52. Kudharau Mamlaka ya Mwajiri
Utangulizi
Ndugu msomaji wa makala za Uchambuzi wa Sheria ambapo tumekuwa tukiichambua Sheria ya Kazi. Katika makala iliyopita tumeona juu ya Utoro Uliokithiri au Kutelekeza Kazi. Leo tunaangalia juu kosa la Kudharau Mamlaka ya Mwajiri. Karibu tujifunze.
Maana ya Kudharau Mamlaka ya Mwajiri
Kudharau mamlaka ya mwajiri ni aina nyingine ya utovu wa nidhamu anaoweza kufanya mfanyakazi, kunakopelekea kusitishwa kwa ajira yake endapo itathibitika mfanyakazi amedharau mamlaka ya mwajiri.
Katika lugha ya kiingereza kudharau mamlaka ya mwajiri kunajulikana kama ‘insubordination’.
Tafsiri ‘insubordination’ inatokana na kesi ya National Union of Public Service & Allied Worker’s Union (NUPSAWA) Obo Mani and 9 Others vs National Loitteries Board, Labour Case No.576/2012 iliyoamuliwa na Mahakama ya Juu ya Afrika ya Kusini ikisema;
‘Unfair labour practice occurring when an employee refuses to accept the authority of his or her employer or of a person in a position of authority over an employee’
Kwa tafsiri ina maana ya kwamba Kudharau mamlaka ya mwajiri inatokea pale mfanyakazi anakataa kutekeleza maagizo ya mwajiri au mtu mwenye mamlaka juu yake kwa niaba ya mwajiri.
Sheria ya Kazi na Ajira kupitia Kanuni za Utendaji Bora ‘Employment and Labour Relations (Code of Good Prictice)’ inaeleza kuwa mfanyakazi anaweza kuachishwa kazi kwa kosa la Kudharau Mamlaka ya mwajiri.
‘commission of serious or repeated act of insubordination at the employer or during working hours against the employer’
Maana yake
‘vitendo vya mfanyakazi vya kujirudia au tendo moja la kudharau mamlaka ya mwajiri au kudharau mwajiri muda wa kazi’
Vigezo vya kuchukua hatua dhidi ya mfanyakazi kwa Kudharau Mamlaka ya mwajiri
Vipo vigezo vya kisheria vinavyopaswa kuzingatiwa na mwajiri ili kuweza kuchukua hatua dhidi ya mfanyakazi. Waajiri wengi wanashindwa kufahamu ni makosa yepi au vitendo gani vikifanywa na mfanyakazi vinaashiria kosa la kudharau mamlaka ya mwajiri. Mwongozo wa kisheria unaanisha vigezo vinavyoweza kumruhusu mwajiri kumchukulia hatua za kinidhamu mfanyakazi kwa kosa la kudharau mamlaka.
- Kukataa kwa makusudi kutii maelekezo halali ya mwajiri
Mfanyakazi anapokataa kwa makusudi kutekeleza maagizo halali ya mwajiri anatenda kosa la kudharau mamlaka ya mwajiri. Mwajiri anapotoa maelekezo aidha yeye binafsi au kupitia kiongozi mahali pa kazi ni wajibu wa mfanyakazi kutii maagizo hayo. Kukataa maelekezo hayo kunapelekea kutenda kosa la utovu wa nidhamu.
- Maelekezo ya mwajiri ni lazima yake kwa mujibu wa sheria na taratibu za kazi
Mfanyakazi anawajibika tu kutii maelekezo ya mwajiri yaliyo kwa mujibu wa sheria na taratibu za kazi. Kwa namna yoyote ile mfanyakazi hatolazimika kutii maagizo ya mwajiri yaliyo kinyume cha sheria au taratibu za kazi. Ni lazima maelekezo ya mwajiri yawe halali kwa maana yapo ndani ya sheria na taratibu za kazi na yanamuhusu mfanyakazi husika.
- Maelekezo hayo ni lazima yawe majukumu muhimu yanayopaswa kufanywa/kutekelezwa na mfanyakazi
Ni muhimu pia kuthibitisha kuwa maelekezo husika anayotoa kwa mfanyakazi ni lazima yawe majukumu yanayomuhusu mfanyakazi. Mfanyakazi anawajibika kufanyia kazi maelekezo ambayo yapo ndani ya uwezo wake na kwa kawaida yanaweza kufanyika. Mwajiri hapaswi kutoa maelekezo ambayo kwa kawaida hayatekelezeki au yapo nje ya uwezo wa mfanyakazi husika.
Hitimisho
Kudharau mamlaka ya mwajiri ni moja wapo ya kosa linaloweza kusababisha mfanyakazi kusitishwa ajira yake. Ni muhimu mwajiri kuzingatia ili kumwachisa mfanyakazi kwa kosa la kudharau mamlaka ni lazima afuate utaratibu wa haki na kuthibitisha sababu husika. Mwajiri anapaswa kuhakikisha maagizo anayotoa ni halali na yenye kufuata sheria. Mfanyakazi anapaswa kuzingatia kutekeleza maagizo ya mwajiri wake ambayo ni halali wakati wote. Kudharau mamlaka ya mwajiri ni kosa ambalo linaweza kusababisha kusitishwa kwa ajira ya mfanyakazi.
Kwa ushauri zaidi usisite kuwasiliana nasi kama inavyoelekezwa hapo chini katika makala hii.
Kumbuka ‘kutokujua sheria si utetezi iwapo utatenda kosa lolote’ tafuta maarifa sahihi ya kisheria yakusaidie kufanya maamuzi sahihi kila siku.
Nakutakia siku njema ndugu yangu.
Mwandishi Isaack Zake ni wakili wa Mahakama Kuu ya Tanzania wa kujitegemea anayefanya katika ofisi za Uwakili Zake Advocates zilizopo Dar es Salaam, Mtaa wa Bibi Titi Mohamed. Isaack Zake anatoa elimu ya kisheria, ushauri wa kisheria na usimamizi wa kisheria katika maeneo mbalimbali kama Sheria za Kazi, Mirathi, Ndoa, Mikataba na Biashara. Kwa ushauri usisite kuwasiliana naye kwa 0713 888 040 na email zakejr@gmail.com