Sheria Leo. Maisha ni Haki yako
Karibu sana ndugu msomaji na mfuatiliaji wa mtandao wako wa www.ulizasheria.co.tz. tunapenda kutambulisha kwako ukurasa ambao unakupa mwongozo wa maisha yako ya kila siku kujiufunza kuishi kwa mujibu wa sheria. Ukurasa huu unakupa ufafanuzi wa baadhi ya mambo ya kisheria ambayo tunakutana nayo na tunayaishi kila siku. Karibu sana ndugu msomaji tujifunze kwa pamoja.
Kama nilivyotambulisha hapa juu katika ukurasa wa Sheria leo tunakwenda kuchambua kwa ufupi juu ya MAISHA NI HAKI YAKO. Kama wewe ni mwanadamu au umezaliwa katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, basi Katiba ya JMT inaeleza wazi wazi kuwa kila mwananchi anayo haki ya kuishi. Ibara ya 14 ya Katiba ya JMT inasema ‘kila mtu anayo haki ya kuishi na kupata hifadhi ya maisha yake kwa jamii kwa mujibu wa sheria’. Ndugu msomaji Sheria mama ya Taifa hili inatambua kuwa wewe una haki ya kuishi na jamii inapaswa kulinda maisha yako. Pamoja na kupewa haki hiyo ya maisha maana yake na wewe kama sehemu ya jamii unao wajibu wa kulinda maisha ya wengine katika jamii.
Hivi karibuni tumekuwa tunashuhudia mauaji ya kutisha na watu kadhaa kushabikia vitu hivyo huku upendo baina ya wananchi umepungua sana. Ni rai yangu siku ya leo upate muda wa kutafakari juu ya haki hii ya maisha ambayo imehakikishwa katika Katiba ya JMT ambapo muda wote wanajamii wamejitoa kukulinda wewe ikiwa unajua au hujui ni wajibu wako sasa kujitoa kulinda maisha ya wanajamii wenzako. Ndugu yangu uliyepata nafasi ya kuishi leo, heshimu haki hiyo kwako na kwa ajili ya wengine.
Kumbuka ‘kutokujua sheria si utetezi iwapo utatenda kosa lolote’ tafuta maarifa sahihi ya kisheria yakusaidie kufanya maamuzi sahihi kila siku. Wasiliana nami kupitia www.ulizasheria.co.tz
Nakutakia siku njema sana ndugu yangu
Wako
Isaack Zake, Wakili
Sawa
Karibu