Ijue Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Utangulizi

Karibu ndugu yangu msomaji na mfuatiliaji wa ukurasa wetu. Tunaendelea kukuletea maarifa ya kisheria kwa uchambuzi wa masuala kadhaa ya kisheria. Katika makala zilizotangulia tulijifunza juu ya maana ya sheria, na makundi ya sheria. Katika mfululizo huu unaoanza leo tutakuwa tunaelezea kwa kifupi baadhi ya Sheria ambazo tunahusiana nazo siku kwa siku. Lengo ni kukusaidia ndugu msomaji kuwa makini na ufahamu juu sheria ambazo kwa kujua au kutokujua zinakuhusu ili kukusaidia kuchukua hatua zinazostahili. Leo tutaanza kuichambua kwa ufupi Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Maana ya Katiba

Katiba inaweza kutafsiriwa kama sheria kuu ya nchi au sheria mama ya nchi fulani. Katiba ni msingi wa uendeshaji wa mambo yote katika nchi. Katiba inamaanisha makubaliano au mkataba kati ya watawaliwa na watawala.

Historia ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Taifa la Tanzania lilipata uhuru mwaka 1961 kama Tanganyika na baadae baada ya mapinduzi ya Zanzibar ya tarehe 12 Januari 1964, nchi hizi mbili ziliungana na kuunda nchi moja ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Katika kipindi chote hicho tangu uhuru wa Tanganyika (Tanzania Bara) hata sasa nchi hii imekuwa na historia ya Kikatiba kama ifuatavyo;

  • Katiba ya Uhuru (The Independent Constitution) – 1961: Katiba hii iliandaliwa na Uingereza ambapo kiongozi mkuu wa shughuli za Serikali alikuwa Hayati Mwl.Julius Nyerere kama Waziri Mkuu wa kwanza wa Tanganyika huru. Katika Katiba hii iliruhusu na uwepo wa vyama vingi.
  • Katiba ya Jamhuri (The Republic Constitution) – 1962: Hapa Tanganyika ilitambulika kama Jamhuri na kuanzishwa madaraka ya Rais wa Jamhuri ambaye alikuwa Hayati Mwl.Julius Nyerere.
  • Katiba ya Muda (The Interim Constitution) – 1965: Katiba hii ilikuja kama suluhisho la Muungano wa Tanganyika na Zanzibar. Katika Katiba hii vyama vingi vilifutwa na kutambuliwa chama kimoja tu yaani TANU kwa upande wa Tanganyika na ASP kwa upande wa Zanzibar.
  • Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (The United Republic Constitution of Tanzania) – 1977: Katiba hii iliwekwa kukidhi haja ya muungano wa nchi mbili yaani Tanganyika na Zanzibar. Katiba hii ndiyo inatumika hata sasa kulingana na mabadiliko ya mara kwa mara yaliyofanyika.

Mambo ya Kuzingatia

  • Uundwaji wa katiba zote hizi tangu mwaka 1961 hata ya mwaka 1977 ambayo inatumika mpaka sasa haikuhusisha maoni ya wananchi bali kulikuwa na Wabunge ambao waliunda Bunge la Katiba.
  • Tanzania ilianza mchakato wa kuundwa kwa Katiba mpya mnano mwaka 2013/2014 ambao bado haujakamilika. Mchakato huu ulihusisha ukusanyaji wa maoni ya wananchi kila mahali Tanzania Bara na Zanzibar.

Mambo ya Msingi yanayoainishwa katika Katiba ya Jamhuri ya Muungano

Kama tulivyoeleza awali Katiba ni Sheria mama ya taifa lolote na inaainisha muundo wa mihimili ya dola na utendaji kazi wake. Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania 1977 ina sura zifuatazo

  • Sura ya Kwanza: Jamhuri ya Muungano, Vyama vya Siasa, Watu na siasa ya Ujamaa na Kujitegemea
  • Sura ya Pili: Serikali ya Jamhuri ya Muungano
  • Sura ya Tatu: Bunge la Jamhuri ya Muungano
  • Sura ya Nne: Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Baraza la Mapinduzi la Zanzibar na Baraza la Wawakilishi la Zanzibar
  • Sura ya Tano: Utoaji Haki katika Jamhuri ya Muungano, Mahakama Kuu ya Jamhuri ya Muungano, Tume ya Kuajiri ya Mahakama ya Tanzania Bara, Mahakama Kuu ya Zanzibar, Mahakama ya Rufani ya Jamhuri ya Muungano na Mahakama Maalum ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano
  • Sura ya Sita: Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora na Sekretarieti ya Viongozi wa Umma
  • Sura ya Saba: Masharti kuhusu Fedha za Jamhuri ya Muungano
  • Sura ya Nane: Madaraka ya Umma
  • Sura ya Tisa: Majeshi ya Ulinzi
  • Sura ya Kumi: Mengineyo

Hitimisho

Katiba ya Jamhuri ya Muungano ya Tanzania ndio msingi wa mamlaka zote za Tanzania ambapo kila chombo cha kisheria kunapata uhalali wa mamlaka na utendaji wake kutoka kwenye Katiba. Sheria zote zinapaswa kutungwa kwa mujibu wa Katiba.

Hivyo ni muhimu sana kwa mwananchi kuifahamu Katiba ya Tanzania kwa lengo la kufahamu mambo yote yaliyoainishwa kwenye Katiba kufahamu haki na wajibu wake na mipaka ya madaraka.

Uliza Sheria itaandaa utaratibu wa uchambuzi wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika ukurasa maalum, usikose kufuatilia.

Kumbuka ‘kutokujua sheria si utetezi iwapo utatenda kosa lolote’ tafuta maarifa sahihi ya kisheria yakusaidie kufanya maamuzi sahihi kila siku. Wasiliana nami kwa kutembelea mtandao wako wa  www.ulizasheria.co.tz

Wako,

Isaack Zake, Wakili