Sheria Leo. Sheria Binafsi (Private Laws)
Utangulizi
Karibu sana kwa siku ya leo ndugu yangu msomaji na mfuatiliaji wa ukurasa wa Sheria Leo. Tunaendelea kukuletea maarifa ya kisheria kwa uchambuzi wa masuala kadhaa ya kisheria. Tumekuwa na mfululizo wa kuchambua makundi ya sheria ambayo tuliyaanisha kwenye makala zilizopita. Leo tunakuletea ufafanuzi juu ya uchambuzi wa Sheria Binafsi. Karibu tujifunze
Maana ya Sheria za Binafsi
Kwa kutazama neno Sheria Binafsi unaweza kusema ni sheria zinazotungwa na watu binafsi hata hivyo neno hili linamaanisha aina ya kundi la sheria zinazotungwa kwa lengo la kuratibu mahusiano baina watu kwenye jamii, pia zinahusu kuratibu mahusiano ya taasisi mbalimbali. Hizi ni sheria zinazotungwa ili kuongoza matendo ya wanajamii baina yao.
Sheria hizi zinaratibu haki na wajibu wa wananchi. Sheria hizi zintungwa na Bunge kama zilivyo sheria nyingine lakini hizi ni kwa madhumuni ya kuongoza matendo ya wanajamii miongoni mwao.
Serikali na taasisi zake pia zinaweza kuwa na mahusiano ya kibinafsi na watu au wanajamii mfano uwepo wa mikataba ambayo Serikali inaingia. Katika mazingira haya Serikali inakuwa katika wigo wa sheria binafsi.
Maeneo ya Sheria za Binafsi
Wigo wa sheria binafsi ni mpana sana lakini kwa uchache sheria hizi zinazungumzia maeneo kadhaa. Mfano:
- Sheria za Mikataba
- Sheria ya Madhara
- Sheria za Mirathi
- Sheria za Uwakala
- Sheria za Umiliki wa Mali
Mara zote Sheria binafsi zinahusisha angalau makundi haya ya sheria ambayo tutayafafanua katika makala zinazofuata.
Hitimisho
Kundi hili la sheria Binafsi ni muhimu sana kwa wananchi kuzifahamu kwani zitasaidi wao kujua namna ya kuwajibika kwamujibu wa sheria na namna ya kudai haki zao ikiwa zimevunjwa au kukiukwa na wananchi wenzao au taasisi za kibinafsi au taasisi za umma.
Kumbuka ‘kutokujua sheria si utetezi iwapo utatenda kosa lolote’ tafuta maarifa sahihi ya kisheria yakusaidie kufanya maamuzi sahihi kila siku. Wasiliana nami kwa kutembelea mtandao wako wa www.ulizasheria.co.tz
Wako,
Isaack Zake, Wakili