Katazo la Kazi za Shuruti

Utangulizi

Karibu sana ndugu msomaji na mfuatiliaji wa ukurasa huu kwenye mtandao wako wa www.ulizasheria.co.tz . Kama kawaida yetu lengo la kukuletea makala hizi fupi ni kukusaidia kuishi kwa mujibu wa sheria kila siku. Katika makala iliyopita tulijifunza juu ya Wajibu wa Kushiriki katika Kazi kwa wananchi wote. Leo tunaendelea na mfululizo makala juu ya wajibu wa kila mwanajamii kama uilivyoanishwa kwenye Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Karibu tujifunze.

Maana ya Kazi za Shuruti

Maana ya kazi ya shuruti ni aina ya kazi ambayo mtu analazimishwa kuifanya pasipo hiyari yake mwenyewe ikiwa ni kwa njia ya vitisho au udanganyifu.

Katiba ya JMT inaeleza wazi kuwa hairuhusiwi mtu kufanyishwa kazi za shuruti. Ibara ya 25 (2) ya Katiba ya JMT inasema

bila kujali masharti ya ibara ndogo ya (1), hakutakuwapo  na kazi ya shuruti katika Jamhuri ya Muungano’

Ufafanuzi

Katiba inatamka wazi katazo la kazi ya shuruti kwa mtu yeyote kufanyishwa au kusababisha kazi hizo kufanywa hapa Tanzania. Kazi za shuruti zinahusisha kazi za kikatili, au kazi ya kutweza au kazi nyingine inayodhalilisha utu wa mtu. Katika kazi za shuruti zinaonekana kwenye maeneo ya mashamba, kazi za majumbani au kwenye migodi, biashara ya watu kwa madhumuni ya ngono na maeneo mengine mengi. Sheria inakataza kazi zozote za shuruti au kudhalilisha watu.

Hata hivyo Katiba inatoa ufafanuzi zaidi ni mazingira gani ya kazi yakifanyika haitahesabika kama ni kazi za shuruti au kazi za kikatili au ya kutweza, hii ni kwa mujibu wa Ibara ya 25 (3) inasema,

‘Kwa madhumuni ya ibara hii, na katika Katiba hii kwa jumla, ifahamike kwamba kazi yoyote haitahesabiwa kuwa ni kazi ya shuruti au kazi ya kikatili au ya kutweza endapo kazi hiyo, kwa mujibu wa sheria ni-

  • Kazi inayobidi ifanywe kutokana na hukumu au amri ya mahakama;
  • Kazi inayobidi ifanywe na askari wa jeshi lolote katika kutekeleza majukumu yao;
  • Kazi ambayo mtu yeyote inabidi aifanye kutokana na kuwapo hali ya hatari au baa lolote linalotishia uhai wa ustawi wa jamii
  • Kazi au huduma yoyote ambayo ni sehemu ya-
  • Majukumu ya kawaida ya kuhakikisha ustawi wa jamii;
  • Ujenzi wa taifa wa lazima kwa mujibu wa sheria;
  • Jitihada za taifa za kutumia uwezo wa kila mtu kufanya kazi kwa ajili ya kuimarisha jamii na uchumi wa taifa na kuhakikisha maendeleo na tija ya kitaifa’

Ufafanuzi

Kama Katiba ilivyoainisha kuwa yapo mazingira ambayo mtu au mwananchi anaweza kulazimika kufanya kazi fulani. Mazingira hayo yamebainishwa kwenye ibara ndogo kama zinavyoeleza. Hivyo muhimu kuzingatia mazingira ambayo yanaweza kukusababisha kufanya kazi za namna hiyo.

Hitimisho

Kama tulivyosisitiza kwenye makala zilizopita kuwa suala la kazi ni jambo la msingi sana ndio nguzo kuu ya maendeleo ya jamii yoyote hakuna mbadala wa kazi ila kufanya kazi. Wananchi tuzingatie kuhakikisha hakuna miungoni mwetu anayefanya kazi za shuruti au kudhalilishwa. Ikitokea hali hiyo ni vyema kuchukua hatua za kisheria. Hata hivyo hali hii haitoi mwanya kwa watu kukaa bila kazi bali kwa uhuru wao walio nao wautumie vyema kwa kufanya kazi halali.

 ‘usisubiri ushurutishwe kufanya kazi kwa sheria, chukua hatua fanya kazi yako’.

Kumbuka ‘kutokujua sheria si utetezi iwapo utatenda kosa lolote’ tafuta maarifa sahihi ya kisheria yakusaidie kufanya maamuzi sahihi kila siku. Wasiliana nami kupitia zakejr@gmail.com

Nakutakia siku njema sana ndugu yangu

Wako

Isaack Zake, Wakili