15. Aina za Usitishaji Ajira Kihalali

 

Utangulizi

Ndugu msomaji wa makala za Uchambuzi wa Sheria ambapo tumekuwa tukiishambua Sheria ya Kazi, tumeendelea kuwa pamoja kwa kipindi chote hiki. Makala iliyopita tuliweka msingi wa mfululizo wa makala kuhusu usitishaji wa ajira. Katika makala ya leo tunaanza kuangalia aina ya Usitishaji wa Halali wa Ajira. Karibu tujifunze.

Usitishaji Halali wa Ajira

Kama tulivyotafsiri katika makala iliyopita ni aina ya usitishaji wa ajira ambao unazingatia sababu za msingi, utaratibu wa haki na kufutata matakwa ya Sheria ya Ajira.

Sheria ya Ajira inabainisha juu ya usitishaji wa ajira ulio halali na taratibu zinazopaswa kufuatwa. Sheria ya Ajira imebainisha mazingira na aina ya usitishaji wa ajira ambao utahesabika kuwa ni halali.

 

  1. Usitishaji wa ajira kwa makubaliano ya kimkataba

Sheria ya Ajira inatambua kuwa mahusiano ya kiajira ni ya kimkataba, hivyo upo uwezekano mahusiano hayo kumalizika kwa mujibu wa mkataba. Kwenye mahusiano ya ajira pande zote yaani mwajiri na mfanyakazi wanaweza kuweka kipengele cha kumalizika mkataba wao katika muda fulani. Iwapo mkataba wa ajira ni wa muda maalum basi muda huo ukifika itahesabika kuwa mahusiano ya mwajiri na mfanyakazi yamefikia ukomo.

Hata hivyo, yapo mazingira ambayo mkataba wa muda maalum unaweza kuendelea endapo pande mbili zitahuisha mkataba huo au mfanyakazi akiendelea kufanya kazi baada ya mkataba kumalizika na mwajiri akaendelea kumtambua kama mfanyakazi wake.

 

  1. Usitishaji wa wa ajira wa moja kwa moja (automatic termination)

Aina hii ya usitishaji wa ajira inajitokeza pale tu kinapotokea kifo cha mmoja wapo au kupoteza sifa za kibiashara/taaluma ya mwajiri. Kwamba mfanyakazi anaweza kufariki wakati ana mkataba wa ajira au mwajiri akapoteza sifa za kuendelea kuwa na kazi hizo, basi hapo usitishaji wa ajira utakuwa ni wa moja kwa moja. Usitishaji wa ajira wa moja kwa moja pia unajitokeza pale mfanyakazi anapotimiza umri wa kustaafu kwa mujibu wa mkataba au sheria za kazi endapo mkataba haukuonesha umri huo.

  1. Usitishaji wa ajira unaofanywa na mfanyakazi

Mfanyakazi pia anaruhusiwa kusitisha mahusiano ya kiajira baina yake na mwajiri. Endapo mfanyakazi yupo katika mkataba wa muda maalum na anataka kusitisha ajira anapaswa kumpa taarifa mwajiri ili aweze kusitisha ajira kabla ya mkataba kumalizika. Pia mfanyakazi akiwa kwenye mkataba wa kudumu anaweza kutoa taarifa ya maandishi ya kusitisha ajira kabla ya umri wa kustaafu. Kusitisha huku ajira kwa mfanyakazi kunaitwa kujiuzulu kazi.

Hatahivyo, yapo mazingira ambayo mfanyakazi atasitisha ajira kutokana na hali ya kiajira kwa mwajiri ya kumnyanyasa au kumdhalilisha au kuacha adhalilishwe utu wake kiasi kwamba akaamua kuacha kazi. Katika mazingira haya itahesabika kuwa ameachishwa kazi na mwajiri hata kama mfanyakazi ameandika taarifa ya kujiuzulu.

 

  1. Usisitishaji wa ajira unaofanywa na mwajiri

Mwajiri pia anayo haki ya kusitisha ajira ya mfanyakazi kabla ya kipindi cha makubaliano kumalizika au baada ya kumalizika. Vipo vigezo ambavyo mwajiri anapaswa kuvizingatia wakati wa kumwachisha mfanyakazi kazi. Muhumu ni mwajiri kuzingatia sheria, taratibu na mazoea ambayo yapo katika eneo la kazi ili usitishwaji wa ajira hiyo usiibue migogoro ya baadae.

Haya ni mazingira ya usitishwaji wa ajira kihalali kwa mujibu wa sheria ya ajira na mahusiano kazini. Ni muhimu kufahamu kila aina ya usitishwaji wa ajira una taratibu zake ambazo pande zote zinapaswa kuzingatia wakati wote.

Hitimisho

Usitishaji wa ajira kihalali unasaidia pande zote kuendeleza mahusiano mazuri hata baada ya ajira kukoma. Hii inaweza kuleta fursa za baadae kwa pande mbili kuendeleza mahusiano ya kiajira au kibiashara. Mara nyingi mahusiano ya mfanyakazi na mwajiri wakati wa kuanza kazi yanakuwa mazuri na mwishoni huwa yanaaribika kwa kila upande kutojua haki na wajibu wa kisheria na kimkataba wanaopaswa kutekeleza. Muhimu kuzijua taratibu za kisheria katika usitishaji wa ajira.

Kumbuka ‘kutokujua sheria si utetezi iwapo utatenda kosa lolote tafuta maarifa sahihi ya kisheria yakusaidie kufanya maamuzi sahihi kila siku. Wasiliana nami kupitia zakejr@gmail.com

Nakutakia siku njema sana ndugu yangu

Wako

Isaack Zake, Wakili.

 

 

3 replies
  1. lanitto mapenzi
    lanitto mapenzi says:

    Asante mheshimiwa ni kweli hilo jambo ni gumu kwangu pia na mwajiri wangu mwanzo wa kuniajiri tulianza vizur hata mkataba sina ila kwa sasa simuelewi akinifukuza haki zangu nitapata kweli?

    • ulizasheria
      ulizasheria says:

      Karibu sana Mary Oisso

      Ndio tunatoa mafunzo mbalimbali kwa wadau wa sheria za Kazi wakiwepo HR’s kwa mawasiliano zaidi piga simu 0713 888 040. Pia unaweza kututumia mawasiliano yako kwa namba hizo au e-mail ya zakejr@gmail.com

Comments are closed.