Sheria za Jinai

Utangulizi

Karibu ndugu yangu msomaji na mfuatiliaji wa ukurasa wetu. Tunaendelea kukuletea maarifa ya kisheria kwa uchambuzi wa masuala kadhaa ya kisheria. Leo tunakuletea ufafanuzi juu ya  Sheria za Jinai. Karibu tujifunze.

Katika mfululizo wa makala zilizopita tuliweza kuona juu ya Sheria za Umma na Binafsi. Katika makala hizo tumepata mwanga wa kufahamu makundi ya sheria na namna tunavyoweza kuhusiana nazo.

Maana ya Sheria za Jinai

Ni vizuri kabla ya kujibu swali juu ya maana ya sheria za Jinai ni vyema kufahamu neno Jinai lina maana gani.

Maana ya Jinai ni kitendo kinachofanywa na mtu ambacho kimekatazwa na sheria na kinafutatiwa na adhabu kwa mkosaji ikidhibitika  juu ya kosa husika. Jinai inaweza kutazamwa kuwa ni kitendo kinachotishia, kuumiza au kutishia juu ya mali, afya au usalama na ustawi wa jamii ambacho sheria inakataza.

Ili kosa liwe jinai linatakiwa likidhi vigezo muhimu angalau vitatu;

 • Kiwe kitendo ambacho kimeleta madhara kwa mtu au vitu, kitendo ambacho Mamlaka zimewekwa ili kuzuia kisitokee
 • Kitendo hicho endapo kimetendwa, kiwe kimeanishwa adhabu yake
 • Uwepo wa namna ya mashitaka ambayo yatadhibitisha hatia ya mtu aliyetenda kitendo hicho.

Hivyobasi sheria za Jinai ni kundi la sheria ambazo zinaainisha makosa na adhabu ambazo zinatolewa kwa watu ambao wanakiuka sheria. Sheria hizi zinatoka katika kundi kubwa la Sheria za Umma ambazo tayari tumeziangalia katika makala zilizopita. Hii ina maana kuwa Sheria za Jinai endapo kosa litafanyika Serikali inachukua hatua ya kumkamata mtuhumiwa na kumfikisha mahakamani.

Nchi yetu ya Tanzania ina sheria nyingi zinazoainisha makosa na adhabu (Sheria za Jinai). Mfano wa sheria hizo ni;

 • Kanuni ya Adabu, Sura ya 16 (The Penal Code)
 • Sheria ya Uhujumu Uchumi, Sura ya 200 (The Economic and Organized Crime Control Act)
 • Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa, Sura ya 329 (The Prevention and Combating of Corruption Act)

Malengo makuu ya Sheria za Jinai

Sheria za jinai zina malengo kadhaa;

 • Kuadhibu: lengo hili linafikiwa pale mtenda kosa anatiwa hatiani na adhabu kutolewa kulingana na kosa lake. Katika kuadhibiwa mkosaji anapoteza baadhi ya haki zake ambazo angeweza kuzitumia iwapo asingetenda kosa. Adhabu inaweza kuwa kifungo cha muda gerezani, au kulipa faini, au kuchapwa viboko n.k.
 • Kuzuia: sheria za kijinai pia zinalenga kuzuia utendaji wa makosa mengine au watu wengine kutenda kama wakosaji waliotangulia. Adhabu zinazotolewa zinawatia hofu watu wengine nao kujiepusha na matendo kama ya wakosaji. Ndio maana adhabu ikitolewa mahakama inasema ‘…adhabu hii iwe onyo kwako na kwa watu wenye nia kama yako…
 • Kutenga wakosaji na jamii: sheria za jinai zinasaidia wakosaji kutengwa mbali na jamii ili wasiendeleze makosa yao na kuiumiza jamii. Hapa wakosaji wanaweza kupata adhabu ya kifungo cha muda mrefu au kifungo cha maisha au kifo.
 • Kurekebisha: hali kadhalika ni malengo ya sheria za jinai kusaidia marekebisho au matengenezo ya wakosaji ili kuwa wanajamii wenye mchango kwa jamii pindi watakapomaliza adhabu zao. Yapo mafunzo wanapata wafungwa wakiwa magerezani na wanapotoka wanakuwa na ujuzi unaowasaidia kuwa na mchango kwa jamii.
 • Kurudisha/kurejesha hali ya mwathiriki: lengo hili ni kumsaidia yule aliyeathirika kurudi katika hali yake ya awali kabla kosa halikufanyika. Mara kadhaa mahakama imekuwa ikitoa adhabu ya kulipa fidia kwa aliyekosewa.

Hitimisho

Kundi hili la sheria za Jinai ni muhimu sana kwa wananchi kuzijua ili kujiepusha na makosa haya kwani madhara yake ni makubwa endapo watapatikana na hatia.

Kumbuka ‘kutokujua sheria si utetezi iwapo utatenda kosa lolote’ tafuta maarifa sahihi ya kisheria yakusaidie kufanya maamuzi sahihi kila siku. Wasiliana nami kwa kutembelea mtandao wako wa  www.ulizasheria.co.tz

Wako,

Isaack Zake, Wakili