50. Aina nyingine za Utoro Kazini

Utangulizi

Ndugu msomaji wa makala za Uchambuzi wa Sheria ambapo tumekuwa tukiichambua Sheria ya Kazi. Katika makala iliyopita tumeona juu ya Hatua za Kuchukua kushughulikia Utoro Kazini. Leo tunaangalia juu ya aina nyingine ya utoro kazini. Karibu tujifunze.

Aina nyingine za Utoro kazini

Katika makala zilizotangulia tumeona juu ya utoro kazini unaohusisha kutokufika kazini kwa siku kadhaa na namna mwajiri anavyoweza kuchukua hatua. Hatahivyo, zipo aina nyingine za utoro kazini ambazo Sheria ya Ajira inazitambua na imeweka utaratibu wa namna ya kushughulikia.

Katika mojawapo ya maswali ambayo tulipokea kutoka kwa wasomaji wetu linasema

‘sheria inasemaje juu ya utoro wa mfanyakazi kuwahi kuondoka kazini kabla ya muda?

Katika kujibu swali hili ni lazima kufahamu kuwa utoro kazini haihusishi tu suala la kutokufika kazini kwa siku nzima bali yapo mazingira mengine yanayoweza kuonekana kuwa ni utoro kazini.

Sheria inatambua aina ya utoro kazini kama ifuatavyo;

  • Kutokufika kabisa kazini siku ya kazi
  • Kuchelewa kufika kazini kulingana na muda wa kazi
  • Kuwahi kutoka kazini pasipo ruhusa ya mwajiri
  • Kushindwa kuzingatia muda uliopewa na mwajiri. Mfano kuchelewa kurudi kazini baada ya kupewa muda wa chakula, n.k

Katika makala zilizotangulia tumeweza kuangalia aina moja tu ya utoro kazini yaani kutokufika kazini kwa siku nzima pasipo na sababu na kutokufika huko kukafikia siku 5. Aina nyingine za utoro kama zilivyoneshwa hapo juu ni kuchelewa kazini, kuwahi kutoka au kutokuzingatia muda katika ruhusa ulizopewa na mwajiri.

Kwa hali ilivyo sasa aina hizi nyingine za utoro ndizo zimekithiri sana na zinalalamikiwa mno na waajiri. Kila siku wafanyakazi wamekuwa na visingizio vya kuchelewa kazini au kuwahi kutoka kabla ya muda wa kazi. Hali hii inaathiri utendaji wa kazi na uzalishaji mahali pa kazi.

Wafanyakazi wamekuwa na sababu nyingi sana zinazoweza kutumika kama visingizio vya wao kutokuwahi kazini ikiwepo na suala la foleni, ugonjwa, watoto, misiba, kuharibika kwa vyombo vya usafiri, ukosefu wa nishati ya umeme, ukosefu wa usafiri n.k.

Hatua za kuchukua

Mwajiri kama msimamizi mkuu wa shughuli za kazi anayo haki na wajibu wa kuchukua hatua stahiki endapo tabia hii ya utoro inakithiri miongoni mwa wafanyakazi.

Sheria ya Ajira inaelekeza kuwa mwajiri anaweza kutoa onyo kwa mfanyakazi husika juu ya kurekebisha tabia yake na kubadili mwenendo wake ili kuwahi kazini na kuepuka utoro kazini. Onyo la mwajiri linaweza kutolewa kwa njia ya mdomo na endapo tabia hii inaendelea kushamiri basi onyo la maandishi linaweza kutolewa.

Hitimisho

Ni muhimu kutambua kuwa muda ndio kitu cha thamani sana ambacho mwajiri anapaswa kukilinda na mfanyakazi anapaswa kuheshimu. Ili kazi ilete tija, manufaa na ufanisi bora kwa wateja wa ofisi ni lazima muda uzingatiwe wakati wote.

Mfanyakazi, ili uweze kulipwa ni muhimu kuhakikisha muda wa mwajiri unautendea haki. Ipo dhana kwa wafanyakazi kwa kuwa wanalipwa kwa mwezi basi suala la muda si muhimu kwao kwani wakifanya kazi au wasipofanya bado watalipwa. Ni nadra sana kukuta changamoto ya kupoteza muda kwa wafanyakazi wanaolipwa kwa siku au wiki.

Ni muhimu sana kufahamu kuwa hali na mazingira ya kazi katika zama zilizoendelea inabadilika kwa kasi sana, hivyo wafanyakazi wanapaswa kuzingatia kuwa mabadiliko haya yanaweza kuathiri mfumo wa malipo kuzingatia tija, ufanisi na utendaji wa masaa ya wafanyakazi kama nchi za magharibi zinavyofanya. Mabadiliko haya yapo mlangoni ni suala la muda tu.

 

Kwa ushauri zaidi usisite kuwasiliana nasi kama inavyoelekezwa hapo chini katika makala hii.

Kumbuka ‘kutokujua sheria si utetezi iwapo utatenda kosa lolote tafuta maarifa sahihi ya kisheria yakusaidie kufanya maamuzi sahihi kila siku.

Nakutakia siku njema ndugu yangu.

Mwandishi Isaack Zake ni wakili wa Mahakama Kuu ya Tanzania wa kujitegemea anayefanya katika ofisi za Uwakili Zake Advocates zilizopo Dar es Salaam, Mtaa wa Bibi Titi Mohamed. Isaack Zake anatoa elimu ya kisheria, ushauri wa kisheria na usimamizi wa kisheria katika maeneo mbalimbali kama Sheria za Kazi, Mirathi, Ndoa, Mikataba na Biashara. Kwa ushauri usisite kuwasiliana naye kwa 0713 888 040 na email zakejr@gmail.com