Uhuru wa Kushiriki Shughuli za Umma

Utangulizi

Karibu sana ndugu msomaji na mfuatiliaji wa ukurasa huu kwenye mtandao wako wa www.ulizasheria.co.tz . Kama kawaida yetu lengo la kukuletea makala hizi fupi ni kukusaidia kuishi kwa mujibu wa sheria kila siku. Katika makala iliyopita tulijifunza juu ya Uhuru wa mtu kushirikiana na wengine. Leo tunaendelea na mfululizo makala juu ya haki mbali mbali za kibinadamu kama zilivyoanishwa kwenye Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Karibu tujifunze

Maana ya Uhuru wa Kushiriki shughuli za Umma

Katiba ya JMT inaeleza wazi kuwa kila mwananchi anao Uhuru wa kushiriki shughuli za umma. Ibara ya 21 (1) ya Katiba ya JMT inasema

Bila ya kuathiri masharti ya ibara ya 39,ya 47 na ya 67 ya Katiba hii na sheria za nchi kuhusiana na masharti ya kuchagua na kuchaguliwa, au kuteua na kuteuliwa kushiriki katika shughuli za utawala wa nchi, kila raia wa Jamhuri ya Muungano anayo haki, ya kushiriki katika shughuli za utawala wa nchi, ama moja kwa moja au kwa kupitia wawakilishi waliochaguliwa na wananchi kwa hiari yao, kwa kuzingatia utaratibu uliowekwa na sheria au kwa mujibu wa sheria’

Ufafanuzi

Kwa mujibu wa ibara hii ya katiba inaonesha kuwa kila mwananchi anayo haki ya kushiriki juu ya utawala wa nchi ikiwa ni moja kwa moja au kupitia uwakilishi.

 • Ushiriki wa utawala wa nchi moja kwa moja kama mwananchi ni kuhakikisha anatimiza wajibu wake kwa mujibu wa katiba na sheria kama raia wa Tanzania.
 • Ushiriki wa utawala wa nchi kwa uwakilishi ni kushiriki katika kuchagua wawakilishi katika ngazi ya Rais na Makamu wa Rais pamoja na wabunge ambao kwa niaba ya wananchi wanahusika na uendeshaji wa shughuli za kiserikali siku kwa siku.

Ibara ya 39 inaeleza juu ya sifa za mtu anazopaswa kuwa nazo ili kuchaguliwa kuwa Rais ambazo ni pamoja na kuwa raia wa kuzaliwa wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, mwenye umri kuanzia miaka 40 na ni mwanachama wa chama cha siasa aliyependekezwa n.k. hii inaonesha kuwa ikiwa yupo mwananchi amekidhi vigezo vya kuchaguliwa katika nafasi ya Rais au Makamu wa Rais au Mbunge basi mtu huyo anaweza kushiriki katika shughuli za utawala wa nchi.

Kwa kawaida Tanzania imekuwa na utaratibu wa mamlaka za kisiasa za nchi kuwekwa kwa njia ya uchaguzi ambao unafanyika kila baada ya miaka 5. Uchaguzi wa kwanza wa hivi karibuni mara baada ya kurudishwa mfumo wa vyama vingi ulikuwa mwaka 1995. Tangu wakati huo serikali zimekuwa zikibadilisha na madaraka kwa njia ya uchaguzi.

 

Hitimisho

Mwananchi anawajibika kufahamu wajibu wake wa kushiriki shughuli za nchi ikiwa ni moja kwa moja au kupitia uwakilishi. Ni muhimu kuhusika katika kujua namna shughuli za kiserikali zinavyoendeshwa na kuona ni kwa namna gani sera, sheria, kanuni na miongozo inavyotumika ili kuleta maendeleo. Kama wananchi hatupaswi kukaa pembeni na kulalamika kama mambo hayaendi tulivyotarajia kwani nasi tunao wajibu wa kutekeleza kwa nafasi yetu

 ‘una haki ya kushiriki shughuli za umma, usilalamike timiza wajibu wako’.

Kumbuka ‘kutokujua sheria si utetezi iwapo utatenda kosa lolote’ tafuta maarifa sahihi ya kisheria yakusaidie kufanya maamuzi sahihi kila siku. Wasiliana nami kupitia zakejr@gmail.com

Nakutakia siku njema sana ndugu yangu

Wako

Isaack Zake, Wakili

2 replies
  • ulizasheria
   ulizasheria says:

   karibu Alvin

   Ni kweli unachosema kwa sasa haki hii ya kuchaguliwa ni mpaka uwe mwanachama wa chama cha kisiasa. Hata hivyo historia ya kikatiba ya nchi hii inaonesha kuwa baada ya uhuru tulikuwa na vyama vingi na hata wagombea binafsi. Wakati vyama vingi vinarudi mwaka 1992 ndipo tafsiri juu ya haki ya mgombea huru ilianza kuleta shida. Tumeona juhudi kubwa alizofanya Marehemu Mch. Christopher Mtikila katika kufungua mashauri juu ya haki ya mgombea binafsi. Mpaka sasa Katiba inaruhusu mgombea kupitia chama cha siasa. Inawezekana huko baadae haki hii ikarudishwa kwenye Katiba kwa kadri inatakavyoonekana inafaa.

   Asante

Comments are closed.