Sheria Leo. Haki ni Nini?

Utangulizi

Karibu sana ndugu msomaji na mfuatiliaji wa ukurasa huu wa Sheria Leo. Kama kawaida yetu lengo la kukuletea makala hizi fupi ni kukusaidia kuishi kwa mujibu wa sheria kila siku. Leo tunakwenda kujibu swali la Haki ni Nini?

Ndugu msomaji watu wengi wamekuwa wakisema na kudai vitu mbali mbali na kusema ni Haki yangu. Nadhani umeshawahi kusikia mtu akisema ‘Hii ni haki yangu’ au ‘ameninyang’anya haki yangu’au ‘nipatie haki yangu’. Je, unafahamu nini maana ya neno HAKI. Fuatana nami katika kujifunza katika darasa la Sheria Leo. Karibu.

Neno Haki kwa tafsiri ya kamusi ya Kiswahili sanifu lina maana ya ‘jambo ambalo mtu anastahiki au kitu anachostahili kuwa nacho.

Kwa tafsiri ya kamusi ya kisheria neno Haki lina maana ‘kile mtu anachostahili kuwa nacho au kile anachoruhusiwa kufanya, au kile anachostahili kupokea kutoka kwa wengine kwa mujibu wa sheria’.

Kwa tafsiri hii tunaweza kuona kuwa sheria ndio msingi wa haki, sheria ndio inasema kile unachostahili kuwa nacho au unachoruhusiwa kufanya au unachotakiwa kupata kutoka kwa wengine. Kwa maana pana zaidi tunaweza kusema Haki ni maslahi ya mtu ambayo yanatambuliwa na kulindwa na sheria.

Katika sheria zetu za Tanzania zipo haki mbali mbali zinazotambuliwa kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya 1977. Haki hizi zinafafanuliwa kupitia sheria mbali mbali zilizotungwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na mamlaka nyingine zenye uwezo wa kutunga sheria. Mfano wa haki hizo ni; haki ya usawa, haki ya kuishi, haki ya uhuru binafsi, haki ya kufanya kazi na haki ya kumiliki mali.n.k.

Dondoo

  • Haki ni kile mtu anachostahili kuwa nacho, au unachoruhusiwa kufanya au kupata kutoka kwa wengine
  • Sheria ndio inatoa haki au kutambua haki za watu. Hivyo ili ujue haki yako ni ipi lazima uijue sheria inayotoa haki hiyo.
  • Haki endapo itavunjwa mwenye haki anaweza kuchukua hatua za kisheria kupata haki yake.

Ndugu msomaji fahamu haki zako na jinsi ambavyo zinalindwa na sheria na endapo zitavunjwa fuata hatua zinazotakiwa kupata haki yako.

Kumbuka ‘kutokujua sheria si utetezi iwapo utatenda kosa lolote’ tafuta maarifa sahihi ya kisheria yakusaidie kufanya maamuzi sahihi. Wasiliana nami kupitia www.ulizasheria.co.tz

Wako

Isaack Zake, Wakili