3 B: Taasisi za Kazi

Utangulizi

Ndugu msomaji leo tunaendelea kufanya uchambuzi juu ya sheria za kazi. Kama hukupata kusoma makala iliyopita fuatilia somo Ijue Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini. Makala iliyotangulia tulianza kuangalia juu ya Taasisi za Kazi kama hukusoma fuatilia kwenye maneno haya Taasisi za Kazi,  ambapo tulianza kuangalia juu ya Baraza la Kazi, Uchumi na Jamii, Tume ya Usuluhishi na Uamuzi na Kamati ya Huduma Muhimu. Leo tunakwenda kuchambua Taasisi za kazi sehemu ya pili. Karibu sana.

4. Bodi za Mishahara (Bodi)

Bodi ya mishahara zinaweza kuteuliwa kwa kuzingatia sekta au eneo. Bodi za mishahara zinateuliwa na Waziri wa mwenye dhamana ya utumishi wa umma kwa ajili ya sekta ya umma na Waziri wa kazi kwa sekta binafsi. Bodi za ujira zinaundwa na Mwenyekiti akisadiwa na wajumbe 2 kwa kuzingatia uwakilishi wa waajiri, wafanyakazi.

Kazi za Bodi;

  • Kufanya uchunguzi kuhusu kima cha chini cha mshahara na masharti ya ajira kisekta
  • Kusaidia kuanzisha na kukuza majadiliano ya pamoja baina ya vyama vya wafanyakazi na waajiri
  • Kutoa mapendekezo kwa Waziri kuhusu kima cha chini cha mshahara na masharti ya ajira kisekta.

Hapa lazima kuelewa kuwa soko la ajira limegawanywa katika sekta mbali mbali mfano sekta ya umma, usafirishaji, kilimo, ujenzi na madini. Masharti ya viwango vya ajira yanatofautiana kisekta pia na hata kima cha chini cha mishahara inatofautiana kisekta. Hivyo ni muhimu kwa wadau wa sheria za kazi kufahamu sekta waliyopo na ni nini viwango vya kuzingatia katika sekta husika.

Mamlaka ya Bodi

  • Kumhoji mtu ambaye anaweza kutoa taarifa kuhusiana na uchunguzi inayofanya
  • Kumtaka mtu yeyote kwa maandishi kutoa taarifa, nyaraka, kitabu au kitu chochote kitakachosaidia uchunguzi
  • Kuwezesha majadiliano ya pamoja kuhusu kima cha chini cha mshahara baina ya vyama vya wafanyakazi na jumuiya za waajiri.

Waziri ana mamlaka ya kutoa tamko au agizo la ujira katika sekta au eneo husika ambalo litawabana waajiri na wafanyakazi na kuwa sehemu ya viwango vya ajira. Masharti ya amri ya ulipaji mishahara yataendelea kutumika mpaka pale yatapobadilishwa au kufutwa na waziri au yamefanyiwa marekebisho au yamesimamiwa kwa makubaliano ya pamoja kati ya wafanyakazi na waajiri.

 5. Usimamizi wa Kazi na Ukaguzi (Idara ya Kazi)

Idara ya kazi inaongozwa na Kamishna wa Kazi akiwa na jukumu la kusimamia utekelezaji wa Sheria ya Ajira. Katika idara hii imegawanywa sehemu ya Uhusiano Kazini, Ukaguzi wa Kazi na Hifadhi ya Jamii ambazo zitaongozwa na Makamishna wasaidizi. Pia idara ya kazi itahusisha maafisa wa kazi ambao ni watendaji katika kusimamia utekelezaji wa sheria za kazi.

Mamlaka ya Idara ya Kazi

Maafisa wa kazi wanayo mamlaka ya kuingia eneo la mwajiri kufanya ukaguzi, upekuzi, kukamata nyaraka, kuchukua sampuli, vipimo, kupiga picha, kumhoji mtu yeyote, kufungua mashitaka Mahakamani dhidi ya mtu anayekiuka Sheria za Kazi na kuendesha mashtaka kwa jina la kamishna.

Pia afisa wa kazi anaweza kutoa amri ya kumtaka mwajiri azingatie Sheria za Kazi endapo atabaini mwajiri anakiuka Sheria za Kazi.

 6. Mahakama ya Kazi

Mahakama ya Kazi ni Divisheni ya Mahakama Kuu ya Tanzania. Mahakama kuu Divisheni ya Kazi itaundwa na Jaji atakayekaa na walau washauri wawili wa baraza ambao ni wawakilishi wa mwajiri na mfanyakazi. Kazi za mahakama kuu ya kazi ni kutafsiri sheria, kusikiliza migogoro na kupitia marejeo ya uamuzi wowote toka vyombo vingine vya Taasisi za kazi. Mahakama ya kazi inafanya taratibu zake kama mahakama kuu nyingine za Tanzania. Hata hivyo uwalikishi katika mahakama hii ni mpana zaidi unaweza kuwakilishwa na ofisa wa chama cha wafanyakazi, au jumuiya ya waajiri au wakili au mtu yeyote wa chaguo lako.

Endapo mtu hajaridhika na maamuzi ya mahakama ya kazi anaweza kukata rufaa kwenda Mahakama ya Rufaa ya Tanzania.

Hitimisho

Ndugu msomaji leo tumeangalia Taasisi za Kazi ambazo ni vyombo vinavyohusika na utekelezaji wa Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini. Taasisi hizi zimeundwa kisheria kupitia Sheria ya Taasisi za Kazi ya mwaka 2004.

  • Tumejadili kwa ufupi aina za Taasisi ambazo ni Baraza la kazi, uchumi na jamii, Tume ya Usuluhishi na Uamuzi, Kamati ya Huduma Muhimu, Bodi ya Mishahara, Usimamizi wa Kazi na Ukaguzi na Mahakama ya Kazi.
  • Tumeainisha muundo wa Taasisi hizi, kazi zake na mamlaka yake.

Usikose kufuatilia tena uchambuzi juu ya sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini.

Usisite kunitumia maswali yako yoyote kuhusu sheria katika mtandao wako  kumbuka ‘kutokujua sheria si utetezi iwapo utatenda kosa lolote’ tafuta maarifa sahihi ya kisheria yakusaidie kufanya maamuzi sahihi. Wasiliana nami kupitia www.ulizasheria.co.tz

wako

Isaack Zake, Wakili

2 replies
  1. Ramadhan kilima
    Ramadhan kilima says:

    Ahsante kaka, hivi kama mwajiri anasema utaingia kazini saa 2 asubuhi na kutoka saa 12 jioni je sheria inasemaje kuhusu hili?

    • ulizasheria
      ulizasheria says:

      Sheria haiwapangii wafanyakazi muda wa kuingia na kutoka bali suala la muda ni kutokana na aina ya kazi na maelewano ya pande zote mbili. Muhimu kufahamu kuwa mfanyakazi kwa siku anapaswa kufanya kazi si zaidi ya saa 9 za kawaida na saa 3 za ziada.

      Karibu

Comments are closed.