Sheria Leo. Je, Sheria ni Muhimu?

Karibu sana ndugu msomaji wa ukurasa wa Sheria Leo, ambapo tunajifunza mambo mbalimbali ya kisheria ambayo yatatusaidia kila siku kufanya maamuzi sahihi na kuishi kwa mujibu wa sheria. Leo tunakwenda kujibu swali linalosema ‘Je, Sheria ni Muhimu?’ Karibu sana.

Ndugu msomaji ni wazi kabisa mtu hawezi kuhangaika kutafuta kitu au maarifa ya jambo fulani kama halina umuhimu katika maisha yake. Kila siku tunaamka na kwenda kwenye shughuli zetu kutafuta mambo ambayo tunaona ni muhimu kwetu, mfano chakula, mavazi na hata malazi. Tunafahamu umuhimu wa vitu hivi na maana yake katika maisha yetu ndio maana kila kukicha tunatafuta.

Wengi wetu tunadhani kuwa sheria si muhimu kwetu au inawahusu watu fulani au tabaka fulani jambo hili si kweli, sheria inawahusu watu wote. Hivyo ni muhimu kwa kila mtu kuzifahamu sheria. Huwezi kuingia gharama ya kutafuta jambo kama hufahamu maana ya jambo hilo  katika maisha yako.

Kabla hatujajibu swali letu la Je, Sheria ni Muhumu? karibu tuone kwa ufupi nini maana ya Sheria.

Sheria ni mfumo kanuni na taratibu zilizowekwa kwenye jamii na mamlaka kwa ajili ya kuwaongoza matendo yao na mahusiano yao. Sheria ni utaratibu unaotengeneza mfumo na mwelekeo wa maisha chini ya mamlaka husika. Mfano kanuni katika nchi, familia, ukoo, shule na ofisi nk.

Kwa ufafanuzi wa ziada ya maana ya sheria bonyeza hapa Nini Maana ya Sheria?

Kwa maana hii tunaweza kuona umuhimu wa sheria kwani pasipo sheria jamii haiwezi kukaa kwa pamoja na kuweza kustawi na kuwa na maendeleo. Sheria ni muhimu sana kwani ndizo zinaongoza matendo yako na tabia yako kila siku unavyopaswa kuishi katikati ya jamii. Uhuru ambao tunaona tunao ni kwa mujibu wa sheria. Sheria inaongoza kitu cha kuongea, kitu cha kufanya na kitu gani haupaswi kufanya. Ni sawa kusema sheria ni mfumo unaoongoza maisha yetu ya kila siku.

Ndugu msomaji ni muhimu ufahamu kuwa kila unalofanya au usilofanya au unalotamka lina sheria yake au mwongozo wake ambao wewe unapaswa kujuua. Sheria ni mfumo wa ajabu sana ambao unaratibu maisha yako tangu ukiwa tumboni kwa mama yako na hata ukiwa kaburini. Zipo sheria zinazuia utoaji wa mimba (Sheria ya Kanuni ya Adhabu Sura 16 ya Sheria – The Penal Code) na hata sheria ya makaburi (Sheria ya Kuhamisha Makaburi Sura 72 – The Grave (Removal) Act).

Ndugu msomaji kama kuna sheria inayoratibu maisha yako ukiwa bado hujazaliwa na kuna sheria inayoratibu hata masalia ya mwili wako ukiwa umezikwa, je, si zaidi sana kuna sheria za kuratibu maisha yako kila siku.

Unachotakiwa kufanya ndugu yangu kila siku kabla ya kutekeleza maamuzi yoyote iwe kwa maneno au vitendo angalia kama upo kwa mujibu wa sheria.

Kumbuka ‘kutokujua sheria si utetezi iwapo utatenda kosa lolote’ tafuta maarifa sahihi ya kisheria yakusaidie kufanya maamuzi sahihi kila siku. Wasiliana nami kwa kutembelea mtandao wako wa  www.ulizasheria.co.tz

Wako

Isaack Zake, Wakili

4 replies
  1. Marbel
    Marbel says:

    Asante sana Bwana Wakili kwa shule ya leo…
    Nimepata kujua kwamba Kuna sheria ya makaburi jambo ambalo sikulifahamu awali..

Comments are closed.