14. Usitishaji wa Ajira

Utangulizi

Ndugu msomaji wa makala za Uchambuzi wa Sheria ambapo tumekuwa tukiichambua Sheria ya Kazi, tumeendelea kuwa pamoja kwa kipindi chote hiki. Makala iliyopita tuliweza kuangalia kuhusu migomo mahala pa kazi na taratibu za kuzingatia ili mgomo uwe halali. Katika makala ya leo tunaanza kuangalia mfululizo wa makala za Usitishaji wa Ajira. Karibu tujifunze.

Maana ya Usitishaji wa Ajira

Usitishaji wa ajira una maana ya ukomo wa mkataba au mahusiano ya kiajira baina ya mwajiri na mfanyakazi.

Kama tulivyoeleza katika makala za awali kuwa mahusiano baina ya mwajiri na mfanyakazi na mahusiano ya mkataba uwe wa maandishi au wa mdomo. Sheria ya Ajira na Mahusiano kazini inatambua aina mbali mbali za mahusiano baina ya pande mbili yaani mkataba usio wa muda maalum, mkataba kwa kazi maalum na mkataba wa kipindi maalum. Kwa vyovyote vile mahusiano yote ya kimkataba yanafungwa kulingana na muda.

Zipo sababu nyingi zinazoweza kuchangia usitishwaji wa mahusiano ya kiajira baina ya mwajiri na mfanyakazi. Sababu hizo zinaweza kuwa ni za kimkataba, au sababu za mwajiri au zile za mfanyakazi. Sheria ya kazi inazianisha sababu zote hizi ili pande zote zipate kujua ni hatua gani za kuchukua katika kusitisha mahusiano ya kiajira.

Aina za Usitishaji wa Ajira

Kwa madhumuni ya kusaidia kuelewa dhana nzima jinsi Sheria ya Kazi inavyozungumza suala la usitishaji wa ajira, uchambuzi wa makala hizi zitajikita katika makundi makuu mawili ya aina za usitishaji wa ajira;

  • Usitishaji wa ajira wa halali
  • Usitishaji wa ajira usio halali

 

  1. Usitishaji wa ajira ulio halali

Hii ni aina ya usitishaji wa ajira ambao unazingatia sababu za msingi, utaratibu wa haki na kufutata matakwa ya Sheria ya Ajira. Kama tulivyobainisha kuwa mahusiano ya kiajira yanafungwa na ukomo wa muda, hivyo muda utakapokuwa umekamilika wa kiajira na taratibu zikafuatwa basi usitishwaji huo utakuwa wa halali. Katika ufafanuzi tutaangalia aina mbali mbali za sababu za usitishwaji wa ajira na taratibu za kisheria za kuzingatia.

  1. Usitishaji wa ajira usio halali

Hii ni aina ya usitishaji wa ajira ambao hauzingatii sababu za halali au utaratibu wa haki pamoja na matakwa ya Sheria ya Ajira. Yapo mazingira ambayo yanajitokeza ikiwa ni kwa kutokujua sheria au kwa makusudi usitishwaji wa ajira unajitokeza ambao hauzingatii matakwa ya kisheria. Kunapojitokeza aina hii ya usitishwaji wa ajira, mfanyakazi anayo haki ya kupinga usitishwaji huo kwa kupitia vyombo vilivyowekwa kwenye mfumo wa ajira mahali pa kazi au kwenda Tume ya Usuluhishi na Uamuzi.

Lazima nikiri kuwa kwa asilimia kubwa ya migogoro ya kazi iliyopo kwenye vyombo vya maamuzi inatokana suala la usitishwaji wa ajira. Hivyo kuna kila sababu ya kutoa elimu ya kutosha kusaidia wadau wote kuilewa sheria na kufuata miongozo ndani ya sheria ili kusaidia kupunguza migogoro isiyo ya lazima.

Hitimisho

Athari kubwa inayojitokeza kutokana na suala hili la usitishaji wa ajira kutokueleweka vizuri kwa wadau na kusababisha migogoro mingi ambayo inaathiri kwa kiasi kikubwa utendaji wa kazi na uzalishaji kwa ujumla. Muhimu sana kwa wadau, ikiwa ni Serikali, vyama vya wafanyakazi na jumuiya za waajiri, wafanyakazi na mawakili kuchukua hatua madhubuti kutoa elimu ya kutosha kusaidia kupunguza migogoro ili kuleta tija, manufaa na ufanisi mahala pa kazi.

Kumbuka ‘kutokujua sheria si utetezi iwapo utatenda kosa lolote tafuta maarifa sahihi ya kisheria yakusaidie kufanya maamuzi sahihi kila siku. Wasiliana nami kupitia zakejr@gmail.com

Nakutakia siku njema sana ndugu yangu

Wako

Isaack Zake, Wakili.

1 reply

Comments are closed.