73. Vigezo vya ziada kwa Mwajiriwa bora
Utangulizi
Ndugu msomaji wa makala za Uchambuzi wa Sheria ambapo tumekuwa tukiichambua Sheria ya Kazi. Katika makala zilizotangulia tumeangalia mambo mbalimbali yanayohusu sheria za kazi na namna zinavyoathiri mahusiano baina ya mfanyakazi na mwajiri. Tumeanza kujifunza kanuni mbalimbali ambazo mwajiri anapaswa kuzingatia pale anapokusudia kuajiri mfanyakazi. Makala iliyopita tulianza kujifunza Kanuni ya tatu juu ya Namna bora ya kupata mwajiriwa mwenye vigezo.
Leo tunakwenda kuangalia vigezo vya ziada vya kupata mwajiriwa bora. Karibu tujifunze.
Vigezo vya Kisheria
Katika makala iliyopita tumeweza kuoana msingi wa kuweka usawa kwa watu wote ambao wananuia kujaza nafasi ya ajira iliyotangazwa mahali pa kazi. Sheria ya Ajira Kifungu cha 7 kinaeleza wazi mwajiri anapaswa kuzingatia mazingira ya usawa wakati wa kuajiri na kuepusha aina yoyote ya ubaguzi.
Hatahivyo, mwajiri ambaye ndiye anajua mahitaji ya nafasi ya ajira anayoitangaza anapaswa kuhakikisha mbali na vigezo vya kisheria anaainisha vigezo vingine vya ziada kwa lengo la kupata mwajiriwa bora zaidi miongoni mwa waombaji wengi wenye vigezo.
Vigezo vya Ziada
- Kigezo cha kitaaluma
Kigezo cha taaluma ni moja kati ya vigezo ambavyo mwajiri huwa anatumia katika kutafuta mwajiriwa wa nafasi ya kazi. Tunaona hata katika matangazo ya ajira msisitizo huwekwa sana katika taaluma za wale wanaotaka kufanya kazi husika. Hatahivyo kulingana na soko la ajira kwa sasa na wingi wa waombaji, kigezo cha taaluma kimekuwa ni rahisi kwa wengi kukifikia kwa taaluma nyingi. Watu wana taaluma na wengine wana vigezo vya kitaaluma zaidi ya vile vinavyotakiwa na mwajiri. Pamoja na msingi wake kuwa muhimu, kigezo cha kitaaluma hakipaswi kuwa pekee katika kuamua au kutokuamua mtu wa kumwajiri. Mwajiri anapaswa kuhakikisha anaangalia vigezo vingine. Wapo wengi wana vyeti lakini uwezo wa kufanya kazi haupo, tunashuhudia hivyo katika maeneo mengi ya kazi.
- Kigezo cha uzoefu
Hiki ni kigezo kingine ambacho waajiri hujaribu kupima kwa lengo la kuchagua mtu wa kuajiriwa. Kazi inaweza kutangazwa inamtaka mtu mwenye uzoefu wa kipindi kisichopungua miaka 3 – 5 katika kazi hiyo. Pamoja na umuhimu wa kigezo hiki bado kinaweza kumnyima mwajiri fursa ya kupata watu wapya wenye mawazo mapya katika kuitenda kazi husika kwa namna bora zaidi. Changamoto ya kigezo cha uzoefu inaweza kusababisha mwajiriwa kuleta au kufanya kazi kwa mazoea pasipo ubunifu.
- Kigezo cha ubunifu
Hiki ni kigezo kingine muhimu sana ambacho mwajiri anapaswa kukizingatia na kukipa kipaombele. Katika mazingira ya kazi na ushindani mkubwa duniani, kitu pekee kinachoweza kusaidia taasisi kwa haraka na tija ni kuwa na watu wenye udhubutu wa kubuni namna bora zaidi ya kutenda kazi na kuboresha mifumo kukidhi mahitaji. Ni muhimu sana mwajiri kuhakikisha anatafuta watu wenye utofauti na mazoea, watu ambao wapo tayari kufanya vitu vipya vyenye tija katika taasisi ya kazi.
- Kigezo cha uaminifu
Uaminifu katika kazi ni jambo muhimu sana la kuzingatia. Kuna mtazamo kwa baadhi ya waajiriwa kila wanapopata kazi wanatafuta fursa ya kunufaika wao kwanza kutokana na shughuli au biashara ya mwajiri. Lazima mwajiri atafute namna ya kuhakikisha anapata watu waaminifu katika shughuli anayoifanya.
- Kigezo cha ushirikiano
Mwajiriwa anayetegemea kufanya kazi kwenye taasisi au ofisi ni lazima aoneshe uwezo wa kushirikiana si tu na mwajiri bali na waajiriwa wenzake, wateja na wadau wengine katika kazi. Kama mwajiri ataajiri mtu ambaye hana namna bora ya kushirikiana na wateja tayari mwajiriwa huyo ataleta doa ambalo litaigharimu taasisi kwa muda mrefu. Sehemu ya kazi haipaswi kuwa sehemu ya migogoro bali sehemu ya kuzalisha na kufanya kazi kwa ushirikiano mkubwa kila mtu akitekeleza majukumu yake ipasavyo
- Kigezo cha kujifunza
Moja kati ya vigezo muhimu sana vitakavyomsaidia mwajiri kuhakikisha anapata mwajiriwa bora miongoni mwa wengi wenye vigezo basi ni muhimu kuangalia kigezo cha kujifunza. Wahitimu wengi wanapomaliza shule au vyuo huwa hawana muda au utayari wa kuendelea kujifunza. Wahitimu hawapati muda wa kusoma vitabu vinavyohusiana na aina ya kazi au taaluma waliyonayo, wanaishia kubaki na vyeti. Utamaduni wa watu kusoma vitabu umepotea sana ndani ya waafrika. Namna bora ya mwombaji wa ajira kujitofautisha ni kuwa na maarifa ya ziada ya kukuwezesha kuifanya kazi tofauti na wengine kwa kujisomea vitabu. Mwajiri ukitaka kujua tabia hii kama ipo kwa watu unaotaka kuwaajiri angalia CV zao utaona katika ‘hobby’ zao hakuna wanaosema wanasoma vitabu. Weka maswali kuuliza juu ya vitabu mtu alivyosoma na ikiwezekana aeleze amejifunza nini ndani ya vitabu husika.
Katika makala ijayo, tutaangalia athari za kutozingatia vigezo vya kisheria na vya ziada katika kuajiri.
Kumbuka ‘kutokujua sheria si utetezi iwapo utatenda kosa lolote’ tafuta maarifa sahihi ya kisheria yakusaidie kufanya maamuzi sahihi kila siku.
Nakutakia siku njema ndugu yangu.
Isaack Zake, Wakili
Mwandishi Isaack Zake ni wakili wa Mahakama Kuu ya Tanzania wa kujitegemea anayefanya katika ofisi za Uwakili Zake Advocates zilizopo Dar es Salaam, Mtaa wa Bibi Titi Mohamed. Isaack Zake anatoa elimu ya kisheria, ushauri wa kisheria na usimamizi wa kisheria katika maeneo mbalimbali kama Sheria za Kazi, Mirathi, Ndoa, Mikataba na Biashara. Kwa ushauri usisite kuwasiliana naye kwa 0713 888 040 na email zakejr@gmail.com