Wajibu wa Kushiriki Kazini

Utangulizi

Karibu sana ndugu msomaji na mfuatiliaji wa ukurasa huu kwenye mtandao wako wa www.ulizasheria.co.tz . Kama kawaida yetu lengo la kukuletea makala hizi fupi ni kukusaidia kuishi kwa mujibu wa sheria kila siku. Katika makala iliyopita tulijifunza juu ya Haki ya Kumiliki Mali. Leo tunaendelea na mfululizo makala juu ya wajibu wa kila mwanajamii kama uilivyoanishwa kwenye Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Karibu tujifunze

Maana ya Wajibu

Katika makala moja wapo za mwanzoni Sheria Leo.6:Wajibu ni Nini? nilizingumza maana ya neno wajibu. Tupitie tena maana hiyo kutusadia kuelewa wajibu unaoainishwa kwenye Katiba ya JMT

Kulingana na kamusi ya Kiswahili neno wajibu lina maana ya ‘jambo linalomlazimu mtu kulitimiza, jambo ambalo mtu hana hiari nalo katika kulifanya; sharti, faradhi, jukumu’

Kwa tafsiri kutoka kwenye Kamusi ya maneno ya Kisheria, neno  wajibu lina maana ya ‘ tendo au vitendo ambavyo mtu analazimika kufanya kwa mujibu wa sheria’

Kwa maana zinazobainishwa hapo juu inaonesha kuwa sheria ndio msingi wa wajibu, sheria ndio inaeleza kile ambacho wewe  mwananchi unawajibika kufanya. Sheria inakushurutisha ukifanye au ufanye jambo fulani.

Hali kadhalika katika Katiba ya JMT baada ya kueleza haki zile ambazo mwananchi anazo kama tulivyoona katika mfululizo wa makala zilizopita, pia inaeleza wajibu wa mwananchi yaani mambo anayolazimika kufanya ili haki hizo ziweze kufikiwa.

Maana ya Wajibu wa Kushiriki Kazini

Katiba ya JMT inaeleza wazi kuwa kila mwananchi anao Wajibu wa kushiriki katika kazi. Ibara ya 25 (1) ya Katiba ya JMT inasema

kazi pekee ndiyo huzaa utajiri wa mali katika jamii, ndilo chimbuko la ustawi wa Wananchi na kipimo cha Utu. Na kila mtu anao wajibu wa-

  • Kushiriki kwa kujituma na kwa uaminifu katika kazi halali na ya uzalishaji mali; na
  • Kutimiza nidhamu ya kazi na kujitahidi kufikia malengo ya uzalishaji mali ya binafsi na yale malengo ya pamoja yanayotakiwa au yaliyowekwa na sheria’

Ufafanuzi

Kama tulivyofafanua katika makala zilizopita juu ya nafasi na umuhimu wa kazi katika jamii, Katiba ya JMT nayo inatoa msisitizo huo juu ya kazi. Kwamba kazi ndio huzaa fedha, mali na utajiri na pekee inaonesha ustawi wa jamii. Kama tunaona jamii yetu haijaendelea, matatizo ya ujinga, umasikini na maradhi yanazidi kuongezeka tatizo hatujawekeza nguvu za kutosha katika kufanya kazi.

Katiba inabainisha kuwa Utu wa mtu unapimwa kwa kile anachofanya katika jamii yake kwa kuifanya kuwa bora zaidi. Pamekuwa na mtazamo hasi sana katika fikra za watu ili mtu uonekane una utu basi uwe unatoa misaada mingi kwa watu. Hili si jambo zuri sana kwani misaada mingi hudumaza fikra za kujitegemea. Wapo watu ambao kwa mtazamo wa nje wanaweza kufanya kazi na kuzalisha, lakini kutwa unawakuta barabarani wanaomba omba. Haipasi kuwa hivi kwa jamii yetu, ni lazima kazi iheshimiwe na utu wa watu hutambuliwe kwa thamani anayoitoa kwa jamii kutokana na kazi anayofanya.

Pia upo mtazamo hasi kwamba utu wa mtu unapimwa kutokana na cheo, hadhi au nafasi aliyonayo mtu kwenye jamii au uongozi. Jambo hili si sahihi hata kidogo, ni lazima mwananchi mmoja mmoja ajithamini mwenyewe kwa kile anachofanya. Maswala ya cheo au hadhi ni mambo ya muda tu, muhimu kwenye kile cheo au nafasi umeitumia vipi kwa kuboresha maisha ya wengine.

Katiba ya JMT inaeleza kuwa kila mwananchi ana wajibu wa kushiriki katika kazi, hili si ombi bali ni suala la lazima kwa mtu yeyote. Katika ushiriki huu wa kazi mwananchi anapaswa kuhakikisha anafanya yafuatayo;

  • Kujituma katika kazi, yaani kufanya kazi kwa bidii yote mtu anayohitajika kuitoa
  • Kufanya kazi kwa uaminifu. Hapa kuna changamoto kubwa watu hawaaminiki kabisa iwe kwenye biashara, huduma na hata kazi za umma
  • Nidhamu ya kazi ili kukusadia kufika malengo binafsi na malengo ya pamoja ya shirika au umma.

Mwananchi yeyote anayefanya kazi za uzalishaji ni lazima afanye tathmini yake juu ya mwenendo wake katika kazi ikiwa anaonesha hali ya kujituma, uaminifu na nidhamu katika kazi.

 

Hitimisho

Wajibu wa kazi hauishii kwenda kazini na kusaini umefika na kisha baada ya saa za kazi kwenda nyumbani, wajibu huu ni zaidi ya hapo. Pamoja na kuwa na wafanyakazi wengi tumeshuhudia mashirika na taasisi binafsi zikipunguza wafanyakazi mojawapo ya tatizo ni wafanyakazi kutokuzalisha ipasavyo hivyo gharama za uendeshaji  kuwa kubwa kuliko faida. Mfanyakazi hakikisha unafanya kazi kwa moyo mmoja, toa nguvu zako, moyo wako, akili yako kwa ajili ya kazi, si suala la kumnufaisha mwajiri wako bali ni kwa ajili yako kwanza kwa tija utakayoitoa kwenye jamii lazima utafikia malengo yako.

kwa nidhamu, uaminifu na kujituma tutende kazi zetu kila siku kuzaa utajiri kwetu binafsi na kwa ustawi wa jamii.

Kumbuka ‘kutokujua sheria si utetezi iwapo utatenda kosa lolote’ tafuta maarifa sahihi ya kisheria yakusaidie kufanya maamuzi sahihi kila siku. Wasiliana nami kupitia zakejr@gmail.com

Nakutakia siku njema sana ndugu yangu

Wako

Isaack Zake, Wakili