Ijue Sheria ya Ndoa

Utangulizi

Karibu sana ndugu msomaji wa makala ambapo umekuwa ukipata maarifa juu ya sheria mbali mbali na dhana kadhaa za kisheria kila siku. Leo tunaendelea na mfululizo wa makala 10 za utabulisho wa baadhi ya sheria ambazo zina matumizi ya kila siku kwa mwananchi. Katika kundi la sheria za madai leo tunaangalia Sheria ya Ndoa. Karibu tujifunze.

 Msingi wa Uwepo wa Sheria ya Ndoa

Sheria ya ndoa ni zao au aina mojawapo ya sheria za mkataba. Jaamii yoyote ulimwenguni iliyostaarabika inazo taratibu na mila zinazowaunganisha wanajamii katika taasisi ya ndoa. Hata hivyo suala la ndoa linatambulika kitamaduni na kisheria pia. Hivyo Mamlaka zinazohusika na utungaji wa sheria iliona vyema kutunga sheria ambayo itatumika kuratibu, kuongoza masuala ya ndoa kutokana na umuhimu uliopo katika mahusiano ya ndoa kwenye jamii.

Maana ya Ndoa

Kwa tafsiri ya kawaida ndoa ina maana ya muunganiko baina ya mwanamume na mwanamke.

Tafsiri ya ndoa kwa mujibu wa sheria ina maana ya muungano wa hiyari kati ya mwanamume na mwanamke unaokusudiwa kudumu kwa muda wa maisha yao.

Sheria inayoongoza masuala ya ndoa katika nchi yetu ya Tanzania ni Sheria ya Ndoa ya 1971.

 Aina za Ndoa

Sheria ya ndoa inatambua aina mbili za ndoa yaani;

 • Ndoa ya mke mmoja: huu ni muungano ambao unaruhusu mwanamume kuoa mke mmoja tu. Mfano ndoa za Kikristo.
 • Ndoa ya wake wengi: huu ni muungano ambao unaruhusu mwanamume kuoa mke zaidi ya mmoja. Mfano ndoa za Kimila na Kiislam

NB: Sheria ya ndoa hairuhusu mwanamke kuolewa na zaidi ya mwanamume mmoja

Vigezo vinavyofanya Ndoa iwe halali

Vipo vigezo vinavyopaswa kuzingatiwa ili ndoa iwe halali;

 • Muungano lazima uwe wa hiyari: kama tulivyoeleza kuwa ndoa ni aina ya mkataba hivyo ni muhimu pande zote ziwe zimeridhia pasipo kulazimishwa.
 • Muungano ni kati ya mwanamume na mwanamke: ndoa ni baina ya watu wenye jinsia mbili tofauti. Sheria ya ndoa haitambui mahusiano ya jinsia moja ni kunyume cha sheria.
 • Muungano huo unakusudi la kudumu: ndoa inakuduwa iwepo siku zote mpaka mmoja wa mwanandoa atakapofariki. Sheria haitambui ndoa za kipindi maalum. Hata hivyo yakijitokeza matatizo ambayo yanakubalika kisheria ndoa inaweza kuvunjwa na talaka kutolewa.
 • Wanandoa wasiwe maharimu: ndoa haipaswi kuwa kwa ndugu wa damu au wa karibu. Sheria inakataza mtu kufunga ndoa na mzazi wake,mtoto wake, au mjukuu wake au dada, mama au shangazi au mjomba, baba au mama wa kambo n.k.
 • Wanandoa wawe na umri unaokubalika kisheria: kama tulivyoainisha kwenye sheria ya mkataba umri unaotambuliwa ni kuanzia miaka 18. Hata hivyo Sheria ya Ndoa imetoa mazingira ambayo mtu chini ya umri huo anaweza kuingia kwenye ndoa. Zipo juhudi za kisheria zimefanywa ili kipengele hiki kifanyiwe marekebisho kwani umri chini ya miaka 18 ni umri wa mtoto kulingana na Sheria ya Mtoto ya 2009.

 

Aina za Ufungaji wa Ndoa

Sheria ya Ndoa inatambua aina kuu 3 za ufungaji wa ndoa ambazo mojawapo ikitumika ndoa hiyo inahesabika kuwa halali;

 • Ndoa ya Kimila

Ndoa inafungwa kimila iwapo mmoja wa wanandoa au wote wanafuata sheria na miiko ya mila za kabila fulani. Sheria inamtaja mdhamini wa ndoa iliyofungwa kimila kuwa Katibu Tarafa, na kwamba ndoa ya kimila lazima ifungwe na mtu anayetambulika katika eneo hilo au kabila hilo ana uwezo au mamlaka hayo. Kazi ya Katibu Tarafa kama mdhamini ni kuhakikisha wanandoa hao wanapata vyeti kutoka kwa Msajili wa Ndoa.

