4. Kinga na Ulinzi katika Kazi

Utangulizi

Ndugu msomaji wa makala za Uchambuzi wa Sheria , leo tunaendelea na uchambuzi wa Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini. Katika makala zilizopita tumeangalia juu ya Ijue Sheria ya Kazi na Taasisi za Kazi fuatilia makala hizo ili kupata msingi wa elimu hii.

Ndugu msomaji leo tunakwenda kuangalia Ulinzi katika Sheria ya Kazi. Ulinzi katika sheria ya kazi unalengo la kuainisha makundi maalum au wadau ambao kutokana na hali yao au umri wao wanaweza kunyanyasika katika mahusiano ya kazi. Hivyobasi sheria imetoa ulinzi kwa makundi haya.

Ulinzi huu wa sheria za kazi umeanishwa katika maeneo makuu matatu ambayo tutakwenda kuyaangalia katika makala hii.

  1. Ulinzi kwa watoto

Sheria ya Kazi imeanisha kuwa moja wapo la kundi ambalo linaathirika na unyanyasaji katika jamii hasa katika masuala ya ajira ni watoto. Wengi wamekuwa wakiwaingiza kwenye ajira watoto wadogo hasa kwa kazi za migodini, mashambani na kazi za majumbani kama wasaidizi. Sheria ya Kazi imeweka katazo kuwa ni marufuku kuajiri mtoto mwenye umri  chini ya maiaka 14.

Aidha mtoto mwenye umri wa miaka 14 anaweza kuajiriwa kufanya kazi nyepesi tu, ambazo haziwezi kuwa na madhara kwa afya na maendeleo ya mtoto katika masomo au mafunzo anayoudhuria.

Pia sheria imeweka katazo kuwa ni marufuku mtoto chini ya miaka 18 kuajiriwa kwenye machimbo, viwanda au kama baharia kwenye meli au mahali pa kazi pasipo rasmi au eneo lolole ambalo mazingira yake yanaweza kuchukuliwa ni hatari na Waziri wa Kazi.

Kimsingi sheria inakataza mtoto kuajiriwa katika ajira ambayo si sahihi kwa umri wake au inayohatarisha ustawi wake, kielimu, kiakili, au kiroho au maendeleo ya kimaadili au kijamii.

Hatahivyo sheria inatoa ruhusa mtoto chini ya umri wa miaka 14 kufanya kazi katika mazingira yaliyotajwa kama hatarishi ikiwa ni kwa lengo la mafunzo tu.

Ileweke ni kosa la jinai kumwajiri mtoto chini ya miaka 14 au chini ya miaka 18 katika maeneo yaliyoainishwa au kumrubuni mtoto ili kumwajiri. Mwajiri atakayepatikana na hatia ya kosa hilo anaweza kuadhibiwa kwa faini isiyozidi Tsh.1,000,000/- au kifungo cha mwaka mmoja au vyote kwa pamoja.

  1. Katazo la ajira za shuruti

Sheria ya Kazi imeweka katazo la kisheria la kumshurutisha mtu kufanya kazi. Kazi za shuruti ni aina ya kazi anayolazimishwa mtu kuifanya pasipo ridhaa yake. Kazi za shuruti zinajumuisha pia kazi ambazo mtu hulazimika kufanya kulipa deni, kufanya akiwa amefungiwa au anazolazimika kuzifanya baada ya kupewa vitisho mbalimbali ikiwa ni pamoja na kitisho cha kuadhibiwa.

Hatahivyo sheria inaaninisha kuwa yapo mazingira yatakayolazimisha mtu kufanya kazi na haitahesabiwa kama ni kazi ya shuruti. Mazingira hayo ni kama ifuatavyo;

  • Kazi za kijeshi kwa mujibu wa sheria ya ulinzi wa taifa
  • Kazi ambayo ni sehemu ya wajibu wa kawaida wa raia wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
  • Kazi katika kutekeleza amri ya mahakama chini ya usimamizi wa mamlaka ya Umma
  • Kazi wakati wa hali ya dharula au majanga hatarishi kwa maisha na ustawi wa jamii
  • Kazi za jamii ambazo jamii husika wamekubaliana kwa pamoja kuzifanya.

