67. Hitaji la Kuajiri

Utangulizi

Ndugu msomaji wa makala za Uchambuzi wa Sheria ambapo tumekuwa tukiichambua Sheria ya Kazi. Katika makala zilizotangulia tumeangalia mambo mbalimbali yanayohusu sheria za kazi na namna zinavyoathiri mahusiano baina ya mfanyakazi na mwajiri. Leo tunakwenda kujifunza kanuni mbalimbali ambazo mwajiri anapaswa kuzingatia pale anapokusudia kuajiri mfanyakazi. Mfululizo huu wa makala utamsaidia mwajiri kujua vipaombele vyake na mambo ya msingi kufuata wakati anafanya maamuzi ya kuajiri. Leo tunakwenda kujifunza Kanuni ya kwanza inayohusu Hitaji la Kuajiri. Karibu tujifunze.

Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini

Kama tunavyofahamu mahusiano ya kiajira yanaongozwa na Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini, Na.6 ya 2004 pamoja na Sheria ya Taasisi za Kazi, Na.7 ya 2004. Msingi wa matumizi ya sheria hizi ni pale yanapojitokeza mahusiano ya kiajira baina ya mwajiri na mwajiriwa. Hivyo ni muhimu sana kwa pande zote kufahamu misingi na kanuni zinazoweza kuwasaidia mahusiano ya kiajira yaendeshwe kwa mujibu wa sheria.

Mwajiri anao wajibu mkubwa wa kuhakikisha matakwa ya Sheria hizi za Ajira yanatekelezwa kikamilifu. Hivyo katika kuhakikisha mwajiri anajengewa uwezo wa kufuata sheria, kanuni na mazoea ya masuala ya ajira ni muhimu kujua hatua au kanuni anazopaswa kuzingatia pindi anapokusudia kuanzisha mahusiano ya kiajira na mwajiriwa au waajiriwa.

Kanuni  1

Hitaji la Kuajiri

Je, mwajiri au taasisi inalo hitaji la kuajiri kwa wakati huu?

Hili ni swali muhimu sana kwa mwajiri au taasisi inayokusudia kutoa ajira katika kipindi husika kujiuliza kwanza endapo ipo sababu au zipo sababu za msingi za kuajiri.

Kumekuwa na tabia ya baadhi ya waajiri kutokuzingatia kwa umakini wa swali hili la msingi na kujikuta kuajiri baadhi ya watu au kutengeneza nafasi za ajira ambazo kwa namna yoyote haziwezi kuleta tija, manufaa na ufanisi mahali pa kazi. Aina ya waajiri hawa hawana msingi wa kufanya maamuzi yao ya kuajiri bali wanafanya kwa mhemuko au uhusiano walio nao na wale wanaokusudiwa kuajiriwa. Hali hii kama tutakavyokuja kuona inaleta changamoto zaidi katika mahusiano ya kiajira.

Msingi sahihi wa kuajiri au kutengeneza nafasi ya ajira ni lazima uzingatie muundo wa taasisi husika unahitaji mtu wa namna gani mwenye kuleta tija kiasi gani. msingi wa kuajiri unategemea maono ya taasisi, dhima au dhamira na malengo ya taasisi (vision, mission and goals). Bila kuzingatia misingi hii mwajiri anaweza kujikuta anaajiri aina ya watu kutegemea na vigezo vya kinasaba, kijamii, au hata kidini pasipo kuzingatia vigezo halisi na hivyo kusababish migogoro baada ya muda.

Ikumbukwe kuwa suala la kuajiri linahusisha kuongeza gharama za uendeshaji wa taasisi husika na kuongeza uwajibikaji wa mwajiri katika kuhakikisha matakwa yote ya kisheria kuhusiana na ajira yanazingatiwa kikamilifu, hivyo ni lazima uhakikishe kuna sababu za msingi na halali kuajiri mtu kama vile sheria inavyotaka pindi unapomwachisha mtu ajira uwe na sababu za msingi na halali.

Mambo ya msingi ya kuzingatia

Katika suala la kuajiri au kutengeneza nafasi ya ajira katika taasisi au mwajiri binafsi ni lazima azingatie mambo haya muhimu

  • Je, taasisi ina hitaji la mfanyakazi/mwajiriwa?
  • Je, ni nini maono, dhamira na malengo ya taasisi?
  • Je, kitu gani cha thamani taasisi inatarajia kutoka kwa mwajiri anayetegemewa kuajiriwa katika nafasi husika?
  • Je, taasisi ina uwezo au ina utayari wa kutimiza masharti au matakwa ya sheria kuhusiana na mahusiano ya kiajira?

Maswali haya yote yanapaswa kujibiwa kabla ya kutangaza au kuonesha nia ya kuajiri mfanyakazi husika. Waajiri wengi wanatengeneza nafasi huku tayari wana mtu au watu ambao wanakusudia kuwaajiri katika nafasi hizo. Mfumo huo wa kuajiri kwa sababu tayari yupo mtu au watu waliokusudiwa katika nafasi hauleti tija kwa mwajiri bali unakaribisha migogoro muda si mrefu mahali pa kazi.

Ni muhimu sana mwajiri kuzingatia hatua hii ya kwanza kwani ndio itaamua aina ya mahusiano ya kiajira baina ya mwajiri na mwajiriwa na ndio itaonesha endapo kutakuwa na tija, ufanisi na manufaa au itazalisha balaa mahali pa kazi.

Endelea kufuatana nasi tunapoendelea kujadili Kanuni hizi za msingi za kuzingatia kabla ya kuajiri.

Kumbuka ‘kutokujua sheria si utetezi iwapo utatenda kosa lolote tafuta maarifa sahihi ya kisheria yakusaidie kufanya maamuzi sahihi kila siku.

Nakutakia siku njema ndugu yangu.

Mwandishi Isaack Zake ni wakili wa Mahakama Kuu ya Tanzania wa kujitegemea anayefanya katika ofisi za Uwakili Zake Advocates zilizopo Dar es Salaam, Mtaa wa Bibi Titi Mohamed. Isaack Zake anatoa elimu ya kisheria, ushauri wa kisheria na usimamizi wa kisheria katika maeneo mbalimbali kama Sheria za Kazi, Mirathi, Ndoa, Mikataba na Biashara. Kwa ushauri usisite kuwasiliana naye kwa 0713 888 040 na email zakejr@gmail.com