 • Ndoa ya Kidini

Hii ni aina ya ndoa inayofungwa kulingana na taratibu za kidini. Ndoa hii inafuata taratibu zote za kuwa na matangazo ya kisheria ya siku 21 kabla ya ndoa na inafungwa na kiongozi wa dini mwenye leseni ya kufungisha ndoa. Ndoa hii inaweza kufungwa kwenye nyumba ya ibada ambayo wanandoa wanaabudu au mahali pa wazi.

 

 • Ndoa ya Kiserikali

Ndoa hii hufungwa mbele ya Mkuu wa Wilaya ambaye ni Msajili wa ndoa wa wilaya. Mara nyingi wanaita ndoa ya ‘bomani’. Ndoa hii inafungwa ofisini kwa Mkuu wa wilaya au mahali pengine popote patakapochaguliwa na wanandoa.

Muhimu:

 • Ndoa zote hizi lazima zifungishwe na watu wenye mamlaka ya kufunga hizo ndoa.
 • Ndoa zote hizi lazima kiwepo cheti cha ndoa kinachotolewa na Msajili wa ndoa.
 • Ndoa zote lazima zifuate taratibu za kisheria kama zilivyoanishwa kwa vigezo vinavyofanya ndoa iwe halali.

Hitimisho

Sheria ya ndoa ina masuala mengi sana ambayo yanapaswa kujadiliwa. Mathalani nyakati hizi kumekuwa na mashauri mengi sana mahakamani ya kuvunja ndoa, familia zinaparaganyika kila siku kutokana na taasisi hii kutokuwa vizuri. Moja ya sababu inawezekana kuwa uelewa mdogo wa sheria hii ya ndoa kwa wanandoa wenyewe na jamii inayowazunguka.

Ndoa ni taasisi muhimu sana kwa jamii kwani sisi sote tunategemea ustawi wa ndoa ndivyo maisha yetu yanaweza kustawi katika Nyanja zote. Tunategemea watoto, vijana, wasomi, wataalam na wavumbuzi wa mambo mbali mbali watoke kwenye ndoa. Kama ndoa za jamii yetu hazipo vizuri hali ya jamii yetu ya baadae ipo mashakani.

Hivyo ni rai yetu ndugu msomaji uendelee kufuatilia makala za uliza sheria hata tutakapopata wasaa wa kuichambua sheria hii kwa undani zaidi. Hata hivyo usisite kutuma maswali yako kwa eneo lolote katika Sheria ya Ndoa nasi tutakujibu.

Kumbuka ‘kutokujua sheria si utetezi iwapo utatenda kosa lolote’ tafuta maarifa sahihi ya kisheria yakusaidie kufanya maamuzi sahihi kila siku. Wasiliana nami kupitia www.ulizasheria.co.tz

Wako

Isaack Zake, Wakili

2 replies
 1. Martin Tindwa
  Martin Tindwa says:

  Nauliza kuhusu ambacho kinazungumzwa mtaani ukikaa na mwanamke zaidi ya miezi sita ni mkeo ni sheria ya IPI inagusa hili

  • ulizasheria
   ulizasheria says:

   Nashukuru kwa swali zuri ndugu Martin Tindwa

   Kile kinachosemwa mtaani ni dhana ya kisheria ambayo inazungumzia uwepo wa ndoa baina ya mwanamume na mwanamke endapo watu hawa hawakufuata taratibu za kisheria kufunga ndoa bali wanaishi pamoja. dhana hii ili iweze kukubalika kisheria kuna vigezo lazima vithibitike.
   a. Lazima idhibitike mwanamume na mwanamke wameishi kwa pamoja mfululizo kwa kipindi cha miaka 2 au zaidi
   b. Lazima idhibitike kuwa umma unaowazunguka wanawachukulia na kuwapa heshima kama mke na mume
   c. Lazima idhibitike kuwa wana umri wa kisheria wa kuweza kuwa na ndoa
   d. Lazima ithibitike kuwa kati yao hakuna aliye na ndoa inayoendelea.

   Dhana hii inatambuliwa katika Sheria ya Ndoa ya 1971, Kifungu cha 160.

   Karibu sana

Comments are closed.