mfanyakazi anaweza kuchukua. Karibu tujifunze.

Hatua ya 2

Tathmini muda wa ajira (umefanya kazi kwa muda gani?)

Suala la muda katika mahusiano ya kiajira ni la muhimu sana kwa wafanyakazi na waajiri. Wafanyakazi wasio na mkataba si wengi wenye kukumbuka siku ya kuajiriwa.

Mfanyakazi na mwajiri hakikisha ya kwamba unakumbuka siku ya kuanza kazi kwani ina sehemu kubwa katika maamuzi juu ya haki anazostahili mfanyakazi au madai anayopaswa kulipa mwajiri.

Mfumo wa madai ya haki za kiajira kwa mfanyakazi aliyefanya kazi chini ya kipindi cha miezi 6 ni tofauti na yule aliyefanya kazi zaidi ya miezi 6. Hali kadhalika mfanyakazi aliyefanya kazi kwa kipindi zaidi ya miezi 12 ana aina ya haki tofuauti na yule aliye chini ya muda huo. Hivyo ni muhimu sana kwa mfanyakazi na hata mwajiri ambaye hajatoa mkataba kujua ni lini mfanyakazi alianza kazi.

Madai ya Mfanyakazi chini ya Miezi 6

Endapo mwajiri atamwachisha mfanyakazi ajira yake huku kipindi cha ajira hiyo kikiwa chini ya miezi 6 mfanyakazi bado anayo haki na sababu za kufungua madai dhidi ya mwajiri pale mwajiri aliposhindwa kuwa na sababu za msingi au kufuata utaratibu wa haki.

Madai yanayoweza kufunguliwa na mfanyakazi aliyeachishwa kazi chini ya miezi 6 dhidi ya mwajiri ni fidia dhidi ya kuvunjiwa mkataba.

Napenda ieleweke hapa kuwa neno ‘mkataba’ halina maana ya makubaliano yaliyoandikwa tu bali hata makubaliano ya mdomo baina ya pande mbili, sheria inayatambua kama mkataba. Hivyo, mfanyakazi anayo haki na uwezo wa kupinga kitendo cha kusitishwa kwa ajira yake ambayo aliingia na mwajiri mkataba wa maneno.

Katika kufungua shauri au mgogoro wa kiajira, mfanyakazi atapaswa kueleza ni lini alianza kazi na lini alipata taarifa ya kusitishwa kwa ajira yake na pia aina ya mgogoro wake ni suala la kuvunjwa kwa mkataba wa ajira ambao ulifanyika kwa mdomo. Madai haya yanaweza kufunguliwa na mfanyakazi aliyefanya kazi chini ya miezi 6.

Sheria ya Kazi na Ajira inaweka zuio kwa wafanyakazi wote walioachishwa kazi chini ya miezi 6 kudai kuachishwa kazi ‘isivyo halali’ yaani ‘Unfair termination’. Hivyo iwapo mfanyakazi aliyeachishwa kazi chini ya miezi 6 atafungua mgogoro kudai ‘kuachishwa isivyo halali’ au ‘unfair termination’ basi mgogoro huo utatupiliwa mbali na Tume.

Madai ya mfanyakazi zaidi ya miezi 6

Sheria ya Kazi na Ajira inamwezesha mfanyakazi aliyefanya kazi kwa mwajiri zaidi ya miezi 6 kufungua madai ya ‘kusitishwa ajira isivyo halali’ au ‘unfair termination’ au hata kupinga kwa ‘kuvunjwa mkataba’ au ‘breach of contract’. Sheria ya kazi inampa wigo mpana zaidi mfanyakazi aliyefanya kazi kwa kipindi cha zaidi ya miezi 6 namna bora ya kuleta madai yake mbele ya Tume.

Ni dhahiri ya kwamba kigezo cha mkataba wa maandishi hakiwezi kumzuia mfanyakazi kudai dhidi ya mwajiri endapo usitishwaji wa ajira haukufuata utaratibu bila kujali muda aliofanya kazi kwa mwajiri husika. Ni muhimu sana kwa pande zote kuwa na ufahamu juu ya muda wa mahusiano ya kiajira.

Kwa ushauri zaidi usisite kuwasiliana nasi kama inavyoelekezwa hapo chini katika makala hii.

Kumbuka ‘kutokujua sheria si utetezi iwapo utatenda kosa lolote tafuta maarifa sahihi ya kisheria yakusaidie kufanya maamuzi sahihi kila siku.

Nakutakia siku njema ndugu yangu.

Mwandishi Isaack Zake ni wakili wa Mahakama Kuu ya Tanzania wa kujitegemea anayefanya katika ofisi za Uwakili Zake Advocates zilizopo Dar es Salaam, Mtaa wa Bibi Titi Mohamed. Isaack Zake anatoa elimu ya kisheria, ushauri wa kisheria na usimamizi wa kisheria katika maeneo mbalimbali kama Sheria za Kazi, Mirathi, Ndoa, Mikataba na Biashara. Kwa ushauri usisite kuwasiliana naye kwa 0713 888 040 na email zakejr@gmail.com