4. Wadau wa Sheria za Barabarani – Waenda kwa Miguu

Utangulizi

Karibu sana ndugu msomaji na mfuatiliaji wa ukurasa huu wa Sheria Barabara kwenye mtandao wako wa Uliza Sheria. Ukurasa huu maalum unakuletea uchambuzi wa Sheria mbalimbali zinazohusiana na barabara. Kila siku kuna matukio mengi sana yanaendelea barabarani, lakini si watu wengi wanaojua taratibu zinazopaswa kuchukuliwa ili kushughulikia matukio hayo. Katika makala iliyopita tulijifunza juu ya madhara ya watu kujichukulia sheria mkononi hususan kwenye makosa ya barabarani. Leo tunaanza kuangalia na kuchambua wadau mbalimbali wa sheria za barabarani. Karibu tujifunze.

Sheria ya Usalama Barabarani

Sheria ya Usalama Barabarani Sura ya 168 ina wigo mpana wa kutambua watumiaji mbalimbali wa barabara. Watu wengi wanafikiri kuwa Sheria ya Usalama Barabarani inawahusu madereva tu wa vyombo vya moto, la hasha dhana hii si kweli.

Kila mmoja wetu ambaye kwa njia moja au nyingine atakuwa na matumizi ya barabara iwe akitembea au abiria au akiendesha chombo chochote kupita barabarani, huyo ni mdau wa Sheria za Barabara na anahusika kufahamu juu ya haki na wajibu alionao pindi anapotumia barabara.

Wadau wa Sheria za Barabara: Waenda kwa Miguu

Leo tunawazungumzia wadau muhimu katika matumizi ya barabara ambao ni waenda kwa miguu. Hili ni kundi kubwa kabisa kuliko makundi yote ya wadau wanaotumia barabara. Hatahivyo, kundi hili kwa sehemu kubwa halina ufahamu juu ya sheria zinazowaongoza pindi wanapokuwa katika matumizi ya barabara.

Halikadhalika, kundi la waenda kwa miguu ndilo linaloathirika sana pindi ajali au matatizo yanapojitokeza kuhusiana na matumizi ya barabara.

Mambo ya msingi kuzingatia

 • Tumia njia ya watembea kwa miguu; iwapo barabara unayotembea imetengewa njia ya waenda kwa miguu basi hakikisha unatembea kwenye njia hiyo na sio barabarani. Watu wengi pamoja na uwepo wa njia za waenda kwa miguu hawazitumii njia hizo na hatimaye huweza kupata ajali au kugongwa na vyombo vya moto.
 • Tembea upande wa kulia; endapo barabara husika ina njia ya watembea kwa miguu, hakikisha unatembea upande wa kulia ili uweze kuyaona magari au vyombo vya moto vinavyokuja mbele yako.
 • Kutembea na watoto; usiruhusu mtoto kutembea peke yake akiwa barabarani au kwenye njia ya watembea kwa miguu. Tembea na mtoto au watoto kwa kuwashika mikono.
 • Kutembea kwenye kundi; iwapo watu wanatembea kwenye kundi kwenye matembezi ambayo yanatumia barabara, wanapaswa kutembea upande wa kulia. Waandaaji wahakikishe kuna walinzi mbele na nyuma waliovaa au wenye alama za kuonesha ishara zinazong’aa wakati wa mchana au zinazoakisi wakati wa giza.

Mambo ya kuzingatia Unapovuka Barabara

 • Tafuta sehemu salama ya kuvuka; maeneo mengine ya barabara kuna vivuko vya punda milia au taa za kuongoza waenda kwa miguu jinsi ya kuvuka n.k
 • Simama kwenye ukingo wa barabara kabla ya kuvuka
 • Angalia magari/pikipiki barabarani pande zote zinazokuzunguka
 • Kama kuna gari/pikipiki inayokuja iache ipite kwanza
 • Utakapohakikisha usalama wako vuka moja kwa moja barabara pasipo kukimbia
 • Angalia na sikiliza magari/pikipiki pindi unapovuka