 

  1. Katazo la ubaguzi

Sheria ya Kazi inabainisha katazo la ubaguzi kwa waajiri dhidi ya wafanyakazi kwa namna yoyote ile. Waajiri wanakatazwa kuwabagua wafanyakazi wao kwa namna yoyote ile iwe katika sera au utendaji  kwa misingi ya rangi, utaifa, kabila au mahali anapotoka mfanyakazi, mbari/ukoo, asili ya jamii, mwelekeo wa kisiasa au kidini, jinsia, ujauzito, ulemavu, hali ya ndoa, VVU/UKIMWI,umri au hali ya maisha. Pia unyanyasaji kwa mfanyakazi itahesabika ni aina ya ubaguzi.

Hatahivyo haitahesabika kuwa ni ubaguzi endapo mwajiri atafanya yafuatayo;-

  • Kuchukua hatua ambazo zinaendana na ukuzaji wa usawa na utokomezaji wa ubaguzi katika sehemu ya kazi
  • Kutofautisha, kutenga au kumpendelea mtu yeyote kwa masharti ya kazi yaliyowekwa
  • Kuajiri raia kwa mujibu wa sheria.

Katazo la ubaguzi pia linahusisha marufuku kwa vyama vya wafanyakazi au jumuiya za waajiri kufanya ubaguzi;

  • Katika kuwapokea, au kuwawakilisha au kuwaachisha uanachama
  • Katika sera yoyote ya ajira au mazoea ya ajira
  • Katika makubaliano yoyote ya pamoja

Sheria ya Kazi inawataka waajiri kutengeneza mpango maalum unaonesha namna wanavyotoa fursa sawa na kuondoa ubaguzi mahali pa kazi na kuusajili mpango huo kwa kamishna wa kazi.

Hitimisho

Ndugu msomaji kama nilivyotangulia kueleza leo tunajifunza juu ya kinga na ulinzi kama zilivyoainishwa katika sheria ya Kazi. Tumeweza kuona kuwa sheria inaweka makatazo kadhaa ikiwepo ajira kwa watoto, katazo kwa kazi za shuruti na katazo kwa ubaguzi kazini.

Hii itatusaidia sisi sote wadau wa ajira yaani wafanyakazi na waajiri kuzingatia sheria ya kazi kuepuka makosa yanayojitokeza kila siku.

Usisite kunitumia maswali yako yoyote kuhusu sheria katika mtandao wako kumbuka kutokujua sheria sio utetezi katika kutenda makosa chukua hatua sasa uliza nasi tutakupatia majibu sahihi kwenye changamoto yako yoyote ya kisheria.

2 replies
    • ulizasheria
      ulizasheria says:

      Asante kwa swali lako zuri. Sheria haimkatazi mtu kuwa na kazi zaidi ya moja. suala la kazi mbili au zaidi inatokana na makubaliano yako na waajiri wako. cha muhimu mahali pale unapofanya kazi unatekeleza kwa wakati wajibu wako na majukumu yako na kwa namna yoyote kaziyako nyingine haiingilii masharti ya kazi nyingine. Msingi ni kujipanga na muda ulionao namna ya kuutumia kutimiza wajibu katika kazi zako. Hata hivyo hii ni changamoto kubwa kwa watu walioajiriwa full time (yaani unakuta anahitajika kazini kila siku kwa zaidi ya masaa 8) na kufanya masaa 45 kwa wiki. hiki ndio kiwango cha chini cha muda wa kufanya kazi kwa mwajiri mmoja.

      Uwezekano wa kuwa na kazi zaidi ya moja ni pale mtu unapofanya kazi kama mkandarasi huru (Independent contractor) na sio kama Mfanyakazi (mwajiriwa). Nitafafanua dhana hii katika uchambuzi wa Sheria ya kazi.

      Karibu sana

Comments are closed.