65. Ni lazima Mwajiri kutoa mkataba wa maandishi kwa mfanyakazi


Utangulizi

Ndugu msomaji wa makala za Uchambuzi wa Sheria ambapo tumekuwa tukiichambua Sheria ya Kazi. Katika makala zilizotangulia tumeangalia mambo mbalimbali yanayohusu sheria za kazi na namna zinavyoathiri mahusiano baina ya mfanyakazi na mwajiri. Leo tunakwenda kuangalia sehemu ya mabadiliko ya sheria ambayo inamtaka mwajiri kuhakikisha anatoa mkataba wa maandishi kwa mfanyakazi. Karibu tujifunze.

Mkataba wa ajira

Kama tulivyoona katika makala za awali juu ya mahusiano ya kiajira yanaweza kufanyika kwa mdomo au kwa maandishi. Sheria ya kazi na ajira ilikuwa inaruhusu makubaliano ya kiajira kufanyika kwa mdomo na iliweka ulazima kwa wafanyakazi wanaofanya kazi nje ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuwa na mikataba ya maandishi.

Kifungu cha sheria kinachohusiana na masuala ya mkataba ni kifungu cha 14 (2) cha Sheria ya Kazi ambacho kabla ya mabadiliko ya sheria kilikuwa  kinasema

‘A contract with an employee shall be in writing if the contract provides that the employee is to work outside the United Republic of Tanzania’

Hali hii iliwalazimu tu waajiri ambao wako nje ya Tanzania kuhakikisha mkataba wa ajira kwa wafanyakazi unakuwa kwa maandishi.

Waajiri wote walio ndani ya Tanzania walikuwa na hiyari ya kuchagua kuandika mikataba au kuwa na makubaliano ya mdomo na waajiriwa.

Mwanya huu wa ukosefu au hiyari ya kuandika mkataba wa ajira au la ulisababisha ukosefu mkubwa sana wa haki za waajiriwa na hivyo kuwa katika hali ya wasi wasi na ajira zao.

Bunge la Jamhuri ya Muungano kwa kuona umuhimu wa mkataba wa maandishi kwa wafanyakazi wote liliona vyema kupitia kifungu hicho cha sheria na kufanya mabadiliko ambayo yaliwahusisha na waajiriwa wote wanaofanya kazi ndani ya Tanzania kuwa na haki ya mkataba wa maandishi.

Kifungu cha 14 (2) cha Sheria ya Kazi, Sura ya 366 Toleo 2018 kimefanyiwa mabadiliko na kusema

‘A contract with an employee shall be in writing if the contract provides that the employee is to work within or outside the United Republic of Tanzania’

Kwa tafsiri nyepesi kifungu hiki kinasema

‘Mkataba na mfanyakazi ni lazima uwe wa maandishi bila kujali mfanyakazi huyo atafanya kazi zake ndani ya Tanzania au nje ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania’

Hii ni habari nzuri kwa wafanyakazi ambao kwa muda mrefu maslahi yao ya kiajira hayakuwekwa au kuanishwa katika mikataba ya maandishi.

Kumekuwa na ugumu au uzito wa waajiri wengi kutoa mikataba kwa wafanyakazi wao pasipo sababu za msingi. Mabadiliko haya ya kisheria yanamlazimisha mwajiri kuhakikisha anatoa mikataba ya maandishi kwa wafanyakazi wake wote.

Athari za mwajiri kutotoa mkataba wa maandishi

Sheria ya Kazi na Ajira imeweka wazi juu ya athari kwa mwajiri kutokuzingatia matakwa ya sheria ya kutoa mkataba wa maandishi. Endapo mwajiri atabainika kukaidi kutoa mkataba wa ajira wakati wa uchunguzi wa Maafisa wa Kazi atalazimika kutoa mikataba husika au kulipa faini au kufikishwa mahakamani kwa kukaidi sheria ambapo akipatikana na hatia anaweza kulipa faini mpaka kiasi kisichozidi Million 5 au kifungo kisichopungua miezi 3.

Hitimisho

Ni muhimu sana kwako mwajiri kuzingatia sheria za kazi na ajira kwa kuhakikisha waajiriwa wako wanayo mikataba ya maandishi, hiyo ni kwa faida yako kama mwajiri na pia kwa wafanyakazi wako.

‘Zingatia sheria mapema kabla athari za kutokuzingatia hazijakukuta’

Kumbuka ‘kutokujua sheria si utetezi iwapo utatenda kosa lolote tafuta maarifa sahihi ya kisheria yakusaidie kufanya maamuzi sahihi kila siku.

Nakutakia siku njema ndugu yangu.

Mwandishi Isaack Zake ni wakili wa Mahakama Kuu ya Tanzania wa kujitegemea anayefanya katika ofisi za Uwakili Zake Advocates zilizopo Dar es Salaam, Mtaa wa Bibi Titi Mohamed. Isaack Zake anatoa elimu ya kisheria, ushauri wa kisheria na usimamizi wa kisheria katika maeneo mbalimbali kama Sheria za Kazi, Mirathi, Ndoa, Mikataba na Biashara. Kwa ushauri usisite kuwasiliana naye kwa 0713 888 040 na email zakejr@gmail.com