66. Hitaji la Kukusanya taarifa za Mfanyakazi

Utangulizi

Ndugu msomaji wa makala za Uchambuzi wa Sheria ambapo tumekuwa tukiichambua Sheria ya Kazi. Katika makala zilizotangulia tumeangalia mambo mbalimbali yanayohusu sheria za kazi na namna zinavyoathiri mahusiano baina ya mfanyakazi na mwajiri. Leo tunakwenda kuangalia juu ya umuhimu wa kukusanya taarifa za mfanyakazi. Karibu tujifunze.

Umuhimu wa taarifa

Taarifa katika mahusiano yoyote ni kitu cha msingi sana kuzingatiwa na kuhakikisha kuwa una taarifa sahihi. Kadhalika kwenye mahusiano ya kiajira, ni kazi ya mwajiri kuhakikisha anazo taarifa zote muhimu kuhusiana na mfanyakazi/mwajiriwa wake.

Mahusiano mengi ya kiajira huendeshwa kwa mazoea pasipo mwajiri kuchukua jukumu hili muhimu la kupata taarifa sahihi na toshelevu kuhusiana na mwajiriwa. Hali hii hupelekea migogoro isiyo ya lazima na kumweka mwajiri katika hali isiyo nzuri.

Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini, Na.6/2004 katika Kifungu cha 15 kinaeleza wazi wajibu wa mwajiri kuhakikisha anampatia mwajiriwa maelezo ya kumbukumbu kwa maandishi  yanayohusu mambo yafuatayo;

  • Jina, umri, anwani ya kudumu na jinsi ya mwajiriwa
  • Mahali alipoajiriwa
  • Maelezo ya kazi
  • Tarehe ya kuanza kazi
  • Aina ya kazi na muda wa mkataba
  • Sehemu ya kazi
  • Saa za kazi
  • Ujira, njia ya ukokotoaji wake, na maelezo ya kina kuhusu mafao yoyote au malipo ya kitu/mali; na
  • Mambo mengine yaliyoelezwa

Waajiri wengi hawaoni umuhimu wa kuandaa maelezo haya na wanaingia makubaliano na waajiriwa pasipo kutoa maelezo au kupata taarifa za msingi za waajiriwa wao.

Waajiri wengi wanaishia kujua jina la mfanyakazi na kiasi anacholipwa ikiwa kwa kutwa au juma au mwezi.

Changamoto ya ukosefu wa taarifa muhimu

Katika matakwa ya kisheria kwa mwajiri kuhakikisha anatoa maelezo ya kiajira kwa mwajiriwa kuna hitaji la kupata anwani ya kudumu. Waajiri wengi hawafuatilii ni wapi waajiriwa wao wanaishi au wanaweza kupatikana endapo kunajitokeza tatizo lolote.

Tumeshuhudia waajiri wanapata changamoto sana pale matatizo yanatokea kazini na mwajiriwa anatoroka au haonekani kazini kwa muda mrefu, mwajiri anakosa hatua za kuchukua kwa sababu hakufanya wajibu wake ipasavyo wa kukusanya taarifa za mwajiriwa. Waajiri wanaishia tu kuwa na namba ya simu ya mfanyakazi ambayo si ya kutumaini sana kwani mfanyakazi anaweza akaamua asipatikane.

Panapotokea suala la wizi au uharibifu wa mali, mwajiri anakosa namna ya kuanza kushughulika na mwajiriwa husika kwa sababu hana taarifa za kudumu kuhusiana na mwajiriwa huyo. Wengi wanakuwa na sanduku la posta lakini katika nyakati hizi si wengi wanasoma barua.

Hatua za kuchukua

Ni muhimu kwa mwajiri kuwa na mkakati wa kukusanya taarifa muhimu za wafanyakazi wake ili awe na mazingira mazuri ya kuchukua hatua endapo patajitokeza changamoto;

  • Pata majina sahihi ya mfanyakazi ambayo yapo kwenye kitambulisho cha kura au utaifa au leseni
  • Mtake mfanyakazi akupatie namba zake za simu na namba za watu wake wa karibu wasiopungua watatu.
  • Mtake mfanyakazi akuletee barua ya utambulisho kutoka kwenye serikali ya mtaa anaoishi ikimtambulisha kama mkazi wa eneo fulani, na endapo atahama basi atoe taarifa.
  • Chukua hatua ya kutembelea mfanyakazi wako ujue mahali anapokaa au uwe na utaratibu wa kuhakikisha walau maafisa wa ofisi yako wanafahamiana wanapoishi
  • Tengeneza fomu maalum kwa ajili ya kukusanya taarifa zote muhimu unazotaka kutoka kwa mfanyakazi wako ambayo anapaswa kuijaza na kutia sahihi yake.

Hitimisho

Mahusiano ya kiajira pasipo kufahamiana huwa yanazaa hali ya kutokuaminiana na hatimaye kusababisha migogoro isiyo ya lazima. Ni kazi ya mwajiri kuhakikisha anawajua wafanyakazi wake vizuri ili kuweza kuchukua hatua stahiki pale zinapohitajika. Hakikisha unakusanya taarifa muhimu za mfanyakazi pindi tu anapoanza kazi katika ofisi yako na pale zitakapobadilika upate taarifa mapema.

Kumbuka ‘kutokujua sheria si utetezi iwapo utatenda kosa lolote tafuta maarifa sahihi ya kisheria yakusaidie kufanya maamuzi sahihi kila siku.

Nakutakia siku njema ndugu yangu.

Mwandishi Isaack Zake ni wakili wa Mahakama Kuu ya Tanzania wa kujitegemea anayefanya katika ofisi za Uwakili Zake Advocates zilizopo Dar es Salaam, Mtaa wa Bibi Titi Mohamed. Isaack Zake anatoa elimu ya kisheria, ushauri wa kisheria na usimamizi wa kisheria katika maeneo mbalimbali kama Sheria za Kazi, Mirathi, Ndoa, Mikataba na Biashara. Kwa ushauri usisite kuwasiliana naye kwa 0713 888 040 na email zakejr@gmail.com