Upi ni ukomo wa mashauri ya Ardhi?
Utangulizi
Karibu sana ndugu msomaji na mfuatiliaji wa ukurasa huu wa Sheria Leo kwenye mtandao wako wa Uliza Sheria. Kama kawaida yetu lengo la kukuletea makala hizi fupi ni kukusaidia kuishi kwa mujibu wa sheria kila siku. Leo tunajibu swali la msomaji wetu kuhusiana na suala la umiliki na ukomo wa mashauri ya ardhi. Karibu tujifunze.
Swali la msomaji wetu
Tunapokea maswali mengi sana kutoka kwa wasomaji wetu na tunapasa muda wa kuwashauri na kuchukua hatua zinazostahili. Leo tunakushirikisha swali mojawapo la msomaji wetu linalosema
‘Familia yetu ilisafisha eneo la ekari 10 na kuanza kilimo mnamo mwaka 1994. Tumeendelea kulitunza shamba hilo na kupanda mazao ya muda na miti ya kudumu kwa kipindi chote. Utaratibu wa kumilikishwa ardhi na Kijiji ulituwezesha kupata hati ya kijiji mwaka 2017 baada ya kukidhi masharti yote. Hivyo tumekuwa na umiliki wa eneo hili kwa muda wa miaka 24 sasa. Wamejitokeza watu wakidai kuwa eneo hilo ni lao, na kwamba mara ya mwisho waliacha kulima mwaka 1995. Je, sheria inasemaje katika suala kama hili? Hamis – Dodoma
Njia za Umiliki wa Ardhi
Swali hili la msomaji wetu limejikita katika maeneo mawili ya kuonesha juu ya umiliki wa ardhi. Maeneo haya tuliyajadili katika Sheria Leo.81. Utaratibu wa Umiliki wa Ardhi kwa njia ya Kusafisha Eneo na Sheria Leo.82. Utaratibu wa Umiliki wa Ardhi kwa njia ya Uvamizi kwa ufafanuzi zaidi unaweza kurejea kuzisoma makala hizo.
Sheria ya Ardhi inatambua umiliki kwa njia ya
- Kusafisha eneo au pori
- Kumiliki ardhi kwa njia ya uvamizi
Umiliki wa ndugu yetu muuliza swali unaweza kuangukia katika maeneo haya mawili yaani kusafisha eneo au uvamizi. Mtu anaweza kumiliki ardhi akisafisha eneo na kuendelea kulitumia kwa muda mrefu kiasi kwamba jamii na majirani anaopakana nao wakatambua kuwa yeye ni mmiliki halali.
Hali kadhalika mtu anaweza kumiliki kwa njia ya uvamizi ‘adverse possession’ wa eneo kwa muda mrefu pasipo kuingiliwa na mmiliki wa awali katika kipindi kisichopungua miaka 12 mfululizo.
Ni wazi kuwa familia husika imekuwa ikimiliki eneo husika kwa kipindi kisichopungua miaka 20 mfululizo na kuthibitisha kutokana na shughuli za maendeleo zilizofanyika katika eneo hilo. Hoja inayotoka kwa upande unaodai eneo ni lao tangu mwaka 1995 inapaswa iambatane na ushahidi wa juu ya matumizi au maendeleo yaliyofanyika katika eneo husika.
Sheria inaeleza wazi kuwa kama mtu amemiliki au amekuwa akiitumia ardhi kwa shughuli mbalimbali mfululizo kwa miaka isiyopungua 12 pasipo kuingiliwa na aliyekuwa mmiliki basi eneo hilo linakuwa ni halali kwa yule anayemiliki kwa sasa.
Pia ifahamike kuwa masuala ya ardhi yana ukomo wa muda wa kuwasilisha mashauri mahakamani. Endapo eneo lako limevamiwa au kuchukuliwa na mtu unapaswa kuchukua hatua za kisheria ndani ya miaka 12. Kushindwa kwako kuchukua hatua za kisheria katika kipindi hicho, ni dhahiri kuwa unazuiwa kisheria kudai haki katika eneo hilo kutokana na kuwa nje ya muda wa kisheria.
Hivyo, hoja ya msingi ambayo wadai wanapaswa kuiwasilisha ni kujieleza walikuwa wapi miaka yote 24 wasichukue hatua siku zote hizo?
Hitimisho
Ni rai yangu kwa wananchi wote hasa wa maeneo ya mijini au vijijini kupata uhalali wa umiliki wa maeneo yao. Lipo wimbi kubwa la watu wasio waaminifu na kwa kutumia watendaji wasio waadilifu wanaweza kupotosha haki ya mtu. Ni vyema kuzifahamu sheria na kuzifuata. Pia wananchi wasitelekeze maeneo na mara baada ya kuona hali ya kimaendeleo imebadilika wanarudi kutaka kudhulumu walioyafanyia kazi kwa muda mrefu.
Kumbuka ‘kutokujua sheria si utetezi iwapo utatenda kosa lolote’ tafuta maarifa sahihi ya kisheria yakusaidie kufanya maamuzi sahihi kila siku.
‘Usikwame kwenye tatizo lolote la kisheria wakati unayo nafasi ya kuuliza, uliza sheria uoneshwe njia’
Nakutakia siku njema sana ndugu yangu.
Mwandishi Isaack Zake ni wakili wa kujitegemea anayefanya katika ofisi za Uwakili Zake Advocates zilizopo Dar es Salaam, Mtaa wa Bibi Titi Mohamed. Isaack Zake anatoa elimu ya kisheria, ushauri wa kisheria katika maeneo mbalimbali kama Sheria za Kazi, Mirathi, Ndoa, Mikataba na Biashara. Kwa ushauri usisite kuwasiliana naye kwa 0713 888 040 na email zakejr@gmail.com