Sheria leo. Ishi kwa Sheria si kwa Mazoea

Ndio ndugu msomaji kama kauli inavyosema hapo juu kwamba usiishi kwa mazoea bali jifunze kuishi kwa Sheria. Kama tulivyojifunza Sheria ni mwongozo au kanuni zilizowekwa kuongoza mwenendo wa wanajamii katika jamii yao. Watu wengi wamezoea kuishi kwa mazoea katika kila eneo ikiwa nyumbani, kazini,njiani n.k.

Napenda kukupa mfano wa jinsi mazoea yanavyoweza kukuingiza kwenye matatizo ya kisheria. Hivi karibuni kikosi cha usalama barabarani kilifanya operesheni kukamata magari katikati ya mji wa Dar yale yaliyokuwa yanakiuka sheria za barabarani hasa kwa matumizi ya barabara. Ikumbukwe tangu kuanzishwa njia ya Mwendokasi zaidi ya mwaka mmoja sasa, barabara kadhaa za katikati ya mji zilibadilishwa matumizi na watumiaji walijulishwa kwa njia mbalimbali. Hata hivyo kama ilivyo mazoea ya watu hawakuchukulia maanani. Siku operation imefanyika walikamatwa madereva wengi sana na wote utetezi wao ni kuwa njia hii tulikuwa tunapita kila siku mbona hatukukamatwa. Askari wa barabarani walikuwa watulivu na kuwachukua madereva na kuwaonesha alama za barabarani zinazoonesha matumizi ya barabara husika. Kilichofuata madereva wote walipigwa faini ya Tsh.30,000/- kila mmoja.

Ndugu msomaji katika kadhia hii ambayo iliwakuta madereva wengi sana nilijifunza jambo kuwa inawezekana unaishi kwa mazoea na katika mazoea hayo kumbe unatenda makosa, siku ukikamatwa utaadhibiwa kwani mazoea yako hayahalalishi makosa unayoyafanya. Sheria inabaki sheria haiwezi kubadilishwa na mazoea yako. Hivyo ni muhimu sana katika maisha yako na mwenendo wako kujiuliza katika eneo hili sheria inasema nini?

Kumbuka ‘kutokujua sheria si utetezi iwapo utatenda kosa lolote’ tafuta maarifa sahihi ya kisheria yakusaidie kufanya maamuzi sahihi kila siku. Wasiliana nami kupitia www.ulizasheria.co.tz

Nakutakia siku njema sana ndugu yangu

 

Wako

Isaack Zake, Wakili

2 replies

Comments are closed.