Mambo ambayo hutakiwi kufanya uwapo barabarani

 • Barabara si eneo la mazoezi ya mwili au viungo; kumekuwa na matumizi yasiyo rasmi hasa sehemu za mijini kuhusiana na vikundi vya mazoezi au watu binafsi. Pamoja na kusisitiza suala la afya ya wananchi, barabara hazijatengenezwa kwa ajili ya kufanyia mazoezi. Endapo suala la mazoezi au mashindano yanapoandaliwa kunakuwepo na kibali maalum na utaratibu unatolewa kwa watumiaji wengine wa barabara. Pia kumekuwa na michezo ya wanaotumia viatu vya magurudumu barabarani. Michezo hii ni hatari kwa usalama wako na watumiaji wengine wa barabara.
 • Matumizi ya simu ukiwa barabarani;  matumizi ya kupitiliza ya simu za mkononi imekuwa sababu kubwa ya ajali kwa madereva na hata waenda kwa miguu. Pindi unapofika barabarani unapaswa kuzingatia usalama wako na ule wa watumiaji wengine. Kuna mifano ya watu wamegongwa kwa sababu walikuwa wanasikiliza muziki kupitia ‘ear phones’ za kwenye simu zao. Unapokuwa barabarani unahitaji umakini wako wote.
 • kufanya biashara/shughuli yoyote maeneo ya barabara; kuna wimbi kubwa la wafanyabiashara wadogo wadogo ambao wanafanya biashara katikati ya barababara na pembezoni mwa barabara. Kwa mujibu wa Sheria ya Barabara ni marufuku mtu kufanya biashara barabarani kwani ni hatari kwa usalama wake na watumiaji wengine wa barabara. Halikadhalika yapo makundi ya watu wanaopita barabarani katika miji mikubwa kama ‘omba omba’ kundi hili linahusisha watu wazee, watoto wadogo na hata watu wenye ulemavu. Hatari kubwa inakuwepo kwa watu wa kundi hili na kuweza kusababisha ajali au madhara makubwa pindi ajali inapotokea.
 • Kutupa takataka barabarani au katika hifadhi ya barabara; hii imekuwa tabia mbaya sana kwa watu hasa maeneo ya miji mikubwa. Watumiaji wa barabara, waenda kwa miguu wamekuwa wakihusika katika uchafuzi wa mazingira ya barabara. Barabara zetu zinalindwa na sheria mbalimbali zinazohusiana na afya na ustawi wa watumiaji wa barabara. Hivyo ni makosa kutupa taka barabarani, unaweza kushtakiwa kwa kosa hili.

Hitimisho

Ni muhimu kama mdau wa barabara, wewe na mimi tunapotumia barabara kwa miguu tunawajibika kufuata sheria na maelekezo yanayotuhakikishia usalama sisi na watumiaji wengine. Kila wakati tunapokuwa barabarani tunapaswa kuchukua taadhari. Matumizi yoyote ya barabara yatakayohatarisha usalama wetu au wa watu wengine au miundombinu ya barabara ni makosa kisheria na unaweza kushtakiwa na mamlaka husika.

Kinachosisitizwa kwako na kwangu watumiaji wa barabara kama waenda kwa miguu ni kuhakikisha hatufanyi kitu ambacho kitaweza kuwa hatari kwetu na kwa watumiaji wengine wa barabara.

Kumbuka ‘kutokujua sheria si utetezi iwapo utatenda kosa lolote’ tafuta maarifa sahihi ya kisheria yakusaidie kufanya maamuzi sahihi kila siku.

Muhimu

Ikiwa una maswali au kuna eneo la kisheria ungependa kupata ufafanuzi basi nafasi ni yako na ndio msingi wa mtandao huu wa Uliza Sheria. Wasiliana nami na kuuliza maswali mbalimbali ili tuyachambue kwenye makala zijazo kwa njia ya e mail zakejr@gmail.com namba ya simu watsup 0713 888 040.

‘Usikwame kwenye tatizo lolote la kisheria wakati unayo nafasi ya kuuliza, uliza sheria uoneshwe njia’

Nakutakia siku njema.

Wako              

Isaack Zake, Wakili