Sheria Leo. Je, ni Lazima wewe kujua Sheria?

Karibu tena katika ukurasa wetu wa uliza sheria ndugu yangu. Leo tunataka kujibu swali juu ya ‘Je, ni lazima wewe kujua Sheria?’

Mara nyingi watu wanadhani kuwa ujuzi wa sheria unawahusu wanasheria pekee au watu wenye shughuli fulani za umma na kadhalika. Sheria ni jambo la kijamii na linamuhusu kila mmoja wetu.

Kama ni mfuatiliaji wa makala hizi na nyingine tunazoandika utakuwa unaona kila tukimalizia makala tunaandika maneno haya ‘kutokujua sheria si utetezi iwapo utatenda kosa lolote’ maneno haya yana msingi sana katika mada ya leo. Maneno haya si kibwagizo tu cha kukuhamasisha ufahamu sheria bali maneno hayo ni sheria yenyewe.

Katika Sheria ya Makosa na Adhabu Sura 16, Kifungu cha 8 kinaeleza bayana kuwa ‘Kutokujua sheria hakuwezi kutumika kama utetezi kwa mtu endapo atakuwa ametenda kosa’. Ndio, ndugu msomaji sheria inaweka wazi kuwa wewe una wajibu wa kujua sheria. Ni LAZIMA WEWE KUZIJUA SHERIA, kwani kwa kutozijua na endapo utatenda kosa lolote kwa kujua au kutokujua, sheria itakuadhibu tu pasipo huruma ya kuwa hukujua. Huo ndio mtazamo wa sheria kwa kila mwananchi au mwanajamii husika ambaye sheria hiyo imetungwa kutumika katika mazingira yake.

Msingi wa mtazamo huu wa kisheria ni kuondoa hali ya kila mmoja akitenda kosa kukimbilia utetezi kwamba sikujua kuwa hili ni kosa.

Ndugu msomaji ni muhimu sana kutafuta maarifa ya sheria katika kila eneo la maisha yako ili matendo yako na yale ambayo unasema yawe kwa mujibu wa sheria. Nakupa ushauri usiache kutembelea mtandao wetu ili uendelee kupata maarifa ya kisheria kila siku.

Kumbuka ‘kutokujua sheria si utetezi iwapo utatenda kosa lolote’ tafuta maarifa sahihi ya kisheria yakusaidie kufanya maamuzi sahihi kila siku. Wasiliana nasi kwa kutembelea mtandao wako wa  www.ulizasheria.co.tz

Nakutakia siku njema.

Wako

Isaack Zake, Wakili

3 replies
 1. Datius Deus
  Datius Deus says:

  Your Message… (*)Asante sana bro Isaack kwa maarifa aya.Mimi Binafsi kazi zangu ni kusimamia sheria za nchi zisivunjwe na kulinda raia na mali zao.Lakini kwa upande wa sheria zenyewe sipo vizuri hata kidogo,sasa kupitia makala zako nadhani ntajifunza mengi na kufanya kazi zangu kwa uweledi.Asante sana.

  • ulizasheria
   ulizasheria says:

   Karibu sana ndugu yangu Datius Deus naamini utaendelea kupata kitu cha kukusaidia kwenye blog hii ili kutekeleza majukumu yako vizuri. nakutakia utendaji mzuri wa majukumu makubwa uliyonayo kwa Taifa.

 2. Datius Deus
  Datius Deus says:

  Your Message… (*)Asante sana Isaack kwa Maarifa aya.Mimi binafsi kazi zangu ni kusimamia sheria za nchi zisifunjwe,ikiwa ni pamoja na kulinda usalama wa raia na mali zake. Lakini kwenye upande wa sheria zenyewe sipo vizuri hata kidogo.Sasa kupitia kurasa zako naamini ntajifunza mengi na kuweza kutekeleza majukumu yangu kwa weledi.

Comments are closed.