84. Lipa kiwango cha Mshahara kinachostahili

Utangulizi

Ndugu msomaji wa makala za Uchambuzi wa Sheria ambapo tumekuwa tukiichambua Sheria ya Kazi. Katika makala zilizotangulia tumeangalia mambo mbalimbali yanayohusu sheria za kazi na namna zinavyoathiri mahusiano baina ya mfanyakazi na mwajiri. Tumeanza kujifunza kanuni mbalimbali ambazo mwajiri anapaswa kuzingatia pale anapokusudia kuajiri mfanyakazi. Katika makala iliyopita tulijifunza juu ya Kanuni ya 10 inayomwelekeza mwajiri kuhakikisha anamjulisha mwajiriwa haki zake za kiajira.

Leo tunajifunza kanuni ya 11 inayohusu na kumtaka mwajiri kulipa kiwango cha Mshahara kinachostahili. Karibu tujifunze.

Kanuni ya 11

Lipa kiwango cha Mshahara kinachostahili

Sheria ya Ajira pamoja na mambo mengine imezungumzia suala la malipo ya kazi ambayo mwajiriwa anapaswa kulipwa kutokana na kazi anayoifanya.

Malalamiko yamekuwako hasa kwa waajiriwa wakidai wanalipwa mishahara midogo au wanapunjwa malipo yao kutokana na kazi wanazofanya mahali pa kazi.

Hali kadhalika waajiri nao wana malalamiko yao kuhusiana na malipo ambayo wanastahili kulipa wafanyakazi wakidai gharama za uendeshaji shughuli zao ni kubwa kutokana na masuala ya kodi na gharama nyingine hivyo wangetaka malipo ya waajiriwa ya wechini ili waweze kumudu kuendesha shughuli zao.

Kwa msingi huu Sheria ya Ajira ilikuja na suluhisho la kuhakikisha suala la malipo linakuwa na mwongozo wa kisheria kwa kuweka viwango vya chini ambavyo mwajiri anapaswa kuzingatia wakati wote kwa ajili ya kulipa wafanyakazi.

Kifungu cha 26 cha Sheria ya Ajira kinaeleza wazi juu ya ukokotoaji wa viwango vya mshahara kwa wanaofanya kazi kwa siku, wiki au mwezi. Pia Kifungu cha 27 cha Sheria ya Ajira kinaeleza juu ya wajibu wa mwajiri kumlipa mwajiriwa mshahara wake ndani ya muda uliokubaliwa na kuhakikisha malipo hayo yanaambatana na ‘salary slip’ yaani maelezo ya malipo na makato yanayohusika.

Hatahivyo, tunaweza kujua ya kuwa mwajiriwa amelipwa kiwango kinachostahili kwa kuangalia mwongozo wa Sheria ya Taasisi za Kazi, Na.7 ya 2004 ambayo imeunda Bodi ya Mishahara. Bodi hii ya Mishahara ina kazi ya kupitia viwango vya mishahara katika kila sekta ya kazi na kutoa mapendekezo kwa Waziri mwenye dhamana ya ajira kwa lengo la kutoa Tangazo la Kima cha Chini cha Mishahara. Hii ni kwa mujibu wa Kifungu cha 34 – 42 cha Sheria ya Taasisi za Kazi, Na.7 ya 2004.

Mwajiri anawajibika kulipa ‘angalau’ kiwango cha kima cha chini kilichotangazwa na Waziri katika muda husika. Hii ina maana mwajiri anaweza kulipa zaidi ya kiwango cha kima cha chini kilichoanishwa kwenye sheria kutokana na sekta husika.

Endapo makubaliano baina ya mwajiri na mwajiriwa katika mkataba wa ajira yataelekeza mwajiriwa kulipwa kiasi zaidi ya kima cha chini kilichopitishwa na Serikali, basi makubaliano hayo yatatumika kama sheria ya kumbana mwajiri kulipa kiasi hicho.

Mfano mpaka sasa viwango vya kima cha chini vilitangazwa na kuwa Sheria na kuanza kutumika tangu tarehe 1 Julai 2013 kupitia Tangazo la Serikali Na.196 la 2013. Hivyo viwango vilivyoainishwa katika kila sekta ndivyo mwajiri ‘angalau’ anapaswa kulipa waajiriwa na si chini ya hapo.

Mifano ya baadhi ya viwango vya kima cha chini wanavyopaswa kulipwa waajiriwa katika sekta mbalimbali;

  • Sekta ya afya  mshahara usipungue Tsh.132,000/- kwa mwezi
  • Sekta ya Biashara, Viwanda mshahara usipungue Tsh.100,000/- kwa mwezi
  • Sekta ya Taasisi za Kifedha mshahara usipungue Tsh.400,000/- kwa mwezi
  • Sekta ya mawasiliano mshahara usipungue Tsh.400,000/- kwa mwezi
  • Sekta ya elimu ya chekechea, msingi na sekondari za binafsi mshahara usipungue Tsh.140,000/- kwa mwezi
  • Sekta ya wafanyakazi wa nyumbani mshahara usipungue Tsh.80,000/- kwa mwezi kwa wafanyakazi wasiolala katika nyumba wanayofanya kazi na usipungue Tsh.40,000/- kwa mwezi kwa wafanyakazi ambao wanakaa katika nyumba husika.

Hii ni baadhi tu ya mifano ya maeneo mbalimbali ya kisekta ambapo kima cha chini kimeainishwa.

Eneo ambalo wamekuwa wakiathiriwa sana na kutolipwa mishahara stahili ni wanaofanya katika kazi za nyumbani. Waajiri wengi hatuwatendei haki wafanyakazi hawa. Mara nyingi mishahara yao hailipwi kabisa au hulipwa chini ya kiwango. Kama na sisi tumeajiriwa mahali tunalalamika juu ya kupunjwa mishahara ni lazima kujikagua, je, tunalipa tuliowaajiri inavyostahili?

Ieleweke ya kuwa mishahara hii sio ukomo au mwongozo wa mwajiri kulipa hivi bali ni lazima aangalie suala la vigezo na utaalam wa wale waajiriwa. Pia mahali pengine pa ajira kuna madaraja ya kupanga namna mishahara inavyopaswa kulipwa kwa usawa na haki.

Muhimu kuhakikisha ya kuwa waajiriwa wanapata stahili zao kama sheria inavyoelekeza.

Mwajiri anayelipa chini ya kima cha kisheria anatenda kosa ambalo anaweza kushtakiwa na kulipa faini na kisha kumrudishia fidia mwajiriwa mapunjo yote yaliyofanyika kwa kipindi chote cha ajira. Hivyo ni muhimu kuhakikisha unalipa kwa mujibu wa sheria na mkataba wa ajira ulioingia na mwajiriwa.

Kumbuka ‘kutokujua sheria si utetezi iwapo utatenda kosa lolote tafuta maarifa sahihi ya kisheria yakusaidie kufanya maamuzi sahihi kila siku.

Nakutakia siku njema ndugu yangu.

Isaack Zake, Wakili

Mwandishi Isaack Zake ni wakili wa Mahakama Kuu ya Tanzania wa kujitegemea anayefanya katika ofisi za Uwakili Zake Advocates zilizopo Dar es Salaam, Mtaa wa Bibi Titi Mohamed. Isaack Zake anatoa elimu ya kisheria, ushauri wa kisheria na usimamizi wa kisheria katika maeneo mbalimbali kama Sheria za Kazi, Mirathi, Ndoa, Mikataba na Biashara. Kwa ushauri usisite kuwasiliana naye kwa 0713 888 040 na email zakejr@gmail.com