2.Ijue Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini

Utangulizi

Karibu sana ndugu msomaji wa ukurasa wa Elimu ya Sheria kwenye kipengele cha Uchambuzi wa Sheria. Kwenye makala ya utangulizi  tulizungumzia juu ya Umuhimu wa Sheria ya Ajira. Leo nakuletea makala nyingine ya kukupa ufahamu juu ya Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini ambayo tutakwenda kuijadili katika mfululizo wa makala hizi. Karibu sana.

Mahusiano ya mfanyakazi na mwajiri yanaongozwa na sheria ya Ajira na Uhusiano Kazini ya mwaka 2004 iliyoanza kutumika mnano tarehe 05/01/2007. Sheria hii imekuja kama jibu kwa changamoto mbali mbali zilizokuwa zinaikumba sekta ya ajira kwa wingi wa sheria zenye kuhusika na masuala ya kazi zilizotangulia. Hata hivyo mabadiliko ya sheria hii yalichagizwa na mambo kadhaa ikiwemo;

  • Mabadiliko ya mfumo wa uchumi kutoka uchumi dola kwenda uchumi wa soko huria
  • Utandawazi
  • Mabadiliko ya kisiasa yaani uwepo wa vyama vingi
  • Haja ya uwepo wa vyama huru vya wafanyakazi
  • Kukidhi matakwa ya mapatano ya Shirika la Wafanyakazi Duniani (ILO)
  • Mapungufu ya sheria za kazi zilizokuwepo.

Sheria ya Ajira na Uhusiano Kazini inahusisha wafanyakazi wote wa umma na katika sekta binafsi wanaofanya kazi Tanzania Bara. Hatahivyo sheria hii imeondoa baadhi ya makundi ya wafanyakazi ambao kwa asili ya kazi zao, wamewekewa utaratibu/sheria kulingana na kazi husika. Makundi hayo ni;

  • Jeshi la wananchi wa Tanzania
  • Polisi
  • Magereza
  • Jeshi la Kujenga Taifa.

Madhumuni ya sheria

Sheria hii ilitungwa kwa madhumuni yafuatayo;

  • Kukuza maendeleo ya uchumi kupitia ufanisi katika uchumi, uzalishaji na haki ya kijamii.
  • Kuweka mfumo wa kisheria kwa ajili ya mahusiano mazuri na haki sawa katika ajira na viwango vya chini kuhusiana na masharti ya kazi
  • Kuweka mfumo wa majadiliano ya pamoja kwa hiari ya vyama vya wafanyakazi na waajiri au jumuiya za waajiri
  • Kudhibiti matumizi ya migomo na kufungia nje kama njia ya utatuzi wa migogoro
  • Kuingiza haki za kikatiba zinazohusiana na masuala ya kazi katika sheria
  • Kutekeleza mikataba ya msingi ya ILO na mingine iliyoridhiwa katika sheria.

Dondoo za makala ya leo;

  • Sheria ya Ajira na Mahusiano kazini litungwa 2004 ili kujibu changamoto za wakati huu ikiwepo mabadiliko ya mfumo wa uchumi na utandawazi
  • Sheria hii inawahusu wafanyakazi na waajiri wote katika sekta binafsi na umma Tanzania Bara isipokuwa vyombo vya ulinzi na usalama.
  • Sheria ilitungwa kwa madhumuni ya kuweka mazingira mazuri ya ukuaji wa uchumi na maendeleo kwa kuzingatia haki za pande zote yaani mfanyakazi na mwajiri.

Ndugu msomaji swali la kujiuliza ni iwapo wewe ni mfanyakazi au mwajiri au unatarajia kuwa mfanyakazi au kuwa mwajiri? Uchambuzi wa sheria hii unakuhusu sana wewe ili kuepuka makosa ambayo yanafanywa na wafanyakazi wengi na waajiri wengi kwa kutokuijua sheria hii. Usiache kufuatana nami katika mfululizo wa makala hizi za uchambuzi wa sheria ya kazi.

Usisite kunitumia maswali yako yoyote kuhusu sheria katika mtandao wako  kumbuka ‘kutokujua sheria si utetezi iwapo utatenda kosa lolote’ tafuta maarifa sahihi ya kisheria yakusaidie kufanya maamuzi sahihi. Wasiliana nami kupitia www.ulizasheria.co.tz

wako

Isaack Zake, Wakili

5 replies
  1. John Tuu
    John Tuu says:

    Napenda kujua kuhusu marekebisho ya kifungu cha 42 cha sheria ya ajira na mahusiano ya kazi 2004.

    Nasikia mstaafu hatalipwa kiinua mgongo. Je, ni kweli? Nitapataje copy ya mabadiliko hayo katika website?

    • ulizasheria
      ulizasheria says:

      Habari yako ndugu John Tuu

      Nashukuru kwa swali lako zuri. Mpaka sasa sijaona mabadiliko ya Kifungu cha 42 cha Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini ya 2004. hivyo haki za mstaafu au mtu mwengine yeyote juu ya kiinua mgongo ziko pale pale. Karibu sana uliza sheria. Pia utuwie radhi kuchelewa kukujibu swali lako mapema.

      Asante sana.

Comments are closed.