Sheria Leo. Je, unajua Haki na Wajibu vinategemeana?

Utangulizi

Karibu sana ndugu msomaji wa ukurasa huu wa Sheria Leo . ukurasa ambao unakupa maarifa juu ya sheria na kukusaidia kuishi kwa mujibu wa sheria kila siku. Lengo mojawapo la ukurasa huu ni kukufahamisha juu ya Haki na Wajibu wako kama raia au mwananchi wa Tanzania. Leo tunakwenda kuchambua kwa uchache juu ya maneno haya yaani Haki na Wajibu. Karibu sana tujifunze kwa pamoja.

Maana za maneno Haki na Wajibu

Neno Haki lina maana ‘kile mtu anachostahili kuwa nacho au kile anachoruhusiwa kufanya, au kile anachostahili kupokea kutoka kwa wengine kwa mujibu wa sheria’na neno Wajibu ‘tendo au vitendo ambavyo mtu analazimika kufanya kwa mujibu wa sheria’. Kwa ufafanuzi zaidi kwenye maana ya maneno haya soma Sheria Leo.5: Haki ni Nini? Sheria Leo.6:Wajibu ni Nini?

Ndugu msomaji kuna msemo usemao kuwa ‘hakuna haki isiyo na wajibu’ msemo huu ni kweli kabisa. Kama tulivyoona maneno haya yaani Haki  na Wajibu asili yake ni sheria yaani yanatokana na sheria.

Kumekuwa na watu wanapenda sana kulalamika wakidai kuhusu haki yaani wanadai kitu ambacho  wanadhani wanastahili au wanachoruhusiwa kufanya, au wanachodhani wanastahili kupokea, ila si watu wanaofuatilia kuhusu wajibu unaoambatana na haki hiyo.

Ni muhimu kufahamu kwamba haki inaambatana na wajibu mara nyingi, kama kuna haki unazodai kama raia basi hakikisha unafahamu wajibu unaoambatana na haki hizo kama raia. Tafuta kujua wajibu wako na wajibika kutekeleza ipasavyo ndipo haki inayohusika na wajibu huo utaipata.

Katiba ya JMT inaeleza kuwa kila mtu ana haki ya kumiliku mali, haimaanishi kwamba unaweza kwenda mahakamani na kudai upewe mali na wewe umiliki, bali unapaswa kufanya kazi halali ili kukuingizia kipato halali na kuweza kupata mali kwa mujibu wa sheria.

Haki na wajibu ni kama pande mbili za shilingi huwezi kuzitenganisha zina thamani sawa katika kufanya shilingi iwe na thamani katika maisha yetu ya kila siku.

Tafuta kwanza kujua wajibu wako, tekeleza wajibu wako kila siku utapata haki yako kila siku.

Nakutakia siku njema katika kuwajibika.

Kumbuka ‘kutokujua sheria si utetezi iwapo utatenda kosa lolote’ tafuta maarifa sahihi ya kisheria yakusaidie kufanya maamuzi sahihi. Wasiliana nami kupitia www.ulizasheria.co.tz

Wako

Isaack Zake, Wakili