16. Vigezo vya Mwajiri kusitisha Ajira Kihalali

Utangulizi

Ndugu msomaji wa makala za Uchambuzi wa Sheria ambapo tumekuwa tukiichambua Sheria ya Kazi, tumeendelea kuwa pamoja kwa kipindi chote hiki. Makala iliyopita tuliweka msingi wa mfululizo wa makala kuhusu usitishaji wa ajira. Katika makala ya leo tunaanza kuangalia aina ya Usitishaji wa Halali wa Ajira. Karibu tujifunze.

Maana ya Usitishaji Halali wa Ajira

Kama tulivyotafsiri katika makala iliyopita ni aina ya usitishaji wa ajira ambao unazingatia sababu za msingi, utaratibu wa haki na kufutata matakwa ya Sheria ya Ajira.

Sheria ya Ajira inabainisha juu ya usitishaji wa ajira ulio halali na taratibu zinazopaswa kufuatwa. Sheria ya Ajira imeweka vigezo vya kisheria ambavyo vikifuatwa basi usitishaji huo wa ajira utakuwa ni halali.

Kuhusu uhalali wa usitishwaji wa ajira, mwajiri ana jukumu la kudhibitisha vigezo ambavyo vimewekwa kwenye sheria ambavyo tunakwenda kuvijadili katika makala hii ya leo. Mambo ya msingi ya kuzingatia katika uhalali;

  1. Mwajiri lazima awe na sababu za msingi na halali za kusitisha ajira.

Sheria inamtaka mwajiri kutoa sababu za msingi za kusitisha ajira ya mfanyakazi wakati wote. Mara mahusiano ya kazi yanapoanza baina ya pande mbili yaani mfanyakazi na mwajiri kunakuwepo na hali ya kutegemeana, hivyo mwajiri hawezi kusitisha ajira au kumfukuza mfanyakazi pasipo kutoa sababu za msingi. Sheria inabainisha sababu ambazo zinaweza kutolewa na mwajiri kwa mfano; utovu wa nidhamu, uwezo mdogo wa kufanya kazi, kutohitajika, mahitaji ya uendeshaji ya mwajiri.n.k muhimu kuwa sababu hiyo lazima idhibitishwe kuwa ni ya kweli na halali katika mazingira hayo.

  1. Mwajiri lazima afuate utaratibu wa kusitisha ajira unaozingatia misingi ya haki.

Usitishaji wa ajira ni suala la mchakato na si suala la ghafla. Kama vile mwajiri alivyofanya mchakato wa kumwajiri mfanyakazi pia upo mchakato wa kusitisha ajira kwa sababu yoyote ile. Hivyo mbali kuwa na sababu halali mwajiri lazima afuate mchakato unaohusiana na sababu ambayo anasitisha ajira ya mfanyakazi. Kwa mfano upo mchakato wa kusitisha ajira kutokana na utovu wa nidhamu, pia upo mchakato wa kusitisha ajira kutokana na kutohitajika au mahitaji ya uendeshaji.

  1. Mwajiri lazima azingatie vipengele vya mkataba vinavyohusiana na usitishaji wa ajira.

Wakati wa usitishaji wa ajira, zipo haki ambazo zimeainishwa kwenye mkataba baina ya mwajiri na mfanyakazi endapo kutatokea suala la usitishaji wa ajira. Mwajiri ni lazima ahakikishe haki hizo zinazingatiwa na kutekelezwa kikamilifu.

  1. Mwajiri lazima azingatie masuala ya notisi, kiiunua mgongo, nauli ya usafiri na malipo mengine ya stahiki ya mfanyakazi.

Sheria ya Ajira inaaisha wajibu wa mwajiri pindi amwachishapo kazi mfanyakazi kuzingatia kulipa malipo ya kisheria. Malipo hayo ni notisi, kiinua mgogongo na nauli ya kusafiri kwa mfanyakazi endapo aliajiriwa nje ya eneo lake la ajira.

Hivi ndivyo vigezo vya msingi ambavyo wakati wote wa usitishaji wa ajira unaofanywa na mwajiri lazima kuzingatiwa na kufuatwa. Kwa njia hii itasaidia pande zote kujua endapo usitishaji wa ajira ulifanyika kihalali au la.

Hitimisho

Mara nyingi migogoro iliyo katika Tume na Mahakama ya Kazi inahusisha suala la usitishaji wa ajira usio halali. Ni muhimu sana kwa mwajiri kuzijua taratibu au kutafuta ushauri wa kisheria kwa wataalam kabla ya kuchukua hatua za kusitisha ajira ili kuepuka makosa ya kimsingi katika usitishaji wa ajira.

Kumbuka ‘kutokujua sheria si utetezi iwapo utatenda kosa lolote tafuta maarifa sahihi ya kisheria yakusaidie kufanya maamuzi sahihi kila siku. Wasiliana nami kupitia zakejr@gmail.com

Nakutakia siku njema sana ndugu yangu

Wako

Isaack Zake, Wakili.