Sheria Leo. Ni nini Asili ya Sheria?

Utangulizi

Ndugu msomaji wa uliza sheria karibu tena siku ya leo katika kuendelea kupata elimu yenye maarifa juu ya sheria. Leo tunaendelea kuangalia mambo ya msingi katika sheria. kwenye makala iliyopita tulijifunza juu ya Maana ya Sheria. Kama hukusoma makala hiyo bonyeza maneno haya Nini Maana ya Sheria?

Leo nimekuandalia somo zuri kabisa lenye swali la kujiuliza ‘Ni nini asili ya Sheria? Sheria inatoka wapi? au chanzo cha sheria ni nini? Karibu ndugu yangu kwenye darasa hili la sheria tujifunze pamoja.

Dhana za asili ya sheria

Ndugu msomaji zipo dhana nyingi na tofauti tofauti sana zinazoelezea asili ya sheria ambazo zimeelezewa na wasomi wa sheria wa karne zilizopita. Hatahivyo wasomi hawa wa sheria wanakubaliana kuwa asili ya sheria inaweza kufuatiliwa tangu kuanza kuishi kwa mwanadamu hapa ulimwenguni. Hivyo msimamo wa wasomi wa sheria wengi ni kuwa sheria ilianza pale watu walipoanza kuishi kama jamii.

Wasomi wa sheria wanakubaliana kuwa asili ya mwanadamu ni matokeo ya uumbaji wa Mungu (Supreme Being). Kwamba kupitia Mungu, watu walipokea sheria kwa ajili ya kuwasaidia wao kuhusiana na pia namna ya kuhusiana na mazingira yao.

Kama inavyofahamika watu wameumbwa na utashi wao binafsi yaani uwezo wa kufanya maamuzi pasipo kulazimishwa au kuingiliwa na watu wengine. Hivyo katika jamii ya watu ambao kila mmoja ana uhuru wa kufanya maamuzi aonavyo yeye inafaa ilizalisha mgongano wa kimaslahi baina ya watu. Kwa mfano mtu mmoja kwenye jamii analima shamba na kupanda mazao ya chakula, wakati mtu mwengine anaona kwenye shamba la mkulima ni chakula safi kwa mifugo yake, tayari kuna mgongano wa maslahi baina ya pande hizi mbili. Katika mazingira haya ya uhuru wa kuamua kwa kila mtu na uwezekano wa mgongano wa maslahi baina ya watu, hapakuwa na budi ila sheria iliingia katika jamii kuwasaidia wote kukaa kwa amani, utulivu na kujiletea maendeleo.

Kama tulivyojifunza maana ya sheria ni mfumo wa kanuni au taratibu za kuongoza matendo ya watu uliowekwa na mamlaka katika jamii fulani. Sheria imekuja kwa lengo la kusaidia jamii au kikundi cha watu kuweza kuishi katika viwango vya utaratibu vinavyokubalika miungoni mwao.

Tunaweza kuona kwenye jedwali juu ya asili ya sheria

Utawala wa Sheria

Mungu

 ⇓

Uumbaji wa Mwanadamu mwenye nguvu ya Utashi

Wanadamu kuishi kwa nguvu ya utashi (kufanya maamuzi)

kuibuka kwa mgongano wa maslahi kutokana na nguvu ya utashi

Uanzishwaji wa Sheria ( kanuni na taratibu zinazokubaliwa na jamii )

Matokeo ni uwepo wa amani, utulivu na utii

Maendeleo

Hitimisho

Ndugu msomaji kama tulivyoona katika makala hii yenye kujiuliza juu ya asili ya sheria kwamba asili yake inatoka kwa Mungu aliyeumba Mwanadamu na jamii zote. Ndio maana kwenye imani za dini mbali mbali zinazungumza juu ya sheria au taratibu ambazo Mungu ameziweka juu ya waamini wa dini husika, jinsi ya kuhusiana na Mungu wao, jinsi ya kuhusiana na jamii na mazingira yanayowazunguka.

Ni muhimu sana kufahamu asili ya sheria ili kuweza kutusaidia kuifahamu sheria inavyoweza kufanya kazi katika maeneo yetu mbali mbali siku kwa siku.

Ndugu msomaji wa makala za ulizasheria nakutakia wakati mwema sana siku ya leo ukiendelea kutafakari somo la leo.

Kumbuka ‘kutokujua sheria si utetezi iwapo utatenda kosa lolote’ tafuta maarifa sahihi ya kisheria yakusaidie kufanya maamuzi sahihi. Wasiliana nami kupitia www.ulizasheria.co.tz

Wako

Isaack Zake, Wakili

2 replies
  1. Richard Kaganda
    Richard Kaganda says:

    Kwa maneno yanayotumika katika sheria ya kutokujua sheria si utetezi iwapo utatenda kosa je neno ili halioneshi kua katika dunia hii haina haki ?

    Maana kama mtu hafahamu alafu anaonekana anabanwa huoni sheria ipo kwa ajiri ya kumbana ata asie sitahili ?

    • ulizasheria
      ulizasheria says:

      Ndugu yangu Richard ni muhimu sana ufahamu kuhusu sheria. Pitia makala nyingine katika ukurasa wa Sheria Leo utaona umuhimu na ulazima wa kuzijua Sheria. Kila mtu akikimbilia kusema hajui hakutakuwa na maana ya Sheria. Ndio maana tumekuletea huduma hii ambapo utapata fursa ya kujifunza na kuuliza juu ya mambo mbali mbali ya kisheria. Karibu sana.

Comments are closed.