51. Utoro Uliokithiri au Kutelekeza Kazi

Utangulizi

Ndugu msomaji wa makala za Uchambuzi wa Sheria ambapo tumekuwa tukiichambua Sheria ya Kazi. Katika makala iliyopita tumeona juu ya aina nyingine za Utoro Kazini. Leo tunaangalia juu Utoro Uliokithiri au Kutelekeza Kazi. Karibu tujifunze.

Maana ya Kutelekeza Kazi

Kutelekeza kazi ni aina ya utoro uliokithiri wa kazi unaojitokeza pale mfanyakazi anapoacha kuja kazini kwa muda mrefu sana na kwa nia ya kutokutaka kurudi kuendelea na kazi.

Katika lugha ya kiingereza zinaoneshwa tofauti ya utoro kazini, utoro uliokithiri au kutelekeza kazi. Maneno haya yanafahamika kama ‘absenteeism’ ‘abscondment’ na ‘disertion’.

Utoro wa kawaida ni ule mfanyakazi anaacha kuja kazini kwa muda lakini anayo nia ya kuendelea kufanya kazi. Ila utoro uliokithiri au kutelekeza kazi ni pale mfanyakazi anaacha kabisa kuja kazini pasipo taarifa yoyote kwa nia ya kutokuja tena kazini.

Kutelekeza kazi au utoro uliokithiri (disertion or abscondment) inatokea mara nyingi pale mfanyakazi amepata kazi nyingine lakini hataki mwajiri wake ajue kama yupo mahali kwengine anafanya kazi. Wapo wafanyakazi hawaonekani kazini kwa mwezi mzima au miezi mitatu au zaidi ya hapo. Hali hii ni utoro uliokithiri au kutelekeza kazi.

Waajiri wengi wanatatizwa na aina ya wafanyakazi wanaotelekeza kazi au wanakuwa watoro waliokithiri na wanashindwa kuchukua hatua stahiki dhidi yao. Hali inakuwa ngumu sana kwa kuwa wafanyakazi hao hukata mawasiliano na mwajiri hivyo mwajiri anakosa namna bora ya kumpata mfanyakazi husika. Pia wafanyakazi hao hawaandiki barua ya kujiuzulu au kuomba likizo ya muda bila malipo bali wanaondoka tu.

Hatua za kuchukua

Lazima ifahamike kwamba kutelekeza kazi au utoro uliokithiri ni utovu wa nidhamu ambao unapaswa kushughulikiwa kinidhamu. Mwajiri hapaswi kuchukua hatua labda ya kutokulipa mshahara bila kufuata taratibu za kinidhamu. Waajiri wengi wanakimbilia kutokulipa mshahara pasipo kuhakikisha hatua za kinidhamu zimechukuliwa kwanza. Tuangalie hatua za kuchukua kwenye tatizo au kosa la utoro uliokithiri au kutelekeza kazi;-

  1. Kuwa na mawasiliano mbadala na wafanyakazi wako

Mwajiri unapaswa uwe na mawasiliano ya kutosha na mfanyakazi wako. Ikiwezekana ufahamu mahali anapokaa au namna ya kumpata endapo yeye mwenyewe hutakuwa na mawasiliano nawe. Hii ni muhimu sana linapokuja suala la kutaka kumchukulia hatua mfanyakazi ambaye haonekani. Unaweza kuwa na mawasiliano ya mwenzi wake au mdhamini wake au eneo la serikali ya mtaa anapoishi.

  1. Anzisha mchakato wa kinidhamu na tuma kwa mawasiliano yote

Mara baada ya kuona mfanyakazi haonekani kazini kwa kipindi cha mwezi mmoja au zaidi basi anzisha mchakato wa kinidhamu kwa kumwandikia shitaka la utoro uliokithiri au kutelekeza kazi na kumtaka ajibu na kufika kwenye kikao cha kinidhamu. Ni muhimu barua hizi zikatumwa katika mawasiliano aliyotoa mwajiri au kupelekwa eneo ambalo anakaa. Hii itasaidia kuonesha kuwa mwajiri ulifanya jitihada zote za kuhakikisha unampata mfanyakazi na anajua kinachoendelea. Kama mwajiri ana uwezo anaweza kutoa tangazo kwenye gazeti linalosomwa na watu wengi juu ya kumwita mfanyakazi kwenye kikao cha kinidhamu.

  1. Endesha kikao cha kinidhamu cha upande mmoja

Endapo mfanyakazi atashindwa kujibu tuhuma au kufika kwenye kikao cha kinidhamu, mwajiri anayo haki ya kuendesha kikao kwa kusikiliza upande mmoja na kudhibitisha kosa la mfanyakazi.

  1. Pitisha adhabu inayostahili kwa mfanyakazi husika

Mara baada ya kikao cha kinidhamu kukaa na kuthibitishwa kwa kosa la mfanyakazi, mwajiri anaweza kutoa adhabu inayostahili kwa mfanyakazi husika ikiwa ni kusitisha ajira yake tangu siku hiyo ya maamuzi ya mwajiri.

Hitimisho

Ni muhimu sana kwa mwajiri kufuata utaratibu wa kisheria wa kusitisha ajira kwa sababu za halali na kufuata utaratibu wa haki. Mara nyingi tunaona mwajiri anaacha kuchukua hatua kwa kigezo kuwa hampati mfanyakazi kwenye mawasiliano au anaamua kuacha kulipa mshahara pasipo kufuata taratibu. Mwendo huu wa mwajiri kutokufuata utaratibu mwisho wake mfanyakazi anarudi na kuonekana hakutendewa haki. Ni muhimu kwa mwajiri kuwa na mawasiliano ya kutosha ya mfanyakazi ambayo anaweza kuyatumia kumfikia mfanyakazi hata kama mfanyakazi hataki afikiwe.

Kwa ushauri zaidi usisite kuwasiliana nasi kama inavyoelekezwa hapo chini katika makala hii.

Kumbuka ‘kutokujua sheria si utetezi iwapo utatenda kosa lolote tafuta maarifa sahihi ya kisheria yakusaidie kufanya maamuzi sahihi kila siku.

Nakutakia siku njema ndugu yangu.

Mwandishi Isaack Zake ni wakili wa Mahakama Kuu ya Tanzania wa kujitegemea anayefanya katika ofisi za Uwakili Zake Advocates zilizopo Dar es Salaam, Mtaa wa Bibi Titi Mohamed. Isaack Zake anatoa elimu ya kisheria, ushauri wa kisheria na usimamizi wa kisheria katika maeneo mbalimbali kama Sheria za Kazi, Mirathi, Ndoa, Mikataba na Biashara. Kwa ushauri usisite kuwasiliana naye kwa 0713 888 040 na email zakejr@gmail.com

 

 

2 replies

Comments are closed.