Ijue Sheria ya Mkataba

Utangulizi

Karibu sana ndugu msomaji wa makala  ambapo umekuwa ukipata maarifa juu ya sheria mbali mbali na dhana kadhaa za kisheria kila siku. Hivi karibuni tumekuwa na mfululizo wa makala za makundi ya sheria. Baada ya kujadili Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Tumeanza mfululizo wa makala 10 za utabulisho wa baadhi ya sheria ambazo zina matumizi ya kila siku kwa mwananchi. Kundi la kwanza la sheria ni zile zinazoangukia kwenye Madai na kundi la pili tutaangalia sheria zinazoangukia kwenye Jinai. Makala iliyopita tulianza kuangalia juu ya Sheria ya Ardhi, soma Ijue Sheria ya Ardhi ambayo inaangukua kwenye Madai. Leo tunakuletea utambulisho wa Sheria za Mikataba. Karibu tujifunze.

 Msingi wa Uwepo wa Sheria ya Mikataba

Katika msingi wa mahusiano ya wanajamii vipo vitu vingi vinatuunganisha na kutufanya kufanya kazi pamoja kwa lengo la kuleta maendeleo. Hali hii inayofanya mwanadamu lazima aishi na kuhusiana na wanadamu wengine inaleta dhana na uwepo wa makubaliano mbali mbali kila siku. Kila siku mtu utakuwa kwenye makubaliano fulani na mtu mwengine. Makubaliano hayo yanaweza kuwa ya kazi au nauli unalipa kupata usafiri, au unanunua bidhaa n.k.

Makubaliano haya ndio msingi wa neno mkataba. Mkataba si lazima uwe kwenye maandishi unaweza kuonekana kwa maneno au namna ya vitendo baina ya wahusika.

Maana ya Mkataba

Kwa tafsiri ya kawida mtu anaweza kusema mkataba ni makubaliano baina ya pande mbili au zaidi. Hata hivyo Sheria inayoongoza masuala ya mikataba inaeleza kwamba

Mkataba ni makubaliano baina ya pande mbili au zaidi yanayofanyika kwa mdomo au maandishi yenye nguvu ya kisheria.

Maana hii ya kisheria inaleta taswira tofauti kabisa baina ya makubaliano ambayo tumezoea kuyafanya kila siku na makubaliano ambayo yapo kwa mujibu wa sheria.

Zipo sheria nyingi zinazoongoza mambo ya mikataba au makubaliano, hata hivyo sheria kuu ni ile Sheria ya Mikataba, Sura ya 345.

Misingi ya Sheria ya Mikataba

Si makubaliano yote ni mkataba. Ili makubaliano yawe mkataba kuna vigezo maalum ambavyo lazima pande husika wavizingatie kabla ya kuingia kwenye makubaliano hayo. Vigezo hivyo ni kama ifuatavyo;

  • Utashi huru: kwamba pande zinazoingia makubaliano lazima wayafanye kwa hiyari yao pasipo kushawishiwa au kulazimishwa au kudanganywa kwa namna yoyote ile.
  • Pande zinazohusika kuwa na uwezo wa kuingia makubaliano: hapa ili makubaliano yawe na nguvu ya kisheria lazima yawe yameingiwa na pande ambazo zina mamlaka na uwezo wa kisheria kuingia makubaliano. Mfano anayeingia makubaliano ya mkataba lazima awe amefikia umri wa kuanzia miaka 18 na mwenye akili timamu.
  • Mbadilishano wa thamani unaokubalika kisheria: yaani malipo yanayotokana na makubaliano lazima yawe halali kisheria, mfano malipo ya mkataba yanaweza kuwa fedha. Si halali kisheria kuwa watu walipane kitu ambacho hakitambuliwi kisheria. Mfano huwezi kuingia mkataba huku malipo yakawa kumpatia upande wa pili mtoto.
  • Jambo la makubaliano liwe linakubalika kisheria: jambo husika ambalo pande zinazoingia mkataba zinakubaliana lazima liwe linakubalika na sheria. Huwezi kuingia mkataba kwa kufanya jambo la kihalifu/kijinai huo ni mkataba haramu. Mfano huwezi kuingia mkataba wa kulipwa kwa kufanya mauwaji ya mtu maana kitendo cha kuua mtu ni jinai kimekatazwa na sheria. Hivyo mkataba kama huo ni batili.

Vyombo vya Utatuzi wa Migogoro ya Mikataba

Sheria za mikataba zipo nyingi sana hata hivyo iwapo kutajitokeza mgogoro juu ya mikataba vipo vyombo au hatua zinazoweza kuchukuliwa ili kutatua mgogoro huo;

  • Usuluhishi wa pande za mkataba; hapa pande husika wanajaribu kukaa na kutatua changamoto iliyojitokeza wenyewe
  • Usuluhishi kwa kuhusisha mtu mwengine; hapa pande husika zinakubaliana na kuteua mtu wa tatu ambaye hana upande ili kuwasaidia kutatua mgogoro.
  • Kufungua mashitaka kwenye mahakama za madai; endapo pande husika zimeshindwa kufikia makubaliano wanaweza kufungua madai kwenye mahakama zenye mamlaka.
  • Kupeleka mgogoro kwenye chombo maalum ambacho kilianishwa ndani ya mkataba kuwa endapo mgogoro utajitokeza kitakuwa na mamlaka ya kuamua.

Hitimisho

Sheria za mikataba ni moja kati ya sheria ambayo tunaiishi kila siku ingawa hatuitilii maanani. Ni vyema mwananchi akawa makini na makubaliano mbali mbali anayofanya ikiwezekana apate ushauri wa kisheria kabla ya kufanya makubaliano na ahakikishe anafanya makubaliano ya maandishi.

Uliza sheria inajipanga kukuletea uchambuzi wa Sheria ya Mikataba ili kuifahamu kwa undani na namna tunavyoweza kuepuka kufanya makosa yanayoweza kutuletea hasara kubwa.

Kumbuka ‘kutokujua sheria si utetezi iwapo utatenda kosa lolote’ tafuta maarifa sahihi ya kisheria yakusaidie kufanya maamuzi sahihi kila siku. Wasiliana nami kupitia www.ulizasheria.co.tz

Wako

Isaack Zake, Wakili

4 replies

Comments are closed.