Ijue Haki ya Kupiga Kura

Utangulizi

Karibu ndugu yangu msomaji na mfuatiliaji wa ukurasa huu. Tunaendelea kukuletea maarifa ya kisheria kwa uchambuzi wa masuala kadhaa ya kisheria. Juma lililopita katika ukurasa wa Sheria Leo tulizungumzia kuhusu Mihimili ya Dola kama ilivyoanishwa katika Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa TanzaniaSheria Leo.33: Je, unaijua Mihimili ya Dola?. Leo tunaendelea na ibara nyingine ya Katiba inayohusu Haki ya Kupiga kura. Karibu tujifunze.

Msingi wa Haki ya Kupiga Kura

Tanzania ni nchi inayoendesha shughuli zake za mamlaka kwa mfumo wa Demokrasia kama ilivyoainishwa katika utangulizi wa Katiba. Demokrasia ni mfumo wa siasa ambao viongozi wanapata mamlaka yao kupitia mfumo wa kuchaguliwa na wananchi kutoka ngazi za chini mpaka ngazi ya juu ya uongozi yaani Rais wa Jamhuri ya Muungano.

Katika nchi ambayo inaongozwa kidemokrasia, haki ya kupiga na kupigiwa kura ni haki za msingi sana ambazo zinawahusu raia wa nchi husika.

Haki ya Kupiga Kura

 Katiba ya JMT , haki ya kupiga kura imeanishwa na Ibara ya 5 (1) ambayo inaeleza ifuatavyo;

‘Kila raia wa Tanzania aliyetimiza umri wa miaka kumi na minane anayo haki ya kupiga kura katika uchaguzi unaofanywa Tanzania na wananchi. Na haki hii itatumiwa kwa kufuata masharti ya ibara ndogo ya (2) pamoja na masharti mengineyo ya Katiba hii na Sheria inayotumika nchini Tanzania kuhusu mambo ya uchaguzi’

Ibara ya 5 (2) ya Katiba ya JMT inaendelea kufafanua masharti ambayo yanapaswa kutimizwa kuwezesha raia kuitumia haki yake ya kupiga kura.

Ufafanuzi

  • Kila raia anayo haki ya kupiga kura katika uchaguzi iwapo ametimiza miaka 18 na kuendelea.
  • Raia anayepiga kura lazima awe na akili timamu
  • Raia lazima awe na uraia wa nchi moja yaani Tanzania
  • Raia awe hajatiwa hatiani kwa makosa fulani ya kijinai
  • Raia lazima awe na kitambulisho cha kudhibitisha umri, uraia au uandikishwaji kwenye daftari la wapiga kura.

Katiba ya JMT inaipa mamlaka Bunge la JMT kupitia Ibara ya 5 (3) kutunga sheria ya Uchaguzi ambayo itaweka masharti kuhusu mambo kadhaa ikiwepo;

  • Uanzishwaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura, na kuweka utaratibu wa kurekebisha yaliyomo katika Daftari hilo;
  • Kutaja sehemu na nyakati za kuandikisha wapiga kura katika Daftari hilo;
  • Utaratibu wa kumwezesha mpiga kura aliyejiandikisha sehemu moja kupiga kura sehemu nyingine na kutaja masharti ya utekelezajiwa utaratibu huo;
  • Kutaja kazi na shughuli za Tume ya Uchaguzi na utaratibu wa kila uchaguzi ambao utaendeshwa chini ya uongozi na usimamii wa Tume ya Uchaguzi.

Hitimisho

Haki ya kupiga kura katika changuzi mbali mbali ndio mamlaka kuu aliyonayo mwananchi katika kuamua hatma ya uongozi na mwenendo wa nchi yake. Kila mwananchi anapaswa kuifahamu haki hii na kuitumia ipasavyo kila nafasi ya uchaguzi inapojitokeza ili kushiriki katika maamuzi juu ya mustakabali wa sasa wa nchi na maisha ya baadae.

Kwa kawaida ya Katiba ya JMT uchaguzi mkuu hufanyika kila baada ya miaka 5 ambapo wanachaguliwa madiwani kuwakilisha Kata, Wabunge kuwakilisha majimbo na kuchaguliwa Rais na Makamu wa Rais kuunda Serikali.

Kumbuka ‘kutokujua sheria si utetezi iwapo utatenda kosa lolote’ tafuta maarifa sahihi ya kisheria yakusaidie kufanya maamuzi sahihi kila siku. Wasiliana nami kwa kutembelea mtandao wako wa  www.ulizasheria.co.tz

Wako,

Isaack Zake, Wakili