Haki ya Kumiliki Mali

Utangulizi

Karibu sana ndugu msomaji na mfuatiliaji wa ukurasa huu kwenye mtandao wako wa www.ulizasheria.co.tz . Kama kawaida yetu lengo la kukuletea makala hizi fupi ni kukusaidia kuishi kwa mujibu wa sheria kila siku. Katika makala iliyopita tulijifunza juu ya Haki ya Kulipwa Ujira wa Haki. Leo tunaendelea na mfululizo makala juu ya haki mbali mbali za kibinadamu kama zilivyoanishwa kwenye Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Karibu tujifunze.

Maana ya Haki ya Kumiliki Mali

Katiba ya JMT inaeleza wazi kuwa kila mwananchi anayo Haki ya kumiliki mali. Ibara ya 24 (1) ya Katiba ya JMT inasema

kila mtu anayo haki ya kumiliki mali, na haki ya hifadhi ya mali yake aliyonayo kwa mujibu wa sheria’

Ufafanuzi

Katiba ya JMT inaeleza wazi kuwa mtu yeyote ana haki ya kumiliki mali ilimradi tu mali hiyo imepatikana kwa njia halali. Mtu anaweza kumiliki mali kwa kufanya kazi na kuzalisha mali, au kurithi au kwa njia ya zawadi. Katiba inatoa hakikisho la uhifadhi wa mali ya mtu awapo katika nchi yetu. Yaani sheria inakuhakikishia kuwa mali uliyonayo inapatiwa ulinzi wa kisheria na vyombo vya dola ikibidi katika kuhakikisha mali yao hainyang’anywi kwa nguvu au kwa hila. Tuna sheria ya makosa ya Jinai ambayo inaonesha makosa yanayohusiana na mali jinsi sheria inavyowaadhibu walitiwa hatiani. Pia lipo Jeshi la Polisi lenye jukumu la kuhakikisha usalama wa raia na mali zao katika nchi.

Katiba ya JMT inaendelea kufafanua juu ya haki ya  mali katika Ibara ya 24 (2) kwamba

‘Bila ya kuathiri masharti ya ibara ndogo ya (1), ni marufuku kwa mtu yeyote kunyang’anywa mali yake kwa madhumuni ya kuitaifisha au madhumuni mengineyo bila ya idhini ya sheria ambayo inaweka masharti ya kutoa fidia inayostahili’

Hapa Katiba inaweka zuio hata kwa Mamlaka za Nchi kutokuwa na uwezo wa kunyang’anya au kutaifisha mali ya mtu pasipo kufuata sheria inayotoa mwanya huo.

Endapo Mamlaka zinahitaji kutumia eneo la mtu kama kiwanja kwa shughuli za umma, basi sheria za Ardhi zinaongoza ulipwaji wa fidia unaostahili kwa mwathiriwa wa zoezi hilo alimradi eneo hili liwe lake kihalali na si maeneo ambayo hayaruhusiwi kumilikiwa na mwananchi kwa sheria.

Hitimisho

Haki ya kumiliki mali ni mojawapo ya haki muhimu sana na inayohakikisha uzalishaji mkubwa katika taifa. Haki hii inachagiza maendeleo kwa watu kuwekeza akili zao, nguvu zao katika kutenda kazi kwa bidii ili kuzalisha mali.

Nitoe rai kwa wananchi wenzangu kuwa hakuna wa kukuzuia kupata mali isipokuwa fikra zako mwenyewe, haki hii haijatolewe kwa wasomi au watu wa daraja Fulani, bali kwa watu wote pamoja na wewe msomaji. Tumia haki hii vizuri kwa kufanya shughuli halali kujenga uchumi wako, familia na wa taifa kwa ujumla.

 ‘haki ya umiliki ni yako binafsi, chukua hatua binafsi umiliki mali kujenga uchumi wako na wa taifa’.

Kumbuka ‘kutokujua sheria si utetezi iwapo utatenda kosa lolote’ tafuta maarifa sahihi ya kisheria yakusaidie kufanya maamuzi sahihi kila siku. Wasiliana nami kupitia zakejr@gmail.com

Nakutakia siku njema sana ndugu yangu

Wako

Isaack Zake, Wakili