Biashara Sheria.12. Sifa za Mkataba Halali Kisheria

Utangulizi

Karibu sana ndugu msomaji wa ukurasa wetu wa Biashara Sheria. Ukurasa huu umekuwa mahsusi kwa ajili ya uchambuzi wa mambo mbalilmbali yanayomwezesha mtu au kikundi kuwa na namna bora ya kuanzisha na kuendesha shughuli zao za kibiashara kwa mujibu wa sheria. Leo tunaanza kujifunza juu ya sifa zinazosababisha mkataba kuwa halali kisheria. Karibu tujifunze.

Maana ya mkataba wa biashara

Mkataba kwa tafsiri ya kawaida ni makubaliano baina ya pande mbili au zaidi. Hivyo mkataba wa kibiashara ni makubaliano yanayohusisha mbadilishano wa huduma au bidhaa baina ya pande mbili au zaidi. Kama ilivyo mikataba mingine, vivyo hivyo mikataba ya kibiashara inaongozwa na sheria kuu ya Mikataba Sura ya 345.

Watu wengi wapo kwenye biashara kwa muda mrefu lakini hawaoni umuhimu wa kufanya makubaliano kisheria bali wanafanya kwa kuaminiana tu. Hali hii si nzuri kwani matokeo yake ni hasara kubwa kwani watu nyakati hizi hawaaminiki.

Maana ya Mkataba kisheria

Kwa tafsiri ya kisheria mkataba ni makubaliano baina ya pande mbili au zaidi yanayofanyika kwa mdomo au maandishi yenye nguvu ya kisheria.

Watu wanaingia makubaliano kila siku aidha yam domo au maandishi lakini makubaliano hayo yanakosa kipengele muhimu sana cha kufanya makubaliano hayo kuwa halali ni ‘nguvu ya kisheria’. Si makubaliano yote yana nguvu ya kisheria. Katika mfululizo wa makala hizi za kuangalia sifa za mikataba ya kibiashara tutajifunza vipengele muhimu vya kuzingatia ili kuingia makubaliano ya kibiashara yenye nguvu ya kisheria yaani yenye kuzibana pande zote kutekeleza majukumu yao kisheria.

  1. Pendekezo na kukubaliwa kwa pendekezo (Offer and acceptance)

Ili mkataba wa kibiashara ili uwe halali ni lazima kuwepo na pendekezo kutoka upande mmoja kwenda upande mwengine na pendekezo hilo ni lazima likubaliwe. Sheria za mikataba zinaeleza juu ya pendekezo yaani ‘offer’ na lile pendekezo liwe limekubaliwa na upande mwengine yaani ‘acceptance’.

Pendekezo hutolewa na mtu  juu ya kitu au jambo fulani akiwa na lengo la kubanwa kisheria juu ya masharti ya kimkataba mara baada ya pendekezo lake kukubaliwa. Pendekezo linaweza kutolewa kwa njia mbalimbali, mfano kwa njia ya barua, gazeti, tangazo au bidhaa iliyowekwa tayari kwa kuuzwa.

Mfano; unapenda katika maduka ya ‘super market’ unakuta bidhaa zimewekwa katika maeneo tofauti tofauti pamoja na bidhaa husika kuna bei imewekwa katika kila bidhaa. Hapa tayari muuzaji ametoa pendekezo au ‘offer’ endapo wewe mnunuzi utakubaliana na ile bei na ile bidhaa na kuamua kuichukua maana yake umeikubali ‘acceptance’.

Kukubaliwa kwa pendekezo ni ahadi au kitendo kinachoonesha utayari wa upande wa pili kukubali kwa pendekezo na masharti ya kimkataba yaliyoambatana nayo. Kukubaliwa huko kwa pendekezo ni lazima kuwasilishwe kwa mtoa pendekezo kwamba pendekezo lake na masharti yake yamekubaliwa.

Kwa ushauri zaidi usisite kuwasiliana nasi kama inavyoelekezwa hapo chini katika makala hii.

Kumbuka ‘kutokujua sheria si utetezi iwapo utatenda kosa lolote tafuta maarifa sahihi ya kisheria yakusaidie kufanya maamuzi sahihi kila siku.

Nakutakia siku njema ndugu yangu.

Mwandishi Isaack Zake ni wakili wa Mahakama Kuu ya Tanzania wa kujitegemea anayefanya katika ofisi za Uwakili Zake Advocates zilizopo Dar es Salaam, Mtaa wa Bibi Titi Mohamed. Isaack Zake anatoa elimu ya kisheria, ushauri wa kisheria na usimamizi wa kisheria katika maeneo mbalimbali kama Sheria za Kazi, Mirathi, Ndoa, Mikataba na Biashara. Kwa ushauri usisite kuwasiliana naye kwa 0713 888 040 na email zakejr@gmail.com

4 replies
  1. Benedictor Richard
    Benedictor Richard says:

    Asante Mh Wakili kwa elimu nzuri.

    Je endapo mkataba wa sheria ya biashara ya ubia haujafuatwa ….mahakama hutumia sheria ipi katika kugawa faida na hasara zilizopatikana katika biashara za ubia?

    • ulizasheria
      ulizasheria says:

      Ipo sheria ya Mikataba ambayo inaongoza mahakama na pia yapo mashauri mbalimbali ambayo yameamuliwa yanakuwa mwongozo wa mahakama kufikia maamuzi ya haki.

Comments are closed.