63. Ukomo wa Muda kwa Madai ya Mshahara
Utangulizi
Ndugu msomaji wa makala za Uchambuzi wa Sheria ambapo tumekuwa tukiichambua Sheria ya Kazi. Kumekuwa na tatizo la waajiri kutokulipa mishahara kwa wakati au kumsimamisha mfanyakazi pasipo mshahara. Wafanyakazi hawachukui hatua yoyote katika kufuatilia madai haya. Leo tunaangalia juu ya ukomo wa muda kwa madai ya mshahara. Karibu tujifunze.
Ukomo wa Muda
Sheria ya Ajira imeweka wazi juu ya ukomo wa muda katika kufuatilia haki au madai yatokanayo na mgogoro wa kikazi. Sheria ya Ajira inaeleza juu ya kufungua shauri au mgogoro wa kazi ndani ya siku 30 endapo madai yatahusika na usitishwaji wa ajira.
Hatahivyo kwa madai mengine yoyote yatokanayo na migogoro ya kiajira, sheria inaongoza kuwa mtu au upande usioridhika unapaswa kufungua mgogoro mbele ya Tume ndani ya siku 60.
Hii ni kwa mujibu wa Kanuni ya 10 (1) na (2) ya Taasisi za Kazi (Usuluhishi na Uamuzi) T.S. Na.64/2007 ambayo inasema
(1) ‘Mgogoro kuhusu uhalali wa kumwachisha kazi mfanyakazi lazima ukatiwe rufaa kwenye Tume ndani ya siku thelathini kuanzia tarehe ya kumwachisha kazi au tarehe ambayo mwajiri ametoa uamuzi wa mwisho wa kumwachisha kazi au kuthibitisha uamuzi wa kumwachisha kazi’
(2) ‘Migogoro mingine yote iwasilishwe kwenye Tume ndani ya siku sitini kuanzia tarehe ya kuanza mgogoro’
Kwa mantiki ya vifungu hivi vya sheria mgogoro wa kuachishwa kazi ni lazima upingwe ndani ya siku 30 huku migogoro mingine yote inapaswa kuwasilishwa mbele ya Tume ndani ya siku 60 tangu tarehe ya kuanza mgogoro.
Mgogoro wa madai ya Mishahara
Mbali na mgogoro wa kusitishwa kwa ajira ya mfanyakazi, mgogoro mwengine ambao umekuwa ukiwakumba waajiriwa na waajiri ni suala la madai ya mishahara. Wapo wafanyakazi wanaodai mishahara zaidi ya miezi 3 au 5 au wengine mpaka miezi 12 hawajalipwa mishahara yao. Wengi hubaki na matumaini ya kuwa ipo siku mishahara husika italipwa na mwajiri.
Hatahivyo, sheria inamtaka mfanyakazi kuchukua hatua za mapema kulinda haki yake ya mshahara au madai yake. Sheria inaongoza kuwa hatua zinapaswa kuchukuliwa ndani ya siku 60 tangu mwajiri aliposhindwa kulipa mshahara. Kushindwa kuchukua hatua mapema kunaweza kuhatarisha kupoteza kabisa haki ya mfanyakazi.
Tunaweza kuona kosa hili la wafanyakazi kupitia mgogoro wa kikazi baina ya Pee Pee (T) Limited na Shabani Juma Omari, Marejeo Na.33 ya 2013 mbele ya Jaji Aboud.
Shabani Juma Omari (Mfanyakazi/mlalamikaji) alifungua mgogoro wa kupinga kusitishwa ajira isivyo halali mbele ya Tume. Tume ilisikiliza shauri na kuona mwajiri (mlalamikiwa/ Pee Pee (T) Limited) alizingatia sababu na utaratibu wa kusitisha ajira. Hatahivyo Tume iliona kuwa Mfanyakazi anastahili kulipwa mishahara kipindi alichokuwa anashtakiwa kwa kosa la jinai kwani alipaswa kuwa amesimamishwa kazi na kulipwa mshahara mzima. Hivyo Tume ikaamuru mfanyakazi kulipwa kiasi cha Tsh.1,260,000/- ikiwa ni mishahara ya miezi 6 wakati mlalamikaji akiwa anakabiliwa na tuhuma za kijinai. Mwajiri hakuridhika na uamuzi wa Tume na hivyo kuomba marejeo mbele ya Mahakama Kuu ya Kazi. Mahakama ya Kazi mara baada ya kupitia ushahidi na nyaraka zilizowasilishwa ilitengua uamuzi wa Tume kwa kuwa haukuzingatia matakwa ya muda. Mahakama ya Kazi iliona kuwa mfanyakazi alichelewa kufungua shauri kuhusiana na madai ya mishahara kwani ukomo wake ni siku 60 tangu mwajiri alipoacha kulipa mishahara husika.
Ndugu msomaji kwa mfano huo tunaweza kuona ya kwamba mfanyakazi anaweza kupoteza haki yake ya madai ya msingi kwa kutokuzingatia muda ambao sheria imeweka. Ni muhimu kufahamu haki yako na juu ya muda unaoweza kutumia kudai haki husika.
Endelea kufuatilia makala nyingine tuendelee kujifunza hatua za kuchukua endapo suala unalodai tayari muda umepita.
Kwa ushauri zaidi usisite kuwasiliana nasi kama inavyoelekezwa hapo chini katika makala hii.
Kumbuka ‘kutokujua sheria si utetezi iwapo utatenda kosa lolote’ tafuta maarifa sahihi ya kisheria yakusaidie kufanya maamuzi sahihi kila siku.
Nakutakia siku njema ndugu yangu.
Mwandishi Isaack Zake ni wakili wa Mahakama Kuu ya Tanzania wa kujitegemea anayefanya katika ofisi za Uwakili Zake Advocates zilizopo Dar es Salaam, Mtaa wa Bibi Titi Mohamed. Isaack Zake anatoa elimu ya kisheria, ushauri wa kisheria na usimamizi wa kisheria katika maeneo mbalimbali kama Sheria za Kazi, Mirathi, Ndoa, Mikataba na Biashara. Kwa ushauri usisite kuwasiliana naye kwa 0713 888 040 na email zakejr@gmail.com