Biashara Sheria.11. Umuhimu wa risiti kwenye mauzo ya huduma au bidhaa

Utangulizi

Karibu sana ndugu msomaji wa ukurasa wetu wa Biashara Sheria. Ukurasa huu umekuwa mahsusi kwa ajili ya uchambuzi wa mambo mbalimbali yanayomwezesha mtu au kikundi kuwa na namna bora ya kuanzisha na kuendesha shughuli zao za kibiashara kwa mujibu wa sheria. Leo tunakwenda kujifunza juu ya Umuhimu wa risiti kwenye mauzo ya huduma au bidhaa. Karibu tujifunze.

Maana ya risiti

Hivi karibuni tumepewa msisitizo zaidi wa kutoa na kudai risiti kkutokana na mauzo ya huduma au bidhaa. Mamlaka ya Mapato (TRA) na Serikali kwa ujumla inasisitiza umuhimu wa kupata risiti kwa kila mauzo au huduma tunazopewa.

Kwa tafsiri ya kawaida ya Kiswahili risiti ni kipande cha karatasi kinachoonyesha kupokewa au kutolewa pesa. Kwa maneno mengine risiti ni stakabadhi.

Msisitizo wa risiti au stakabadhi umekuwa ukitolewa sana hasa katika kuhimiza ukusanyaji wa kodi ya Serikali. Hili ni jambo muhimu sana katika kuchagiza maendeleo ya taifa siku kwa siku kwani Serikali ili kuendelea inahitaji fedha.

Maana ya risiti kisheria

Risiti ni uthibitisho anaotoa muuzaji au mtoa huduma kwenda kwa mnunuzi au mteja yenye kuonesha aina ya bidhaa au huduma aliyotoa na kiasi kilicholipwa kutokana na bidhaa au huduma. Risiti au stakabadhi ni nyaraka ya kisheria na inaonesha mahusiano ya kibiashara au huduma baina ya mfanyabiashara au mtoa huduma na mnunuzi au mteja.

Risiti ni nyaraka inayokubali au kuthibitisha kuwa malipo yamefanyika kwa ajili ya bidhaa au huduma fulani.

Ni nini umuhimu wa risiti kisheria?

  1. Kuonesha uhusiano wa kibiashara au kihuduma kati ya mfanyabiashara na mteja.

 

Kwa kuwa mahusiano mengi ya kibiashara au kihuduma hutokea mara moja na huwa ya muda mfupi, risiti ni njia mojawapo ya kuonesha uhusiano baina ya pande mbili.

  1. Kumlinda mteja na bidhaa au huduma endapo itajitokeza bidhaa ina shida au huduma haikukidhi viwango.

 

Risiti ndio nyaraka inayoweza kumsadia kisheria mnunuzi endapo atapokea huduma au bidhaa yenye upungufu. Si rahisi kama umepata huduma au bidhaa eneo fulani alafu hukupata risiti huwezi kuirudisha kama haijakidhi viwango au makusudi ya yale yaliyokufanya kuinunua. Risiti ndiyo inakupa uaminifu kwa muuzaji kwamba bidhaa ile uliitoa kwake na si kwa mfanyabiashara mwengine.

  1. Uthibitisho wa kisheria endapo madai ya haki au mgogoro utaibuka kuhusiana na mauziano au huduma husika.

 

Suala la mauzo na manunuzi linaweza kuzua mgogoro baina ya pande mbili. Mahakama au vyombo vya maamuzi ili kuweza kufikia uamuzi wowote vitahitaji uthibitisho endapo kulikuwa na mahusiano ya kihuduma au kibiashara kwa pande hizo mbili. Risiti au stakabadhi ni nyaraka muhimu sana katika kupata uthibitisho huo na itasaidia sana kwa chombo cha uamuzi kufikia uamuzi wa haki.

  1. Uthibitisho wa kumsaidia mteja kurudishiwa fedha zake katika kutokana na huduma husika.

 

Kuna ofisi au waajiri ambao wanaruhusu wafanyakazi wao kuingia gharama na kuwarudishia gharama hizo. Kigezo kinachotumika hasa ni mfanyakazi au mtu husika ili arudishiwe gharama zake basi ni lazima awasilishe risiti za huduma au bidhaa husika, pasipo risiti malipo au kurudishiwa fedha hakuwezekani.

  1. Risiti inawalinda kisheria mfanyabiashara na mteja

Sheria za Kodi zinataka pande zote zinazohusika katika utoaji wa huduma au biashara basi kuhakikisha risiti inatolewa na yule anayepokea huduma kuwa na risiti halali. Kukosekana kwa risiti inachukuliwa kama njama ya kuikosesha serikali mapato ambapo ni kosa kisheria. Ili wafanyabiashara au watoa huduma pamoja na wateja wao wawe salama ni kuhakikisha risiti inatolewa kwa mujibu wa sheria katika mauzo au utoaji wa huduma.

Hitimisho

Kama tulivyoona kuwa suala la risiti kwenye mauzo au huduma ni suala za zaidi ya kodi ya Serikali bali ni nyaraka ya kisheria ya kuwalinda wote yaani mfanyabiashara, mnunuzi na hata Serikali. Risiti inasaidia kutatua migogoro mingi kama ikitolewa na kutunzwa katika kumbukumbu. Tujifunze kufuatilia risiti na kutoa risiti mara zote katia huduma na biashara zetu ili kutuepusha na usumbufu usio wa lazima. Kumbuka kutokutoa au kutokudai risiti ni kosa la kijinai ambalo linaweza kupelekea hasara kubwa kwa mfanyabiashara hata mteja pia.

‘Hakikisha unatoa risiti na kudai risiti ikulinde kisheria’

Kwa ushauri zaidi usisite kuwasiliana nasi kama inavyoelekezwa hapo chini katika makala hii.

Kumbuka ‘kutokujua sheria si utetezi iwapo utatenda kosa lolote tafuta maarifa sahihi ya kisheria yakusaidie kufanya maamuzi sahihi kila siku.

Nakutakia siku njema ndugu yangu.

Mwandishi Isaack Zake ni wakili wa Mahakama Kuu ya Tanzania wa kujitegemea anayefanya katika ofisi za Uwakili Zake Advocates zilizopo Dar es Salaam, Mtaa wa Bibi Titi Mohamed. Isaack Zake anatoa elimu ya kisheria, ushauri wa kisheria na usimamizi wa kisheria katika maeneo mbalimbali kama Sheria za Kazi, Mirathi, Ndoa, Mikataba na Biashara. Kwa ushauri usisite kuwasiliana naye kwa 0713 888 040 na email zakejr@gmail.com