Ijue Sheria ya Mirathi

 Utangulizi

Karibu sana ndugu msomaji wa makala za Sheria Leo ambapo umekuwa ukipata maarifa juu ya sheria mbali mbali na dhana kadhaa za kisheria kila siku. Leo tunaendelea na mfululizo wa makala 10 za utabulisho wa baadhi ya sheria ambazo zina matumizi ya kila siku kwa mwananchi. Katika kundi la sheria za madai leo tunaangalia Sheria za Mirathi/Urithi. Karibu tujifunze.

Msingi wa Uwepo wa Sheria ya Mirathi

Dhana ya Urithi ni moja ya dhana kongwe kabisa tangu dunia kuwepo. Dhana hii imekuweo, ipo na itaendelea kuwepo katika maisha yetu ya kila siku vizazi na vizazi. Kwa kuwa sisi sote tunazaliwa tunawakuta waliotutangulia na sisi pia tutaondoka duniani basi urithi ni njia moja wapo ya kisheria inayotumika kuhakikisha warithi halali wanapata haki zao.

Wanadamu kwa kawaida tunazaliwa pasipo na kitu, tunapita katika maisha haya tunapata mali, fedha, nyumba na maslahi mengine mbali mbali. Hata hivyo changamoto ambayo tunayo watu wote ni kuwa hakuna atakayeondoka na vitu vyake alivyopata duniani. Hivyo urithi ndio njia pekee iliyoandaliwa kutusaidia walau kuacha vitu na mali kwa watu wanaostahili.

Maana ya Mirathi                                    

Mirathi ni mali aliyoacha marehemu kwa ajili ya kurithishwa warithi wake halali.

Sheria imeweka taratibu maalum zinazoongoza  ukusanyaji, uangalizi  usimamizi na ugawaji wa mali zilizoachwa na marehemu kwa warithi halali. Dhana ya mirathi pia inajumuisha ulipaji wa madeni yaliyoachwa na marehemu pamoja na mazishi.

Lengo la sheria za mirathi

  • Kutoa utaratibu wa kusimamia mali za marehemu baada ya kifo ikiwapo kuhamisha umiliki kwenda kwa warithi halali
  • Kuhakikisha madeni anayodai yanalipwa na wale wanaomdai wanapata haki yao.

Sheria zinazohusu mirathi Tanzania

  • Sheria za kimila

 Hii hutumika pale ambapo marehemu aliishi kwa kufuata mila na desturi za kabila lake. Sheria ya kimila itatumika pale tu wahusika wa mirathi hiyo wanatoka katika kabila moja na si vinginevyo.

Kanuni za Urithi (Tangazo la serikali Na.436/1963).

 

  • Sheria za Serikali

 Sheria hii itatumika pale endapo itabainika kuwa marehemu alikuwa hafuati sheria za Kiislamu wala taratibu za kimila. Sheria hii inaitwa Sheria ya Urithi ya India ya 1865 (inatumika na watu wanaofuata dini ya Kikristo).

  • Kama marehemu ameacha mjane na watoto mgao utakuwa 1/3 kwa 2/3
  • Kama marehemu hakuacha watoto mjane atapata ½ na ½ nyingine hugawanywa sawa kati ya wazazi, kaka na dada za marehemu.

 

  • Sheria za dini ya kiislamu

 Sheria hizi zinabainishwa katika Quran Tukufu na zinafuatwa na waumini wa dini ya Kiislam. Mgawanyo wake ni kama ifuaatavyo;

  • Warithi wakuu katika sheria hii ni mke au wake, baba,mama na watoto
  • Watoto wa kiume wanapata mara 2 ya watoto wa kike
  • Wajane/mjane wanapata 1/8 ya mali ya marehemu kama kaaacha watoto.
  • Mwosia haruhusiwi kutoa wosia zaidi ya 1/3 ya mali yake.

Aina za Mirathi

  • Mirathi palipo na wosia: hutokea wakati marehemu kabla ya kufariki aliacha maandishi/matamshi au maelezoya namna mali yake itakavyoshughulikiwa/itakavyomilikiwa baada ya kifo chake.

 

  • Mirathi pasipo na wosia: hapa marehemu hakuacha wosia yaani tamko au maandishi hivyo warithi hulazimika kuchagua msimamizi au wasimamizi kupitia mahakama.

 

Hitimisho

Ndugu msomaji sheria zinazohusu mirathi zimekuwa na changamoto kubwa sana katika nchi yetu kwani watu wengi wamekuwa wanapata mali lakini hawaandiki wosia. Kuna dhana kuwa ukiandika wosia ndio unajichulia kifo, dhani hii si ya kweli kabisa kwani haina udhibitisho wowote. Kwa madhila yanayowapata warithi katika jamii yetu itoshe kutuamsha sisi tulio hai sasa kuchukua hatua stahiki kuandika wosia ili warithi wetu wapate haki zao.

Wosia katika mirathi ndio njia pekee na sahihi kwa marehemu kupata nafasi ya kauli na maamuzi juu ya mali zake kusikilizwa na kuheshimiwa ingawa amekufa. Tusipoteze fursa hiyo ndugu zangu.

Uliza sheria itaandaa utaratibu wa uchambuzi wa sheria za mirathi Tanzania, usiache kutuma maswali yako kwenye mtandao wako nasi tutakujibu.

Kumbuka ‘kutokujua sheria si utetezi iwapo utatenda kosa lolote’ tafuta maarifa sahihi ya kisheria yakusaidie kufanya maamuzi sahihi kila siku. Wasiliana nami kupitia www.ulizasheria.co.tz

Wako

Isaack Zake, Wakili