Haki ya Usawa

Utangulizi

Karibu sana ndugu msomaji na mfuatiliaji wa ukurasa huu  kupitia mtandao wako wa www.ulizasheria.co.tz. Kama kawaida yetu lengo la kukuletea makala hizi fupi ni kukusaidia kuishi kwa mujibu wa sheria kila siku. Leo tunakwenda kujifunza juu ya Haki ya Usawa. Karibu tujifunze.

Maana ya Haki ya Usawa

Haki ya usawa ni moja wapo ya haki za binadamu ambayo imeainishwa kwenye Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya 1977. Asili ya haki za binadamu ni kutokana na Tangazo la Ulimwengu la Haki za Binadamu la mwaka 1948 chini ya Umoja wa Mataifa.

Hii ni haki ya msingi na haki ya kwanza kwa kila binadamu. Haki hii inaainishwa katika Katiba ya JMT kwenye Ibara ya 12 inayosema;

‘Binadamu wote huzaliwa huru, na wote ni sawa’

Kwa mujibu wa Ibara hii ya Katiba ya JMT tunaona kuwa kila binadamu anazaliwa akiwa huru na anapata hadhi sawa na binadamu mwengine mahali popote duniani. Chimbuko la utambuzi wa haki hizi unatokana na historia ya mwanadamu tangu awali ambapo wapo ambao walitwaa mamlaka juu yaw engine na kuwafanya watumwa au kuwabagua kulingana na rangi, taifa, kabila au uwezo.

Hivyo tamko la haki za kibinadamu linatutaka wananchi wote na watu wote ulimwengu mzima kuheshimu binadamu wengine mahali popote pasipo kutazama rangi, jinsia, kabila, jamaa, ukoo au asili ya mtu alimradi amezaliwa ni binadamu basi sheria inatambua uhuru wake na usawa wake.

Katiba ya JMT kwenye Ibara ndogo ya 12 (2) inaendelea kusema kuwa

‘ Kila mtu anastahili heshima ya kutambuliwa na kuthaminiwa utu wake’

Jambo hili ni muhimu sana kwetu sote wananchi kufahamu kuwa hatuna tofauti yoyote kati yetu iwe kwa uwezo wa kifedha, kielimu, au hali ya mtu aliyozaliwa nayo ikiwa ana ulemavu au la. Katiba inatutaka tuheshimu utu wa mtu jinsi ile alivyo kwamba ni binadamu na si kunasibisha utu huo na mambo mengine.

Hali hii itatupa sisi sote kuheshimu wenzetu, kuthamini mtu mwenzako na hata kumsadia kwa kuwa ni binadamu mwenzako.

Uhuru huu ambao kila mtu anazaliwa nao unaweza kupotezwa tu pale endapo mtu atadhibitika kutenda makosa na kutiwa hatiani kwa mujibu wa sheria.

Hitimisho

Uhuru na haki ya usawa kwa binadamu wote ni jambo linalolindwa Kikatiba kama ilivyoanishwa kwenye Katiba yetu. Ni muhimu sana kwa mwananchi kuitambua haki hii na kuchukua hatua zinazostahili kuhakikisha haki hii inalindwa kwake na kwa wengine.

Kumbuka ‘kutokujua sheria si utetezi iwapo utatenda kosa lolote’ tafuta maarifa sahihi ya kisheria yakusaidie kufanya maamuzi sahihi. Wasiliana nami kupitia zakejr@gmail.com

Wako

Isaack Zake, Wakili