3 A: Taasisi za Kazi

Utangulizi

Ndugu msomaji leo tunaendelea kufanya uchambuzi juu ya sheria za kazi. Kama hukupata kusoma makala iliyopita fuatilia somo Ijue sheria ya Kazi. Leo tunakwenda kuangalia juu ya Taasisi za Kazi.

Ndugu msomaji, wafanyakazi wengi  na waajiri wengi wanakutana na changamoto mbali mbali katika kutekeleza majukumu yao. Hatahivyo changamoto inakuja pale  linapojitokeza  tatizo wanataka kulitatua wanaanzia wapi? au wanaenda kwenye chombo gani ili kupata majibu sahihi.

Katika makala hii tunakwenda kuangalia Taasisi za Kazi, vyombo vilivyoundwa kuhakikisha Sheria ya Kazi na Mahusiano Kazini inatekelezwa kikamilifu.

Lengo la uchambuzi huu

  • Kuzifahamu Taasisi zinazosimamia Sheria ya Kazi
  • Kufahamu muundo wa Taasisi
  • Kufahamu majukumu ya Taasisi
  • Kufahamu mamlaka ya Taasisi

Nini Maana ya Taasisi za Kazi

Taasisi za Kazi ni vyombo vya kisheria ambavyo vimeundwa kwa lengo la kuwezesha utekelezaji wa Sheria ya Kazi na Mahusiano Kazini. Taasisi hizi zimeundwa na Sheria ya Taasisi za Kazi Na.7 ya 2004.

Taasisi za Kazi zimeundwa kutekeleza majukumu ya ushauri, usimamizi, kuzuia na kutatua migogoro ya kazi. Katika makala hii tutakwenda kuzichambua moja baada ya nyingine kuangalia muundo, kazi na mamlaka wa taasisi hizi.

  1. Baraza la Kazi, Uchumi na Jamii ( BARAZA)

Baraza la Kazi, Uchumi na Jamii linaundwa kwa lengo la kuishauri Serikali juu ya mambo ya kazi, uchumi na jamii kwa ujumla.

Baraza linaundwa na wajumbe 17, Mwenyekiti, Wajumbe 4 wanaowakilisha wafanyakazi, wajumbe 4 wanaowakilisha waajiri, wajumbe 4 wanaowakilisha Serikali na wataalam 4, ambao 2 upande wa wafanyakazi na 2 upande wa waajiri. Wajumbe wanakaa madarakani kwa kipindi cha miaka 3 na wanaweza kuteuliwa tena kushika madaraka.

Kazi za Baraza

Kazi za Baraza kwa ujumla zinahusisha  kuishauri Serikali kuhusu masuala yote yanayohusu Kazi, uchumi na jamii kama vile ukuzaji wa uchumi, sera za soko la ajira na mabadiliko ya sheria za kazi.

  1. Tume ya Usuluhishi wa Uamuzi (TUME)

Tume ya Usuluhishi na Uamuzi ni Idara huru ya Serikali ambayo kazi yake ni kusuluhisha na kuamua migogoro ya kazi. Tume pia inaweza kutoa ushauri na mafunzo kuhusu mbinu za kuzuia na kutatua migogoro, kusimamia uchaguzi wa vyama vya wafanyakazi na jumuiya ya waajiri.

Tume inundwa na wajumbe 7 yaani Mwenyekiti na makamishna wengine 6 ambapo makamishna 6 watatoka katika wawakilishi wa wafnyakazi 2, wawakilishi wa mwajiri 2 na wawakilishi wa serikali 2.

Tume ina mamlaka ya kumteua Mkurugenzi, Wasuluhishi na Waamuzi, kuanzisha ofisi katika maeneo na ngazi za usimamizi kama itakavyoona, kutengeneza kanuni za utendaji wake.

Wasuluhishi na Waamuzi ndio kiini cha utendaji wa Tume hii kwani hao ndio wanahusika na kutatua migogoro ya kazi inayoletwa mbele ya Tume. Utendaji wa wasuluhishi na waamuzi ni kama utendaji wa mahakama za kawaida ingawa zipo kanuni tofauti za kuongoza utendaji wao.

Mamlaka ya Wasuluhishi na Waamuzi

  • Kumwita shaurini mtu yeyote kwa ajili ya kumhoji au kuhudhuria shauri iwapo itaona mtu huyo ni muhimu katika kutatua mgogoro
  • Kumwita mtu yeyote anayehodhi nyaraka au kitu chochote kinachohusika katikaka utatuzi wa mgogoro ili ahojiwe kuhusu nyaraka au kitu hicho au akiwakilishe mbele ya Tume
  • Kuapisha, kupokea uthibitisho kutoka kwa mashahidi
  • Kumuhoji mtu yoyote kuhusu jambo lolote linalohusiana na mgogoro
  1. Kamati ya Huduma Muhimu (KAMATI)

Kamati ya Huduma Muhimu ni sehemu ya Tume na inaundwa na wajumbe 5 wenye elimu, maarifa na uzoefu wa Sheria za Ajira na Uhusiano Kazini. Kwa mujibu wa sheria za kazi zipo huduma ambazo zinabainishwa kuwa ni huduma muhimu. Huduma hizi muhimu zinamfumo wake wa utatuzi wa migogoro endapo itajitokeza.

Lengo  la sheria kuainisha huduma muhimu ni kusaidia jamii isikose huduma hizo endapo mgogoro utajitokeza walau wafanyakazi au mwajiri waruhusu huduma hizo kuendelea kutolewa kwa wastani pasipo kuathiri maslahi mapana ya jamii.

Huduma hizo ni kama maji na usafi, umeme, huduma za afya na huduma za maabara, huduma ya zimamoto, udhibiti wa safari za anga na mawasiliano ya ndege za kiraia na huduma yoyote ya usafirishaji inayohitajika kwa ajili ya kutoa huduma hizi.

Kazi za kamati;-

  • Kubainisha na kutaja huduma muhimu kwa mujibu wa Sheria
  • Kuamua migogoro inayohusiana na huduma muhimu

Kamati ina mamlaka ya;-

  • Kumwita shaurini mtu yeyote kwa ajili ya kumuhoji au kuudhuria vikao vya kamati iwapo itawezesha Kamati kutekeleza majukumu yake
  • Kumuita mtu yeyote anayehodhi nyaraka au kitu chochote kinachohusiana na kazi za Kamati ili ahojiwe kuhusu nyaraka au kitu hicho au akiwasilishe mbele ya Kamati
  • Kuapisha, kupokea udhibitisho kutoka kwa mashahidi
  • Kumuhoji mtu yeyote kuhusu jambo lolote linalohusiana na kazi za Kamati.

ndugu msomaji kwa uchambuzi wa leo tunamalizia na Taasisi hizi hata hivyo usikose kufuatilia tena uchambuzi huu kwenye makala ijayo ili kumalizia Taasisi nyingine 3 zilizobaki ya Kazi.

Usisite kunitumia maswali yako yoyote kuhusu sheria katika mtandao wako  kumbuka ‘kutokujua sheria si utetezi iwapo utatenda kosa lolote’ tafuta maarifa sahihi ya kisheria yakusaidie kufanya maamuzi sahihi. Wasiliana nami kupitia www.ulizasheria.co.tz

wako

Isaack Zake, Wakili