69. Athari za Kisheria kwa Uamuzi wa kuingia mkataba wa kudumu

Utangulizi

Ndugu msomaji wa makala za Uchambuzi wa Sheria ambapo tumekuwa tukiichambua Sheria ya Kazi. Katika makala zilizotangulia tumeangalia mambo mbalimbali yanayohusu sheria za kazi na namna zinavyoathiri mahusiano baina ya mfanyakazi na mwajiri. Tumeanza kujifunza kanuni  ambazo mwajiri anapaswa kuzingatia pale anapokusudia kuajiri mfanyakazi. Makala iliyopita tujifunza Kanuni ya Pili inayozungumzia kufanya uamuzi juu ya aina ya mkataba wa ajira mwajiri anaokusudia kuingia na mwajiriwa.

Leo tunaangalia athari za kisheria endapo mwajiri atafanya uamuzi wa kuingia mahusiano ya kiajira na mwajiriwa katika mkataba wa kudumu. Karibu tujifunze.

Aina za Mkataba

Kama tulivyoona katika malaka iliyopita Sheria ya Ajira inatambua aina kuu tatu za mikataba ya ajira kama zilivyoanishwa katika Kifungu cha 14 (1) (a) – (c)

Mkataba wa ajira na mwajiriwa utakuwa wa aina zifuatazo;

  • mkataba usio wa muda maalum;
  • mkataba wa muda maalum kwa kada ya wataalam na viongozi
  • mkataba wa kazi maalum

Ufafanuzi

Mkataba usio wa muda maalum – aina hii ya mkataba inajulikana kama mkataba wa kudumu. Mkataba huu unaanza pale mwajiriwa anaanza kazi na unaisha pale mwajiriwa anapokuwa amefikisha umri wa kustaafu kwa hiyari au lazima kwa mujibu wa sheria. Umri wa kustaafu ni miaka 55 kwa hiyari au 60 kwa lazima.

Athari za kisheria katika mahusiano ya mkataba wa kudumu

  • Mkataba huu wa ajira unaendelea tangu mwajiriwa alipoanza kazi mpaka atakapofikisha umri wa kustaafu kwa hiyari au kwa lazima.
  • Endapo mwajiri anakusudia kusitisha mkataba huu kabla ya umri wa kustaafu ni lazima
  • Awe na sababu halali na za msingi
  • Afuate utaratibu wa haki katika kusitisha mkataba huu
  • Sababu za msingi na halali zinazoweza kusababisha mkataba wa kudumu kusitishwa ni
  • Utovu wa nidhamu,
  • Zoezi la kupunguza wafanyakazi (retrenchment)
  • Uwezo mdogo wa utendaji wa mwajiriwa
  • Sababu za kiafya kama ugonjwa au kuumia kazini
  • Kwa sababu yoyote ile mwajiri anayotaka kuitumia kusitisha mkataba wa kudumu ni lazima afuate utaratibu uliowekwa kisheria kuhusiana na sababu husika. Mfano anataka kusitisha mkataba kutokana na utovu wa nidhamu ni lazima afuate utaratibu husika kabla ya kusitisha ajira hiyo au kusitisha kutokana na uwezo mdogo basi upo utaratibu.
  • Endapo mwajiri atashindwa kufuata utaratibu, basi mwajiriwa ana haki ya kukata rufaa mbele ya Tume au Mahakama Kuu kupinga uamuzi wa mwajiri.
  • Endapo Tume au Mahakama itaona hapakuwa na sababu halali na za msingi pamoja na utaratibu kutofuatwa basi inaweza kuamuru mwajiriwa husika KURUDISHWA KAZINI au kulipwa FIDIA kiasi kisichopungua mishahara ya miezi 12. Ieleweke Tume au Mahakama inayo mamlaka ya kutoa mishahara zaidi ya miezi 12 inategemea na namna shauri lilivyo mbele yake na ushahidi uliotolewa.

Kwa upande mwengine, endapo mwajiriwa anakusudia kusitisha ajira yake na mwajiri wake ambapo ana mkataba wa kudumu anaweza kufanya hivyo endapo

  • Atakuwa ametimiza umri wa kustaafu kwa hiyari yaani miaka 55 au umri wa kustaafu kwa lazima miaka 60
  • Ataamua kujiuzulu kazi kwa kutoa taarifa ya maandishi.

Ndugu msomaji tunaona jinsi Sheria inavyowabana waajiri katika mazingira ya kuingia makubaliano ya kudumu kiasi kinachosababisha kufuata taratibu nyingi na kuwa na sababu za msingi, wakati kwa upande mwengine mwajiriwa habanwi sana na masharti ya ajira katika mkataba huu wa kudumu.

Hitimisho

Endapo mwajiri anaamua kufanya uamuzi wa kuingia makubaliano ya mkataba wa kudumu ni lazima ajue masharti yanayoambatana na mkataba husika.

Wapo waajiri wengi wanawekeza sana kwa wafanyakazi kwa kuwapeleka mafunzo ili kuongeza ufanisi katika kazi, lakini baada ya kupata ujuzi na utaalam ambao umegharamiwa na mwajiri wafanyakazi hao hugeuka na kwenda mahali pengine kutafuta maslahi bora zaidi. Hivyo ni muhimu kuhakikisha ndani ya mikataba hiyo ya ajira vipo vipengele vitakavyolinda maslahi ya mwajiri pia.

Kumbuka ‘kutokujua sheria si utetezi iwapo utatenda kosa lolote tafuta maarifa sahihi ya kisheria yakusaidie kufanya maamuzi sahihi kila siku.

Nakutakia siku njema ndugu yangu.

Mwandishi Isaack Zake ni wakili wa Mahakama Kuu ya Tanzania wa kujitegemea anayefanya katika ofisi za Uwakili Zake Advocates zilizopo Dar es Salaam, Mtaa wa Bibi Titi Mohamed. Isaack Zake anatoa elimu ya kisheria, ushauri wa kisheria na usimamizi wa kisheria katika maeneo mbalimbali kama Sheria za Kazi, Mirathi, Ndoa, Mikataba na Biashara. Kwa ushauri usisite kuwasiliana naye kwa 0713 888 040 na email zakejr@gmail.com