68. Fanya Maamuzi juu ya aina ya Mkataba wa Ajira
Utangulizi
Ndugu msomaji wa makala za Uchambuzi wa Sheria ambapo tumekuwa tukiichambua Sheria ya Kazi. Katika makala zilizotangulia tumeangalia mambo mbalimbali yanayohusu sheria za kazi na namna zinavyoathiri mahusiano baina ya mfanyakazi na mwajiri. Tumeanza kujifunza kanuni mbalimbali ambazo mwajiri anapaswa kuzingatia pale anapokusudia kuajiri mfanyakazi. Makala iliyopita tujifunza Kanuni ya kwanza inayohusu Hitaji la Kuajiri. Leo tunakwenda kuangalia juu ya Kanuni ya kufanya uamuzi wa aina wa mkataba wa Ajira. Karibu tujifunze.
Mahusiano ya Kiajira ni Mkataba
Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini, Na.6 ya 2004 inatamka wazi ya kuwa mahusiano ya kiajira ni mahusiano ya kimkataba au makubaliano yanayotambuliwa kisheria baina ya mwajiri na mwajiriwa. Haijalishi kama makubaliano hayo yameandikwa kwenye mkataba au la, sheria ya ajira inatambua mahusiano ya kiajira ni mahusiano ya kimkataba.
Sheria ya Ajira inatamka wazi kupitia kifungu cha 14(2) ya kuwa mahusiano ya kiajira ni lazima yaainishwe kwenye mkataba wa maandishi. Napenda kunukuu kifungu husika;
‘A contract with an employee shall be in writing of the contract provides that the employee is to work within or outside the United Republic of Tanzania’
Kwa tafsiri ya kawaida ina maana ya kwamba mkataba na mwajiriwa ni lazima uwe katika maandishi bila kujali mwajiriwa atafanya kazi ndani au nje ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Kanuni 2
Fanya Maamuzi juu ya aina ya Mkataba
Je, ni aina gani ya mkataba wa ajira mwajiri anaokusudia kuingia na mwajiriwa?
Hili ni swali muhimu sana kwa mwajiri au taasisi ambalo linapaswa kupatiwa majibu sahihi kabla zoezi la kuajiri kuanza kufanyika. Katika makala iliyopita tumeweza kuona kuwa ni lazima mwajiri ajue endapo kuna sababu ya kuajiri au kutengeneza nafasi ya ajira katika ofisi au taasisi.
Kwa kujibu swali la Kanuni ya kwanza na kuonesha hitaji la kuajiriwa kwa mtu katika nafasi ya kazi, jambo muhimu la pili la kuzingatia ni aina ya mkataba mwajiri anaopaswa kuingia na mwajiriwa.
Sheria ya Ajira inatambua aina kuu tatu za mikataba ya ajira kama zilivyoanishwa katika Kifungu cha 14 (1) (a) – (c) cha Sheria ya Ajira ambayo napenda kunukuu;
A contract with an employee shall be of the following types- a contract for an unspecified period of time; |
a contract for a specified period of time for professionals and managerial cadre; |
a contract for a specific task. |
Kwa tafsiri ya kawaida Kifungu hiki kinaweza kutafsiriwa ya kuwa
Mkataba wa ajira na mwajiriwa utakuwa wa aina zifuatazo;
- mkataba usio wa muda maalum;
- mkataba wa muda maalum kwa kada ya wataalam na viongozi
- mkataba wa kazi maalum
Hizi ndizo aina za mikataba zinazotambuliwa na Sheria ya Ajira, mwajiri anao wajibu wa kufanya maamuzi juu ya aina ya mkataba kabla ya kutafuta mwajiriwa anayetaka kuingia naye makubaliano.
Ni muhimu kufahamu kuwa kila aina ya mkataba mwajiri anaochagua kuingia na mwajiriwa una wajibu wake kisheria. Hivyo ni lazima mwajiri afahamu mapema matokeo ya mkataba husika.
Ufafanuzi wa aina za mikataba
- Mkataba usio wa muda maalum – aina hii ya mkataba inajulikana kama mkataba wa kudumu. Mkataba huu unaanza pale mwajiriwa anaanza kazi na unaisha pale mwajiriwa anapokuwa amefikisha umri wa kustaafu kwa hiyari au lazima kwa mujibu wa sheria. Umri wa kustaafu ni miaka 55 kwa hiyari au 60 kwa lazima.
Hivyo ni muhimu kwa mwajiri kuazingatia masharti ya mkataba huu kwani kama utamwajiri mwajiriwa wa umri wa miaka 20 basi anapaswa kuwa kazini mpaka angalau miaka 35 au 40 ndipo mkataba utamalizika. Je, mwajiri kwa majukumu ya kazi au ajira unayotaka kuitoa utamuhitaji mwajiriwa kwa kipindi kisichopungua miaka 35 au 40 mfululizo?
- Mkataba wa Muda maalum – aina hii ya mkataba sheria imeweka wazi ni kwa ajili ya kada ya uongozi na wataalam mahali pa kazi. Mkataba huu unatolewa kwa kipindi maalum kama mwajiri atakavyoona inafaa, inaweza kuwa mwaka 1 au 2 au 3 au hata 5. Mwajiri anaweza kuhuisha mkataba na mwajiriwa mara baada ya mkataba kumalizika endapo ataona inafaa kufanya hivyo.
- Mkataba wa kazi maalum – hii ni aina ya mkataba ambapo mwajiri anaingia na mwajiriwa kwa ajili ya kutekeleza kazi maalum. Mwisho wa mkataba huu ni pale kazi inapokamilika. Aina ya mkataba huu imetafsiriwa katika baadhi ya mashauri na Mahakama ya Kazi kama mkataba wa siku. Aina ya mkataba huu malipo hufanyika mara baada ya kazi kumalizika na hakuna.
Kama tulivyoona hapa katika Kanuni hii ya 2 inamtaka mwajiri kufanya maamuzi aina ya mkataba anaotaka kuingia na mwajiriwa mapema zaidi kabla hajaingia katika mkataba husika.
Katika makala inayofuata tutaangalia baadhi ya faida na hasara au athari za kisheria kwa kila aina ya mkataba ambao mwajiri ataamua kuuchagua.
Endelea kufuatana nasi tunapoendelea kujadili Kanuni hizi za msingi za kuzingatia kabla ya kuajiri.
Kumbuka ‘kutokujua sheria si utetezi iwapo utatenda kosa lolote’ tafuta maarifa sahihi ya kisheria yakusaidie kufanya maamuzi sahihi kila siku.
Nakutakia siku njema ndugu yangu.
Mwandishi Isaack Zake ni wakili wa Mahakama Kuu ya Tanzania wa kujitegemea anayefanya katika ofisi za Uwakili Zake Advocates zilizopo Dar es Salaam, Mtaa wa Bibi Titi Mohamed. Isaack Zake anatoa elimu ya kisheria, ushauri wa kisheria na usimamizi wa kisheria katika maeneo mbalimbali kama Sheria za Kazi, Mirathi, Ndoa, Mikataba na Biashara. Kwa ushauri usisite kuwasiliana naye kwa 0713 888 040 na email zakejr@gmail.com