Haki ya Kupata Ujira wa Haki
Utangulizi
Karibu sana ndugu msomaji na mfuatiliaji wa ukurasa huu kwenye mtandao wako wa www.ulizasheria.co.tz . Kama kawaida yetu lengo la kukuletea makala hizi fupi ni kukusaidia kuishi kwa mujibu wa sheria kila siku. Katika makala iliyopita tulijifunza juu ya Haki ya Kufanya Kazi. Leo tunaendelea na mfululizo makala juu ya haki mbali mbali za kibinadamu kama zilivyoanishwa kwenye Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Karibu tujifunze
Maana ya Haki ya Kupata Ujira wa Haki
Katiba ya JMT inaeleza wazi kuwa kila mwananchi anayo Haki ya kupata Ujira wa haki. Ibara ya 23 (1) ya Katiba ya JMT inasema
‘kila mtu, bila ya kuwapo ubaguzi wa aina yoyote, anayo haki ya kupata ujira unaolingana na kazi yake, na watu wote wanaofanya kazi kulingana na uwezo wao watapata malipo kulingana na kiasi na sifa za kazi wanazofanya’
Ufafanuzi
Kama tulivyoeleza kwenye makala iliyopita ya kwamba kazi ndio msingi wa maendeleo ya jamii yoyote. Ujira au malipo au mshahara ni matokeo ya kazi halali ya mtu.
Katiba ya JMT inatamka bayana kuwa mtu anayefanya kazi anayo haki ya kupata ujira unaostahili kazi aliyofanya. Haki hii haitakiwi kubagua watu, yaani wale wanaofanya kazi wasibaguliwe kwa vigezo vya kijinsia, kisiasa, ukabila au asili ya mahali walipotoka. Kigezo muhimu cha malipo ni sifa na uwezo wa kufanya kazi kwa mujibu wa makubaliano kati ya mwajiri na mfanyakazi
Pamekuwa na malalamiko kwa baadhi ya watu wakisema wageni wanapewa malipo makubwa kulinganishwa na wazawa katika majukumu wanayofanya ingawa ni sawa sawa. Zipo sera na taratibu za kisheria kuhakikisha kuwa kila mfanyakazi anayestahili kulipwa ujira analipwa sawa pasipo ubaguzi. Pamoja na malalamiko haya wazawa wengine wanachangia hali hii ya kutokufanya kazi kwa nidhamu, kukosa uadilifu na kujituma. Wengi wanafanya kazi kwa mazoea, ndio maana inawezekana waajiri au wawekezaji wanatoa kipaombele kwa wageni zaidi kuliko wazawa.
Katiba ya JMT inaendelea kufafanua juu ya haki ya ujira katika Ibara ya 23 (2) kwamba
‘kila mtu anayefanya kazi anastahili kupata malipo ya haki’
Malipo ya haki yanatokana na kiwango cha uzalishaji wa kazi kilichofanywa na mfanyakazi. Sheria za kazi zinaainishwa viwango vya kima cha chini katika sekta mbali mbali za uzalishaji. Muhimu kwa wafanyakazi kuzijua sheria za kazi na waajiri pia kuzizingatia ili kuepusha unyonyaji wa nguvu kazi na migogoro mahala pa kazi.
Mabadiliko ya sayansi na teknolojia kwa kiwango kikubwa yanaathiri masuala ya ajira na kusababisha ukosefu wa ajira. Mahala ambapo kazi ilikuwa ikifanywa na watu 10 teknolojia inaweza kuwapunguza na kubaki na mtu 1. Changamoto hizi zinafanya wafanyakazi wawe radhi kufanya kazi hata chini ya kiwango cha ujira ambacho wanastahili kulipwa.
Namna ya kuweza kusaidia wafanyakazi wapate ujira stahiki, ni kuhakikisha wanaunda vyama vya wafanyakazi vyenye nguvu na wataalam wa kuweza kuzingatia na kusimamia maslahi yao. Weledi, ubunifu na ufahamu wa watendaji wa vyama vya wafanyakazi utawezesha wafanyakazi kufikia malengo hasa ya kimaslahi katika majadiliano, mikataba na stahiki nyingine.
Pia taasisi za kiserikali zinazosimamia utekelezaji wa sheria za kazi, zinapaswa kuchukua wajibu wa kufanya ukaguzi mara kwa mara kuangalia uzingatiaji wa sheria za kazi kuhusiana na maslahi mapana ya wafanyakazi na waajiri.
Hitimisho
Haki ya kupata ujira kwa kila mfanyakazi anayefanya kazi halali ni muhimu sana kwani itamsaidia katika ustawi binafsi na kupunguza umaskini katika jamii. Muhimu sana kwa wafanyakazi kuwa waaminifu, wenye nidhamu na juhudi katika kazi wanazopewa. Wafanyakazi waondokane na fikra za kuonewa, bali wajitoe katika kufanya kazi kwa ufanisi kila wakati. Waajiri pia waondokane na fikra za kuibiwa na wafanyakazi, wote wajenge mfumo wa kuaminiana ili manufaa, tija na ufanisi vionekane mahali pa kazi na wafanyakazi walipwe kwa haki pasipo ubaguzi
‘timiza wajibu wako kikamilifu ili upate ujira wa haki’.
Kumbuka ‘kutokujua sheria si utetezi iwapo utatenda kosa lolote’ tafuta maarifa sahihi ya kisheria yakusaidie kufanya maamuzi sahihi kila siku. Wasiliana nami kupitia zakejr@gmail.com
Nakutakia siku njema sana ndugu yangu
Wako
Isaack Zake, Wakili