Sheria Leo. Wajibu ni Nini?
Utangulizi
Karibu tena ndugu msomaji wa ukurasa wa Sheria Leo, asante kutupatia nafasi ya kuendelea kukuletea majibu mbali mbali ya kisheria ambayo wewe au jamii imekuwa ikijiuliza kila siku. Lengo letu ni lile lile kukupatia maarifa ya kukusaidia kufanya maamuzi sahihi kila siku. Leo katika darasa la Sheria tunakwenda kujibu swali la Nini Maana ya Wajibu? Karibu sana.
Ndugu msomaji neno wajibu au kuwajibika si neno geni masikioni mwetu. Tunalisikia kila siku na inawezekana leo umelitamka ukisema ‘Nipo nawajibika’ au ‘naenda kuwajibika’ au unasikia mtu anasema ‘mwanaume huyu hawajibiki’ hivyo neno hili ni la kawaida sana na lina matumizi ya kila siku katika jamii.
Kwa mujibu wa kamusi ya Kiswahili sanifu neno wajibu lina maana ya ‘jambo linalomlazimu mtu kulitimiza; jambo ambalo mtu hana hiari nalo katika kulifanya; sharti, faradhi, jukumu.
Kwa tafsiri kutoka kwenye kamusi ya kisheria neno wajibu lina maana ya ‘tendo au vitendo ambavyo mtu analazimika kufanya kwa mujibu wa sheria’.
Kwa tafsiri hii tunaweza kuona kuwa sheria ndio msingi wa wajibu, sheria ndio inaeleza kile ambacho wewe mwananchi unawajibika kukifanya. Maana yake unashurutishwa kufanya kwa sheria.
Katika sheria zetu za Tanzania upo wajibu mbali mbali unaotambuliwa kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya 1977. Wajibu huu unafafanuliwa kupitia sheria mbali mbali zilizotungwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na mamlaka nyingine zenye uwezo wa kutunga sheria. Mfano wa wajibu huo ni; wajibu wa kushiriki katika kufanya kazi, wajibu wa kuzingatia na kutii sheria zote za nchi, wajibu wa kulinda na kutunza mali ya umma na wajibu wa kuilinda nchi.
Dondoo
- Wajibu ni kile ambacho mtu analazimika kufanya kwa mujibu wa sheria
- Sheria ndio inatoa na kuainisha ni nini wajibu wa wana jamii
- Endapo mtu atakiuka kutimiza wajibu wake kuna hatari ya kuadhibiwa kwa mujibu wa sheria.
Ndugu msomaji tambua na fuatilia wajibu wako kama mwananchi ili utekeleze kila siku, kwani kushindwa kwako kunaweza kusababisha adhabu kwa mujibu wa sheria.
Kumbuka ‘kutokujua sheria si utetezi iwapo utatenda kosa lolote’ tafuta maarifa sahihi ya kisheria yakusaidie kufanya maamuzi sahihi. Wasiliana nami kupitia www.ulizasheria.co.tz
Wako
Isaack Zake, Wakili
Your Message… (*)HONGERA SN WAKILI MSOMI KWA KUWAZA HILI JAMBO. MAANA NI WENGI TUTAFAIDIKA KWA HII BLOG. BARIKIWA SN
Asante sana Furaha kwa kuona thamani ya kazi hii, endelea kufuatilia na kuuliza maswali nasi tutakuwa tayari kukujibu. Karibu sana
Nimeelewa kwa ufasaha maana ya wajibu, nilikuwa naielewa kirahisi rahisi.
Karibu sana Kuyela