Uhuru wa Mtu kushirikiana na wengine
Utangulizi
Karibu sana ndugu msomaji na mfuatiliaji wa ukurasa huu kwenye mtandao wako wa www.ulizasheria.co.tz . Kama kawaida yetu lengo la kukuletea makala hizi fupi ni kukusaidia kuishi kwa mujibu wa sheria kila siku. Katika makala iliyopita tulijifunza juu ya Uhuru wa mtu kuamini dini atakayo. Leo tunaendelea na mfululizo makala juu ya haki mbali mbali za kibinadamu kama zilivyoanishwa kwenye Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Karibu tujifunze.
Maana ya Uhuru wa Mtu kushirikiana na wengine
Katiba ya JMT inaeleza wazi kuwa kila mwananchi anayo Haki ya Uhuru wa kushirikiana na wengine. Ibara ya 20 (1) ya Katiba ya JMT inasema
‘kila mtu anao uhuru wa kukutana na watu wengine kwa hiari yake na kwa amani, kuchanganyika, kushirikiana na watu wengine, na kwa ajili hiyo kutoa mawazo yake hadharani na kuanzisha na kujiunga na vyama au mashirika yaliyoanzishwa kwa madhumuni ya kuhifadhi au kuendeleza imani au maslahi yake au maslahi mengineyo’
Haki hii inajumuisha watu kuungana kwa madhumuni ya kufanya ushirika ikiwa ni vyama vya siasa, au vyama vya kijamii au madhehebu. Uhuru huu wa kujiunga na vyama au ushirika fulani unahakikishwa Kikatiba.
Katika utekelezaji wa haki hii Katiba imeweka masharti ya kuzingatia ambapo marufuku imewekwa ikiwa vyama au ushirika unaanzishwa kwa malengo yafuatayo;
- Kukusudia kukuza au kupigania maslahi, imani au kundi lolote la dini, kundi la kikabila, ukanda, rangi au jinsia, au eneo Fulani katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
- Kupigania kuvunjwa kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
- Kinakubali au kupigania matumizi ya nguvu au mapambano kama njia ya kufikia malengo yake ya kisiasa
- Kinapigania au kinakusudia kuendesha shughuli zake za kisiasa katika sehemu moja tu ya Jamhuri ya Muungano
- Hakiruhusu uongozi wake kuchaguliwa kwa vipindi na kwa njia za kidemokrasia
Hakuna ushirika au chama kitakachoruhusiwa kuendesha shughuli zake kwa kuzingatia malengo hayo juu, kwa mujibu wa Ibara ya 20 (2) ya Katiba ya JMT.
Tanzania ni nchi ambayo inatambua mfumo wa vyama vingi katika uendeshaji wa shughuli za kisiasa. Vyama hivyo vinasajiliwa na Msajili wa Vyama vya Kisiasa na kuendesha shughuli zake kwa mujibu wa sheria ya Vyama vya Kisiasa.
Pia zipo jumuiya nyingi ambazo wananchi pasipo kujali itikadi, jinsia, makabila wanaungana ili kufanya shughuli zao iwe za kiuchumi, kijamii, kitamaduni na hata kidini. Zipo asasi zisizo za kiserikali, makampuni binafsi na makampuni ya umma, vyama vya ushirika na vya michezo n.k.
Hitimisho
Ni muhimu kutumia fursa hii ya kikatiba katika kuanzisha mahusiano mbali mbali ya kijamii na hata kiuchumi ili kusaidia ujenzi wa taifa lenye kujitegemea katika kila nyanja. Ni lazima kama wananchi tujue tulikotoka, tulipo na hasa kule tunapotaka kwenda kwa pamoja kama taifa. Nguvu ya umoja katika kutekeleza jambo lolote haijawahi kushindwa mahali popote. Tutumie nafasi ya kuunda ushirikiano kwa kuleta manufaa, tija na ufanisi.
‘wahenga walipata kusema umoja ni nguvu na utengano ni udhaifu’.
Kumbuka ‘kutokujua sheria si utetezi iwapo utatenda kosa lolote’ tafuta maarifa sahihi ya kisheria yakusaidie kufanya maamuzi sahihi kila siku. Wasiliana nami kupitia zakejr@gmail.com
Nakutakia siku njema sana ndugu yangu
Wako
Isaack Zake, Wakili