Sheria Leo.Sheria za Madai

Utangulizi

Karibu ndugu yangu msomaji na mfuatiliaji wa ukurasa wa Sheria Leo. Tunaendelea kukuletea maarifa ya kisheria kwa uchambuzi wa masuala kadhaa ya kisheria. Leo tunakuletea ufafanuzi juu ya  Sheria za Madai. Karibu tujifunze.

Katika mfululizo wa makala zilizopita tuliweza kuona juu ya Sheria za Umma na Binafsi. Katika makala hizo tumepata mwanga wa kufahamu makundi ya sheria na namna tunavyoweza kuhusiana nazo. Leo tunaangalia kundi lingine la sheria za Madai.

Maana ya Sheria za Madai

Sheria za madai ina maana ya kundi la sheria linaloeleza na kulinda haki binafsi za watu au Taasisi, kutoa nafuu (fidia)  katika mgogoro/kesi endapo haki hizo zimekiukwa.

Ili kosa liwe la madai linatakiwa likidhi vigezo muhimu angalau vinne;

  • Lazima kuwe na wajibu wa kisheria ambao mtu anapaswa kuutekeleza kwa mtu mwengine au Taasisi fulani
  • Kwamba mtu awe ameshindwa kutekeleza wajibu huo, na kushindwa huko kumeathiri haki za mtu mwengine au Taasisi
  • Kushindwa huko kutimiza wajibu kuwe kunatoa nafuu ya fidia au kulazimishwa kutimizwa wajibu kwa yule ambaye amekosa haki yake kwa wajibu kutotimizwa
  • Uwepo wa namna ya mashitaka ambayo yatadhibitisha hatia ya mtu aliyeshindwa kutimiza wajibu.

Hivyobasi sheria za madai ni kundi la sheria ambazo zinaainisha wajibu na haki  ambazo zinatolewa kwa watu ambao wanakiuka sheria inayohusu mambo binafsi. Sheria hizi zinatoka katika kundi kubwa la Sheria Binafsi ambazo tayari tumeziangalia katika makala zilizopita.

Hii ina maana kuwa Sheria za Madai endapo kosa litafanyika mtu binafsi au Taasisi iliyoathiriwa inachukua hatua ya kufuata taratibu za kisheria kupatiwa haki yake iliyokiukwa ikiwa ni pamoja na kumfikisha mahakamani  aliyeshidhwa kutimiza wajibu ili kupata fidia stahiki.

Tanzania ina sheria nyingi zinazoainisha haki na wajibu ambao wananchi na Taasisi zinatakiwa kuzingatia. Mfano wa sheria hizo ni;

  • Sheria ya Mikataba
  • Sheria ya Madhara
  • Sheria zinazohusu Mali

Lengo la Sheria za Madai

Lengo kuu la sheria za madai ni Kufidia, ikiwa ni kwa vitendo vya kutimiza wajibu au kwa fedha yaani kumrudisha mwathirika wa kosa la madai kurudi katika hali yake ya awali kama vile kosa halikutendeka.

Tofauti kati ya makosa ya madai na makosa ya jinai

  • Mashitaka: katika kosa la jinai mashitaka yanafunguliwa na kusimamiwa na Serikali wakati kwenye kosa la madai mashitaka yanafunguliwa na kusimamiwa na mwathiriwa mwenyewe.

 

  • Lengo la sheria: lengo la sheria za jinai ni kuadhibu kwa mfano kifungo au faini ambayo inalipwa kwa Serikali, kwa upande mwengine lengo la sheria za madai ni kufidia ambapo mnufaika ni yule aliyeathiriwa na kosa.

 

  • Kosa: kosa la jinai mtuhumiwa anakuwa amevunja wajibu alionao kwa Jamhuri (serikali) wakati kwenye kosa la madai mtuhumiwa anakuwa amevunja wajibu alionao kwa mtu au Taasisi.

 

  • Uondoaji wa shitaka: katika kosa la jinai aliyeathiriwa hawezi kuondoa shitaka likiwa mahakamani kwani ni maslahi ya Jamhuri, ndio yenye uwezo huo wakati kwenye makosa ya madai aliyefungua shitaka anaweza kuliondoa mahakamani.

Hitimisho

Kundi hili la sheria za madai ni muhimu sana kwa wananchi kuzijua ili kujiepusha na makosa haya kwani madhara yake ni makubwa inahusisha kudaiwa fidia. Pia ni muhimu kufahamu kwa mwananchi kuwa si kila kosa ni la jinai mengine ni ya madai wanaweza kuchukua hatua na kudai haki zao zilizokiukwa.

Kumbuka ‘kutokujua sheria si utetezi iwapo utatenda kosa lolote’ tafuta maarifa sahihi ya kisheria yakusaidie kufanya maamuzi sahihi kila siku. Wasiliana nami kwa kutembelea mtandao wako wa  www.ulizasheria.co.tz

Wako,

Isaack Zake, Wakili