Ijue Sheria ya Ardhi

Utangulizi

Karibu sana ndugu msomaji wa makala ambapo umekuwa ukipata maarifa juu ya sheria mbali mbali na dhana kadhaa za kisheria kila siku. Hivi karibuni tumekuwa na mfululizo wa makala za makundi ya sheria. Makala iliyopita tulianza kuangalia juu ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Katika mfululizo huu tunakwenda kuzianisha sheria kadhaa ambazo zina matumizi ya kila siku katika maisha yetu. Hivyo katika makala ya leo tunaangalia Sheria ya Ardhi kwa ufupi. Karibu sana.

Msingi wa Uwepo wa Sheria ya Ardhi

Ardhi ni eneo la nchi ambalo watu wanaendesha shughuli zao za kila siku. Hakuna shughuli za kibinadamu zinazofanyika pasipo matumizi ya ardhi. Hii inafanya suala la ardhi kuwa la muhimu sana na linahitaji kutazamwa kwa sheria ili wanajamii waweze kuendesha shughuli zao kwa amani na maendeleo.

Matumizi ya ardhi ni moja ya sababu za migogoro mingi mahakamani, migogoro ya kijamii hata baina ya nchi na nchi. Kama wananchi tunashuhudia kila kukicha migogoro mikubwa ya ardhi maeneo tofauti tofauti. Uwepo wa sheria juu ya ardhi ni muhimu sana kwa ajili ya kuweka ustawi wa jamii katika nyanja zote.

Maana ya Ardhi

Kwa tafsiri ya kawaida ardhi ni eneo la juu/tabaka la juu la eneo fulani. Hata hivyo kwa mujibu wa sheria ardhi inabeba maana pana zaidi ya tabaka la juu la udongo.

Sheria ya ardhi inatoa tafsiri ya ardhi kuwa  ni pamoja na ardhi inayoonekana, vitu vilivyoota juu yake, nyumba, na majengo mengine ya kudumu pamoja na vitu vyote vilivyopo chini ya ardhi isipokuwa madini na mafuta.

Hivyo sheria ya ardhi ni kanuni, taratibu na miongozo inayohusu upatikanaji wa ardhi, matumizi na utawala juu ya ardhi.

Sheria kuu zinazotawala mambo ya Ardhi ni Sheria ya Ardhi Na.4 ya 1999 na Sheria ya Ardhi Vijijini Na.5 ya 1999.

Misingi ya Sheria ya Ardhi

Sheria ya Ardhi na Sheria ya Ardhi ya Vijijini imeweka misingi mikuu ya ardhi kwa mujibu wa sera ya Ardhi ya Tanzania 1995 ambayo;

 • Ardhi ni mali ya umma na imekabidhiwa kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kama mdhamini kwa naiba ya raia wote
 • Raia wote wana haki sawa ya kupata, kumiliki na kutumia ardhi
 • Milki za ardhi zilizopo ikiwa ni pamoja na za kimila zinatambuliwa na kulindwa na sheria
 • Ardhi inatumika kwa manufaa yanayozingatia maendeleo endelevu
 • Kuhakikisha kwamba fidia kamili na ya haki inalipwa kwa mmilikaji bila kuchelewa pale ardhi yake inapochukuliwa na Serikali chini ya sheria mpya za ardhi au chini ya sheria ya uchukuaji ardhi kwa manufaa ya umma
 • Kuwa na mfumo bora wa utawala wa ardhi ambao unawezesha wananchi wote kushiriki katika kufanya maamuzi yanayohusiana na masuala ya ardhi wanayoitumia.

Vyombo vya Utatuzi wa Migogoro ya Ardhi

Kama tulivyoeleza kwenye utangulizi, suala la ardhi linaongoza kwa kuwa na migogoro mingi katika jamii. Hivyo Bunge lilipitisha sheria maalum ya kuanzisha vyombo husika na ututuzi wa migogoro ya ardhi. Sheria hiyo inaitwa Sheria ya Utatuzi wa Migogoro ya Ardhi Na.2 ya 2002.

Vyombo hivyo vilivyoanishwa katika sheria hiyo ni;

 • Baraza la Ardhi la Kijiji
 • Baraza la Kata
 • Baraza la Ardhi na Nyumba la Wilaya
 • Mahakama Kuu (Kitengo cha Ardhi)
 • Mahakama ya Rufaa ya Tanzania

Hitimisho

Ardhi ni rasilimali muhimu sana katika ustawi na maendeleo ya jamii kwani shughuli zote za uzalishaji zinategemea matumizi ya ardhi. Hivyo ni muhimu sana kwa mwananchi kuwa na ufahamu wa masuala ya ardhi kwani ni msingi wa maisha yake ya kila siku.

Uliza sheria inajipanga kukuletea uchambuzi wa Sheria ya Ardhi ili kuifahamu kwa undani na namna tunavyoweza kuepuka kufanya makosa.

Kumbuka ‘kutokujua sheria si utetezi iwapo utatenda kosa lolote’ tafuta maarifa sahihi ya kisheria yakusaidie kufanya maamuzi sahihi kila siku. Wasiliana nami kupitia www.ulizasheria.co.tz

Wako

Isaack Zake, Wakili