Haki ya Kufanya Kazi

Utangulizi

Karibu sana ndugu msomaji na mfuatiliaji wa ukurasa huu  kwenye mtandao wako wa www.ulizasheria.co.tz . Kama kawaida yetu lengo la kukuletea makala hizi fupi ni kukusaidia kuishi kwa mujibu wa sheria kila siku. Katika makala iliyopita tulijifunza juu ya Uhuru wa mtu kushiriki shughuli za umma. Leo tunaendelea na mfululizo makala juu ya haki mbali mbali za kibinadamu kama zilivyoanishwa kwenye Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Karibu tujifunze.

Maana ya Haki ya Kufanya Kazi

Katiba ya JMT inaeleza wazi kuwa kila mwananchi ana Haki ya Kufanya Kazi. Ibara ya 22 (1) ya Katiba ya JMT inasema

kila mtu anayo haki ya kufanya kazi’

Ufafanuzi

Kazi ndio msingi wa maendeleo ya jamii yoyote ulimwenguni. Kazi ni kipimo cha utu na chimbuko la ustawi wa jamii katika kila nyanja. Hivyo Katiba inatoa fursa ya kila mtu kufanya kazi.

Kazi zinahusisha shughuli zozote za kuzalisha, biashara, ubunifu au huduma mbalimbali ambazo zina lengo la kuongeza tija, manufaa na ufanisi katika jamii.

Katiba ya JMT inaendelea kufafanua juu ya haki ya kazi katika Ibara ya 22 (2) kwamba

‘kila raia anastahili fursa na haki sawa, kwa masharti ya usawa, ya kushika nafasi yoyote ya kazi na shughuli yoyote iliyo chini ya Mamlaka ya Nchi’

Hii inatoa fursa kwa raia yoyote mwenye vigezo vya kushiriki kazi pasipo kujali jinsia, ukabila au rangi yake ana haki ya kupata nafasi ya kufanya kazi katika taasisi za umma.

Muhimu kuzingatia katika suala la kazi kwamba lazima iwe shuguli halali kwa mujibu wa sheria. Watu wengi wanajiingiza kwenye mambo mengi ya kujipatia fedha pasipo kuleta thamani au manufaa kwa jamii shughuli ambazo ni kinyume na sheria na maadili ya nchi haziwezi kuwa sehemu ya kazi.

Wengine wanasema ‘kazi ni kazi bora mkono kinywani’ usemi huu una ukweli nusu kwani si kila kazi ambayo inaweza kukusababishia kipato, ni halali. Ni muhimu kufahamu suala si kupata kipato au fedha, msingi wa kupima ni je kipato hicho kimetokana na shughuli halali ambayo ipo na inatambuliwa na sheria?

Moja ya changamoto kubwa inayozikumba nchi nyingi zinazoendelea Tanzania ikiwemo ni hali ya ukosefu wa ajira. Wapo wasomi wengi sana katika soko la ajira, pia wapo wengine ambao hawana elimu ya kutosha nao wanahitaji ajira. Hata hivyo jukumu la kuhakikisha uwepo wa ajira si la Serikali peke yake, bali sekta binafsi na hata mtu mmoja mmoja kutafuta suluhu hii.

Haki ya kufanya kazi ni ya kila mtu hivyo ni suala pana zaidi ambalo linapaswa kuangaliwa si kwa ngazi ya kitaifa bali kuanzia ngazi binafsi kwani haki hii imetolewa kwa kila mtu. Ni muhimu kwa kila mtu aliyefikia umri wa kuzalisha atafute shughuli halali ya kufanya ambayo italeta tija, manufaa na ufanisi katika ngazi ya mtu binafsi, familia na taifa kwa ujumla.

Hitimisho

Kazi ndio msingi mkuu wa kuzalisha, kutoa huduma na kufanya biashara ambazo zinaleta fedha, utajiri na mali kwa kila mmoja wetu. Kila mmoja achukue wajibu wa kufanya kazi iwe ameajiriwa au hajaajiriwa cha msingi afanye kitu kitakachoweza kubadilisha maisha ya jamii inayomzunguka kuwa bora zaidi kwa kutatua changamoto zilizopo. Tabia iliyojitokeza katika jamii yetu ya kuishi maisha ya bahati na sibu, michezo ya kubet kila kona haiwezi kubadili maisha ya mtu binafsi au familia au taifa kwa ujumla bali ni janga linalotishia ustawi wetu. Kama unataka fedha, mali na utajiri fanya kazi, fanya kazi, fanya kazi.

 ‘una haki ya kufanya kazi, tafuta kazi, buni kazi na ufanya kazi’

Kumbuka ‘kutokujua sheria si utetezi iwapo utatenda kosa lolote’ tafuta maarifa sahihi ya kisheria yakusaidie kufanya maamuzi sahihi kila siku. Wasiliana nami kupitia zakejr@gmail.com

Nakutakia siku njema sana ndugu yangu

Wako

Isaack Zake, Wakili