83. Mjulishe Mwajiriwa haki zake za kiajira

Utangulizi

Ndugu msomaji wa makala za Uchambuzi wa Sheria ambapo tumekuwa tukiichambua Sheria ya Kazi. Katika makala zilizotangulia tumeangalia mambo mbalimbali yanayohusu sheria za kazi na namna zinavyoathiri mahusiano baina ya mfanyakazi na mwajiri. Tumeanza kujifunza kanuni mbalimbali ambazo mwajiri anapaswa kuzingatia pale anapokusudia kuajiri mfanyakazi. Makala iliyopita tulijifunza Kanuni ya 9 inayomtaka mwajiri kuhakikisha anamjulisha mwajiriwa Sera zinazohusu ajira katika taasisi yake.

Leo tunaendelea kujifunza juu ya Kanuni ya 10 inayomwelekeza mwajiri kuhakikisha anamjulisha mwajiriwa haki zake za kiajira. Karibu tujifunze.

Kanuni ya 10

Haki za Kiajira

Sheria ya ajira na mahusiano kazini inaongoza mwajiri na mwajiriwa katika majukumu wanayopaswa kufanya ikibainisha haki na wajibu wa kila upande. Wajibu wa mwajiriwa ni kufanya kazi kwa mujibu wa taratibu zilizowekwa na mwajiri pamoja na sheria. Wajibu wa mwajiri ni kuhakikisha anatimiza masharti ya kisheria kuhusiana na haki za mwajiriwa.

Kulingana na mfumo wa mahusiano kuonesha kama mwajiri ana nguvu zaidi ya mwajiriwa katika mchakato mzima wa kazi, hivyo sheria ya ajira imeweka wajibu mkubwa kwa mwajiri kuhakikisha anamfahamisha na kumhakikishia mwajiriwa juu ya utekelezaji wa haki za kiajira.

Sheria imeenda mbali zaidi kwa kutamka wazi kuwa mwajiri ni lazima aweke tangazo au fomu inayoonesha haki za kiajira ambazo mwajiriwa anazipata kwa kuwa ni mwajiriwa.

Kifungu cha 16 cha Sheria ya Ajira kinaeleza

‘Every employer shall display a statement in the prescribed form of the employee’s rights under this Act in a conspicuous place’

Kwa tafsiri nyepesi ina maana kuwa kila mwajiri anawajibika kutangaza au kuweka kwenye ubao wa matangazo juu ya haki za mwajiriwa zinazobainishwa chini ya Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini.

Hitaji hili ya kisheria pia limesisitizwa na Kanuni za Sheria ya Ajira inayojulikana kama ‘Employment and Labour Relations (General) Regulations, G.N. No.47 of 2017, kupitia Kifungu cha 12 ikianisha fomu maalum ya Haki za Mwajiriwa mahali pa kazi.

Fomu hiyo maalum inaainisha haki za kiajira kama ifuatavyo;

  • Haki ya kujiunga na kujumuika kwenye chama cha wafanyakazi
  • Haki ya kupewa mkataba wa ajira
  • Haki ya likizo ya mwaka
  • Haki ya likizo ya uzazi kwa wanawake na wanaume, likizo ya ugonjwa
  • Haki ya kupata cheti cha utumishi pindi ajira itakapokoma
  • Haki ya kupata ujira na maelezo ya malipo yaani ‘salary slip’
  • Haki ya kulipwa malipo ya kazi kwa saa za ziada na posho ya kazi za usiku
  • Haki ya mapumziko kwa siku na mwisho wa wiki
  • Haki ya kulipwa gharama za usafiri mpaka eneo aliloajiriwa mwajiriwa
  • Haki ya kulipwa posho ya siku tangu siku ya kuachishwa kazi mpaka siku ya kurudishwa mahali alipoajiriwa mfanyakazi na familia yake
  • Haki nyingine ambazo zimeainishwa katika sheria na mkataba wa ajira

Hizi ni baadhi tu ya haki ambazo mwajiri anapaswa kuhakikisha zimewekwa kwenye fomu maalum kama ilivyoelekeza Sheria ya Ajira na kisha kubandikwa katika eneo lililo wazi kwa kila mfanyakazi kuweza kusoma haki hizo na kuzitekeleza kikamilifu.

Waajiri wengi hawazifahamu haki hizi wala hitaji la kisheria la kuhakikisha zimewekwa mahali pa wazi kwa kila mfanyakazi kusoma. Sheria ya Ajira inamtaka mwajiri kuhakikisha haki hizi zipo wazi, kinyume na hapo endapo itabainika mwajiri hajaweka tangazo hili, maafisa wa kazi wanaweza kumchukulia mwajiri hatua za kisheria kwa kukiuka sheria. Ni vyema kwa mwajiri kuzingatia si tu kubandika tangazo la haki za mfanyakazi bali kuhakikisha mfanyakazi anapatiwa haki hizo wakati wote.

Kwa waajiriwa, ni muhimu kuzifahamu haki hizi si mpaka zibandikwe kwenye tangazo ndipo ziwe haki yako. Haki hizi ni za kisheria, waajiri wengine hawazijui au ni wakaidi kuziweka zijulikane. Wewe uliyepata kuzijua hakikisha unazidai hata kama hazijabandikwa kwenye matangazo ni haki zako inakupasa kuchukua hatua pindi unapoona zinakiukwa. Ni vyema kufahamu ya kuwa woga wako wa kuchukua hatua unaendeleza ukandamizaji dhidi yako na waajiriwa wengine mahali pa kazi.

Kumbuka ‘kutokujua sheria si utetezi iwapo utatenda kosa lolote tafuta maarifa sahihi ya kisheria yakusaidie kufanya maamuzi sahihi kila siku.

Nakutakia siku njema ndugu yangu.

Isaack Zake, Wakili

Mwandishi Isaack Zake ni wakili wa Mahakama Kuu ya Tanzania wa kujitegemea anayefanya katika ofisi za Uwakili Zake Advocates zilizopo Dar es Salaam, Mtaa wa Bibi Titi Mohamed. Isaack Zake anatoa elimu ya kisheria, ushauri wa kisheria na usimamizi wa kisheria katika maeneo mbalimbali kama Sheria za Kazi, Mirathi, Ndoa, Mikataba na Biashara. Kwa ushauri usisite kuwasiliana naye kwa 0713 888 040 na email zakejr@gmail.com