1. Umuhimu wa Sheria ya Ajira

Utangulizi

Ndugu yangu msomani wa ukurasa wa Elimu ya Sheria, kipengele cha Uchambuzi wa Sheria nakukaribisha sana kwenye safari hii ya kujifunza.

Kwa kuanza mfululizo wa makala za Uchambuzi wa Sheria napenda kukuletea makala za kukuelimisha juu ya sheria za Kazi. Katika mfululizo huu tutaichambua Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini ya 2004.

Katika mfumo wa maisha ambao kwa sasa tunao, msingi wa maendeleo ya nchi na wananchi wake ni kufanya kazi. Kazi ni utu, kazi ni msingi wa maendeleo na kutatua changamoto ambazo zinakumba wananchi na taifa kwa ujumla.

Sekta binafsi imehodhi kwa kiasi kikubwa suala la ajira kuliko serikali kama ilivyokuwa wakati wa kipindi cha ujamaa. Hali ya uchumi sasa ni huria hivyo waajiri wana uhuru wa kuchagua wafanyakazi kulingana na matakwa yao.

Watu wengi wapo katika soko la ajira na kila uchao wanaongezeka wenye utaalam mbalimbali na wasio na utaalam wote hawa wanatafuta ajira. Hali hii inapelekea mazingira ya ajira kuwa magumu sana hasa kwa upande wa wafanyakazi ambao mara nyingi wamejikuta wakiwa katika kazi na makubaliano ambayo hawaridhiki nayo na endapo inatokea ajira ile inakwisha inakuwa kilio kwa wafanyakazi/mfanyakazi.

Katika makala hizi tutakwenda kuchambua kwa lugha nyepesi Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini ambapo tunakwenda kupata elimu ya namna mfanyakazi anatakiwa kujipanga anapoingia katika soko la ajira.

Makala hizi pia zitakuwa msaada kwa mwajiri kuweza kujua haki na wajibu wake na mipaka ya mamlaka yake kama inavyoainishwa katika sheria za kazi.

Ndugu msomaji fuatana nami katika mfululizo wa makala hizi ili kwa pamoja tuweze kuboresha mazingira ya mahali pa kazi.

Usisite kunitumia maswali yako yoyote kuhusu sheria katika mtandao wako  kumbuka ‘kutokujua sheria si utetezi iwapo utatenda kosa lolote’ tafuta maarifa sahihi ya kisheria yakusaidie kufanya maamuzi sahihi. Wasiliana nami kupitia www.ulizasheria.co.tz

wako

Isaack Zake, Wakili

4 replies
  1. Hamisi Juma
    Hamisi Juma says:

    Asante mtaalam wa sheria KWA kutupa elimu hii muhimu ya sheria,maana sheria ndio mwongozo wa maisha yetu hapa duniani.swali langu kwako je inawezekana KWA mfanyakazi alieumia kazini wakati akitekeleza wajibuwake akataka kuacha Kazi huku akiwa bado hajalipwa KWA kuumia kwake?Na kama inawezekana anaweza kutumia njia zipi ili asiwe nje ya sheria?
    Asante

    • ulizasheria
      ulizasheria says:

      Karibu sana ndugu
      Katika mazingira ya kuumia Kazini Sheria ya ajira imeweka utaratibu ambao Mwajiri anapaswa kuufuata ili kumwachisha kazi mfanyakazi. Ushauri wangu kwa mfanyakazi aliyeumia kazini kusubiri utaratibu wa kisheria ufuatwe ili kuweza kupata stahiki zake.
      Hata hivyo Sheria ya Fidia kwa Wafanyakazi kupitia Mfuko wa Fidia umeweka utaratibu wa kila Mwajiri kuchangia kiasi cha 1% ya mshahara wa mfanyakazi na Serikali/Taasisi za Umma kuchangia kiasi cha 0.5 cha mshahara wa mfanyakazi.
      Mfanyakazi aliyeumia kazini anapaswa kufuata taratibu zinazoelezwa na Sheria ya Fidia kwa Wafanyakazi na Kanuni zake ili utaratibu wa fidia uweze kuchukuliwa.
      Kutokana na swali lako ni vyema ukawasiliana nami kwa njia ya simu ili kukushauri kutokana na changamoto iliyokukuta au iliyomkuta mtu unayemfahamu
      karibu sana

  2. Tumain J.Anthony
    Tumain J.Anthony says:

    Asante mtaalam;kwa kutupatia elimu ya sheria ya ajira.swali; nimekuwa kwenye ajira kwa muda miaka kadhaa sasa bila ya kuwa na mkataba na hakuna stahiki zozote za kiajira zinazofuatwa lakini katika uchumbuzi wa mazingira yote ya mahusiano ya kiajira yapo,nifanyeje ili kupata stahiki zangu kwa mujibu wa sheria hii?

    • ulizasheria
      ulizasheria says:

      Asante Tumaini

      Swali lako ni zuri, hatua za kufanya kwanza ni kutambua haki zako za kiajira, mfano inapaswa uwe na mkataba wa maandishi kuanisha majukumu yako na aina ya ajira uliyopo kama ni kudumu au ya muda maalum au kazi maalum. Kama ni mkataba wa kudumu unastahili likizo ya siku 28 ya malipo kwa kila mwaka, kama unafanya masaa ya ziada ulipwe, makato yanayopaswa kuwekwa kwenye mfuko wa kijamii (mfano NSSF au PSPF, PPF etc). Ukizitambua haki hizi unaweza kuwasiliana na Ofisi ya Kazi (Labour Office) ambayo ipo karibu yako ili kuwasilisha malalamiko yako juu ya kutopewa haki yako wao watachukua hatua ya kumwita mwajiri na kumkagua kama anatekeleza sheria ya kazi ipasavyo.

      Ipo changamoto kubwa kwa wafanyakazi mara wanapoanza kufuatilia haki zao kwa waajiri wanatishiwa kufukuzwa au kusingiziwa makosa mbali mbali, hata hivyo ni bora kuwa na ujasiri wa kudai na kusimamia haki zako kuliko kuwa mtumwa siku zote. Wasiliana nasi wakati utakapohitaji msaada zaidi.

      Karibu sana ndugu yangu.

Comments are closed.